Mrithi wa Ten Hag aibukia Leeds

LONDON, ENGLAND. KOCHA wa zamani wa Ajax, Alfred Schreuder huenda akateuliwa kuwa kocha mkuu wa Leeds United kwa mujibu wa taarifa.

Schreuder atachukua mikoba ya Jesse Marsch aliyefukuzwa kazi kutokana na mwenendo mbovu wa timu wiki chache zilizopita.

Kocha huyo alifukuzwa kazi Ajax tangu mwezi uliopita na hakupata dili hadi Leeds ilipoonyesha nia ya kumbeba.

Inaelezewa kocha huyo alikuwepo uwanjani akishuhudia mchezo wa Ligi Kuu England, Leeds United ilipomenyana na Manchester United na kupokea kichapo cha mabao 2-0.

Schreuder alikuwa sambamba na wakala wake Milos Malenovic uwanjani Elland Road kabla ya kukutana na mtendaji mkuu wa Leeds. Taarifa zinadai huenda akatangazwa kabla ya mchezo unaofuata wa ligi dhidi ya Everton utakaochezwa wikiendi hii.

Awali, Leeds ilimtolea macho kocha wa Rayo Vallecano, Andoni Iraola, kabla ya kuhamia kwa Arne Slot anayeinoa Feyenoord ya Uholanzi hivi karibuni, lakini kote huko walikataliwa. Schreuder alichukua mikoba ya Erik ten Hag tangu Mei mwaka jana, lakini kutokana na mwenendo mbovu wa Ajax katika mechi za msimu huu mabosi walishindwa kumvumilia.

Ajax imeshindwa kupata ushindi tangu Oktoba, mwaka jana timu hiyo imekuwa ikiandamwa na matokeo ya sare mfululizo. Kwa sasa nafasi ya kocha huyo Ajax imechukuliwa na John Heitinga ambaye ameanza vizuri katika mechi mbili tangu alipochukua mikoba ya Schreuder.