Arsenal yaichapa Man United, ubingwa Premier kuamuliwa siku ya mwisho

Muktasari:
- Arsenal ikiwa ugenini imepata ushindi huo wa bao 1-0 uliotoa picha ya kwamba bingwa wa Premier League msimu huu atapatikana mechi ya mwisho.
BAO la Leandro Trossard dakika ya 20, limetosha kuipa ushindi Arsenal dhidi ya Manchester United katika mchezo wa Ligi Kuu England uliochezwa Uwanja wa Old Trafford.
Arsenal ikiwa ugenini imepata ushindi huo wa bao 1-0 uliotoa picha ya kwamba bingwa wa Premier League msimu huu atapatikana mechi ya mwisho.
Arsenal iliingia katika mchezo wa leo ikiwa nafasi ya pili kwenye msimamo nyuma ya Manchester City kwa tofauti ya pointi mbili, lakini ushindi huo umewarudisha kileleni baada ya kufikisha pointi 86 wakati wapinzani wao wakiwa na 85.
Hivi sasa Arsenal imebakiwa na mchezo mmoja kukamilisha msimu itakapocheza nyumbani dhidi ya Everton siku ya mwisho wa ligi, huku Man City ikibakiwa na mechi mbili dhidi ya Tottenham Hotspur Jumanne ijayo na West Ham United itakayopigwa Jumapili ya wiki ijayo.
Maombi makubwa kwa Arsenal hivi sasa ni kuona Man City ikizuiwa na ndugu zao hao wa London huku wao waifunge Everton siku ya mwisho na kubeba ubingwa ilioukosa kwa miaka 20 kwani mara ya mwisho waliubeba msimu wa 2003/04.
Katika mchezo wa leo, Arsenal iliweka rekodi kadhaa ikiwemo ya kutopoteza mechi yoyote dhidi ya 'big six' msimu huu baada ya kuifunga Man United nje ndani, huku ikishinda dhidi ya Chelsea, Man City, Liverpool na Tottenham, lakini pia imetoka sare na timu hizo katika mechi mojamoja.
Pia Arsenal imefanikiwa kukusanya clean sheet 18 katika mechi 37 huku ikishinda mechi 27 kati ya 37 zikiwa ni nyingi kwao kwa msimu mmoja.
Kipigo cha leo kwa United kinawafanya kukubali kufungwa na Arsenal nje ndani kwa mara ya kwanza tangu ilivyotokea msimu wa 2006/07.
Man United kwa sasa ipo nafasi ya nane kwenye msimamo ikiwa na pointi 54 ikiwa haina uhakika wa kushiriki michuano yoyote ya Ulaya msimu ujao.