Msako wa kocha Chelsea, Liam Rosenior anatajwa tajwa
Muktasari:
- Kwenye orodha ya makocha inaowasaka, mezani kunaripotiwa kuwapo na jina la Liam Rosenior, kocha wa klabu dada Strasbourg akidaiwa kuwa ndiye anayepewa nafasi kubwa ya kwenda kuchukua mikoba hiyo ya kuinoa The Blues huko Stamford Bridge.
LONDON, ENGLAND: CHELSEA ipo sokoni kwa sasa kusaka kocha mpya baada ya mshangao wa kufukuzwa kwa Enzo Maresca siku ya Mwaka Mpya 2026.
Kwenye orodha ya makocha inaowasaka, mezani kunaripotiwa kuwapo na jina la Liam Rosenior, kocha wa klabu dada Strasbourg akidaiwa kuwa ndiye anayepewa nafasi kubwa ya kwenda kuchukua mikoba hiyo ya kuinoa The Blues huko Stamford Bridge.
Kocha huyo wa zamani wa Hull City anaweza kuwa wa sita ndani ya miaka minne tangu bilionea Todd Boehly na mshirika wake Behad Eghbali wainunue Chelsea.
Iwapo Rosenior atachukua kazi hiyo, itakuwa hatua kubwa kutoka Strasbourg ya Ligue 1, huku uzoefu wake mwingine ukiwa ni kuinoa Hull City na Derby County kwa muda.
Hata hivyo, amewavutia Boehly na Eghbali akiwa Strasbourg, klabu ambayo pia inamilikiwa na kundi la Wamarekani chini ya kampuni ya Blue Co.
Mabadiliko ambayo Rosenior anaweza kupeleka Chelsea yatakuwa ya taratibu zaidi kuliko ya mapinduzi. Kama Maresca, anapendelea mfumo wa umiliki wa mpira, ujenzi wa mashambulizi kuanzia nyuma ukianzia kwa kipa.
Lakini, kuna tofauti muhimu za kiufundi. Maresca alikuwa akishikilia kwa ukakamavu mfumo wa 4-2-3-1. Rosenior, kwa upande mwingine, ameonyesha kupendelea mfumo wa 3-4-2-1 akiwa Strasbourg, ingawa mara nyingine ametumia 4-3-1-2.
Kwa kuzingatia udhaifu wa Chelsea katika ulinzi na matatizo ya kumalizia mashambulizi, mfumo huo unaweza kutoa msingi imara zaidi kwa wachezaji wanaopambana kama Cole Palmer.
Mfumo wa 3-4-2-1 ungewaruhusu Palmer na kipaji cha Brazil, Estevao kucheza nyuma ya mshambuliaji mmoja. Palmer atapewa uhuru kamili wa kucheza popote.
Rosenior atajenga mfumo mzima ili kumpa Palmer mpira katika maeneo ya kati ya uwanja (half-spaces). Palmer alicheza soka lake bora chini ya Mauricio Pochettino.
Chini ya Pochettino, Palmer alikuwa akigusa mpira wastani wa mara 65 kwa kila dakika 90.
Umuhimu wake ulikuwa mkubwa kiasi kwamba Chelsea waliitwa mara nyingi “Palmer FC†na mashabiki pinzani. Lakini chini ya Maresca, katika mfumo uliopangiliwa zaidi wa umiliki wa mpira unaohusisha mabeki wanaoingia katikati, Palmer amekuwa akigusa mpira kidogo zaidi, wastani wa mara 57 kwa dakika 90.
Mshambuliaji mkuu anaweza kuwa Joao Pedro, au Rosenior anaweza kuharakisha ujio wa mfungaji wa Strasbourg, Emmanuel Emegha. Rosenior alimfanya Emegha kuwa nahodha Strasbourg na amemsifu sana akisema: “Anawakilisha kila kitu ambacho timu inapaswa kuwa nacho, ubora, nguvu na kujitolea.”
Liam Delap pia atafurahia sana iwapo Rosenior atateuliwa.
Mshambuliaji huyo aliwahi kucheza chini yake huko Hull City alikokuwa kwa mkopo, akifunga mabao nane katika mechi 31. Rosenior alimpenda sana Delap amesema: “Ni wa kipekee na nampenda.”
Delap anaweza kuaminiwa tena kama mshambuliaji wa kati, hasa kwa kuwa Rosenior anapendelea Namba 9 mwenye nguvu na uchezaji wa moja kwa moja.
Hata hivyo, mfumo wake hauonekani kuwafaa sana winga kama Alejandro Garnacho, Pedro Neto na Jamie Gittens. Neto ameonyesha anaweza kucheza sehemu mbalimbali za mbele, lakini Gittens na Garnacho kwa kawaida hucheza pembeni.
Kiungo cha kati pia kitapata sura mpya, lakini misingi itaendelea kubaki ile ile. Ushirikiano wa viungo wenye thamani ya Pauni 220 milioni wa Moises Caicedo na Enzo Fernandez huenda ukaendelea kuwa moyo wa timu. Lakini kwa kuondolewa kwa mabeki wanaoingia katikati na kuanzishwa kwa wing-back, Fernandez hasa atalazimika kufanya kazi zaidi ya ulinzi.
Rosenior pia huenda asipende pasi ndefu za “Hollywood†za Enzo, akipendelea pasi fupi na za haraka. Iwapo Fernandez hatacheza kwa namna anayotaka kocha, nafasi yake inaweza kutishiwa na Andrey Santos. Ulinzi mpya wa watu watano unaweza kujumuisha Malo Gusto na Marc Cucurella kama wing-back wa asili, huku Reece James, Wesley Fofana na Trevoh Chalobah wakilinda mbele ya kipa Robert Sanchez.
Iwapo Rosenior atachagua mfumo wake mwingine wa 4-3-1-2, Palmer anaweza kucheza nyuma ya Joao Pedro na Liam Delap. Mfumo huo pia unaweza kumpa nafasi Andrey Santos kuimarisha nafasi yake kiungo pamoja na Caicedo na Fernandez. Kocha mpya pia anaweza kubadilisha namna Chelsea wanavyocheza bila mpira.
Watakaofaidika: Cole Palmer, Liam Delap, Estevao.
Wanaodhurika: Alejandro Garnacho, Enzo Fernandez, Jamie Gittens.