Mtoto wa mwenye timu amfuata Arteta

Muktasari:
- Arsenal imeshatupwa nje ya Kombe la Ligi na Kombe la FA, huku ikionekana kurusha taulo kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England, lakini ipo kwenye hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na usiku wa Jumanne ilikuwa na kibarua cha kukabiliana na Wadachi, PSV Eindhoven huko ugenini.
LONDON, ENGLAND: JOSH Kroenke, mtoto wa tajiri mmiliki wa klabu ya Arsenal amewasili London kwenda kukutana na kocha wa timu hiyo, Mikel Arteta kuzungumza namna msimu unavyokwenda kumalizika kwenye kikosi hicho.
Arsenal imeshatupwa nje ya Kombe la Ligi na Kombe la FA, huku ikionekana kurusha taulo kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England, lakini ipo kwenye hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na usiku wa Jumanne ilikuwa na kibarua cha kukabiliana na Wadachi, PSV Eindhoven huko ugenini.
Kwenye Ligi Kuu England, Arsenal kwa sasa imeachwa nyuma kwa pointi 13 na Liverpool kwenye kilele cha msimamo wa ligi hiyo. Kwa maana hiyo, eneo ambalo bado lina matumaini makubwa kwa Arsenal kushinda taji msimu huu ni kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, ambako pia mpinzani wake kwenye hatua ya 16 bora si timu ya kitoto, inacheza kijanja. Arteta anasumbuliwa na majeruhi wengi kwenye kikosi.
Sasa, Josh, 44, mtoto wa mmiliki wa klabu hiyo, bilionea Stan Kroenke, 77, aliwasili London kwenda kuzungumza na Arteta juu ya mechi ngumu zinazowakabili katika kipindi hiki cha kuelekea mwisho wa msimu.
Josh amekuwa bega kwa bega katika kuweka mambo sawa kwenye kikosi cha Arsenal na kuisaidia kwa misimu ya karibuni kuwa timu shindani kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England, ikimaliza kwenye nafasi ya pili kwa misimu miwili mfululizo iliyopita, kitu ambacho kinaweza kujitokeza tena msimu huu.
Baada ya Arsenal kuchapwa 1-0 na West Ham mwezi uliopita, Josh Kroenke hataki hilo liwe mwanzo wa timu hiyo kuporomoka zaidi na ndiyo maana ameripotiwa kwenda kuzungumza na kocha Arteta kuona kifanyike kitu gani katika kuirudisha timu hiyo kwenye njia zake za ushindi. Baada ya kipute cha PSV, mchezo ujao Arsenal itakabiliana na Manchester United kwenye Ligi Kuu England.