Mtoano UEFA ni mtihani mzito
Muktasari:
- Mbali ya timu nane za juu ambazo tayari zimeshafuzu kucheza 16 bora, kuanzia timu ya tisa hadi 24, zitacheza mechi mbili nyumbani na ugenini ili kutafuta nane nyingine zitakazokwenda 16 bora.
MADRID, HISPANIA: BAADA ya juzi kumalizika kwa hatua ya ligi ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, vigogo mbalimbali barani humo wamejikuta katika mtihani wa kucheza mechi za mtoano kuwania kufuzu hatua ya 16 bora ya michuano hiyo baada ya kumaliza katika nafasi za chini.
Mbali ya timu nane za juu ambazo tayari zimeshafuzu kucheza 16 bora, kuanzia timu ya tisa hadi 24, zitacheza mechi mbili nyumbani na ugenini ili kutafuta nane nyingine zitakazokwenda 16 bora.
Droo ya mechi hizo inatarajiwa kufanyika leo huko Nyon, Uswisi kuanzia saa 8:00 mchana.
Bingwa mtetezi Real Madrid ambayo imemaliza katika nafasi ya 11 kwenye msimamo wa ligi hiyo, kwenye hatua ya mtoano inaweza kukutana na aidha Celtic au Manchester City na ikishinda kwenda 16 bora itakuwa na uwezekano wa kuumana na Atletico Madrid na Bayer Leverkusen sawa na Bayern Munich ambayo pia inaweza kukutana na Man City au Celtic.
Vilevile PSG inaweza kupangwa na Monaco au Brest na ikipita inaweza kukutana na kati ya Liverpool au Barcelona kwenye 16 bora.
Kwa upande mwingne AC Milan na PSV Eindhoven zinaweza kuumana na Feyenoord na Juventus na mmoja wao akipita anaweza kuumana na Arsenal au Inter Milan.
Baada ya droo ya leo, mechi za mkondo wa kwanza zinatarajiwa kupigwa kuanzia Februari 11 hadi 12 kisha za mkondo wa pili zitaanza Februari 18 hadi 19.
Baada ya hapo itafanyika droo ya robo fainali, Februari 21, baada ya kumaliza kwa mechi hizo za mtoano na kupatikana kwa timu nyingine nane zitakazoungana na nane zilizofuzu moja kwa moja.
Kocha wa Manchester City, Pep Guardiola amekosoa mfumo mpya wa michuano hii ambao anaamini ndiyo umechangia timu nyingi kubwa kushindwa kumaliza nafasi nane za juu kwa sababu umeleta mechi nyingi.
“Ninachopenda, ukiwa kama mtazamaji utainjoi mfumo huu kwa sababu unakupa mambo mengi ambayo hayana uhakika, timu muhimu zinaweza kutolewa na ni jambo zuri. Tatizo ni tunacheza mechi nyingi zaidi Septemba, Oktoba, Novemba.”