Mtoto wa Messi kama baba yake

FLORIDA, MAREKANI. NDIO! mtoto wa nyoka ni nyoka tu. Mateo Lionel Messi ambaye ni mtoto wa Messi ameanza kufuata nyayo za baba yake baada ya kuonyesha kiwango bora akiwa na timu ya vijana ya  Inter Miami  na amefunga mabao matano katika mechi moja.

Katika video mbalimbali, Mateo mwenye umri wa miaka minane alionekana akikokota mpira kwa umbali hadi akafika katika boski na kufunga bao.

Pia alifunga bao kupitia shuti la mbali lilitokana na mpira wa kutengwa na baada ya hapo akaenda kushangilia kwa ishara ya kubusu mashabiki staili ambayo baba yake aliwahi kuitumia mara kadhaa.

Kiwango chake kilionekana kuwa ni kukubwa zaidi ukilinganisha na wachezaji aliokuwa akicheza nao na katika mabao hayo matano alifunga kwa namna tofauti tofauti kuanzia mashuti ya mbali, faulo na kukokota na kupiga.

Mfano bao lake la tano alipiga chenga mabeki waliokuwa katika boski akakokota na kupiga shuti kali lilikwenda kuingilia katika kona ya goli.

Mateo ameingia katika anga za mtoto wa Cristiano Ronaldo, Ronaldo Jr ambaye ameanza kuonyesha kiwango bora kwa muda mrefu tangu akiwa Real Madrid ya watoto.

Kwa sasa ana umri wa miaka 13, na amekuwa mwiba katika timu zote alizopita na mbali ya Madrid, alicheza timu za vijana za Juventus na Manchester United kabla ya kutua Al Nassr ambako baba yake anacheza.