Berkane yaipiga Zamalek, yausogelea ubingwa Shirikisho

Muktasari:

  • Katika mchezo huo wa fainali ya kwanza uliochezwa Uwanja wa Manispaa ya Berkane nchini Morocco, wenyeji RS Berkane walianza kwa kasi na kufanikiwa kupata bao la kwanza dakika ya 13 mfungaji akiwa Issoufou Dayo kwa mkwaju wa penalti.

RS Berkane imeukaribia ubingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 nyumbani dhidi ya Zamalek.

Katika mchezo huo wa fainali ya kwanza uliochezwa Uwanja wa Manispaa ya Berkane nchini Morocco, wenyeji RS Berkane walianza kwa kasi na kufanikiwa kupata bao la kwanza dakika ya 13 mfungaji akiwa Issoufou Dayo kwa mkwaju wa penalti.

Adil Tahif akaongeza bao la pili dakika 30 na kuifanya RS Berkane kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 2-0.

Kipindi cha pili, Zamalek walikuja kivingine na kufanikiwa kupata bao mapema tu dakika ya 46 kupitia Seifeddine Jaziri.

Mchezo wa marudiano wa fainali ya michuano hiyo ambayo huu ni msimu wa 21 inatarajiwa kufanyika Mei 19 mwaka huu kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Cairo uliopo Misri.

RS Berkane na Zamalek msimu huu katika michuano hiyo wamekuwa wababe wakimaliza vinara wa makundi yao huku wakicheza bila ya kupoteza hadi walipotinga fainali.

Katika mchezo huo wa marudiano, RS Berkane itaenda ugenini ikihitaji sare au ushindi wa aina yoyote kubeba ubingwa, wakati Zamalek ikifahamu kwamba ikipata ushindi wa bao 1-0 utatosha kuwa mabingwa kutokana na kuwa na mtaji wa bao la ugenini.