Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mrithi wa Ten Hag aanza kutajwa Old Trafford

Muktasari:

  • Huenda hilo likatokea baada ya mechi ya Jumapili, Man United itakapokwenda Villa Park kukipiga na Aston Villa. Hivyo ni Oktoba hii hii.

MANCHESTER, ENGLAND: SEHEMU ya kwanza ya sinema ya Manchester United Erik ten Hag lazima aondoke na hana muda mrefu ataondoka.

Huenda hilo likatokea baada ya mechi ya Jumapili, Man United itakapokwenda Villa Park kukipiga na Aston Villa. Hivyo ni Oktoba hii hii.

Kipigo kizito cha nyumbani Old Trafford kutoka kwa Tottenham Hotspur kilikuwa cha 10 kwa Man United kupoteza kwa mabao matatu au zaidi katika kipindi cha miaka miwili wakati timu hiyo ikiwa chini ya kocha huyo Mdachi, Ten Hag.

Man United ya Ten Hag si tu inapoteza mfululizo, bali inachapika mfululizo. Crystal Palace, Bournemouth, Brighton na Brentford ni miongoni mwa timu zilizopata matokeo ya ushindi mbele ya Man United.

Kucheza na Man United kwa sasa hivi haitishi tena, kitu ambacho huko nyuma wapinzani walikuwa wakihaha wakisikia kuna mechi ya Man United. Lakini, kwa sasa hivi, ratiba ya kucheza na Man United kila mtu anaitaka  timu hiyo imekuwa nyepesi mno kuikabili.

Imekuwa kawaida kwenye kipindi cha miaka 11 tangu alipoondoka Sir Alex Ferguson. Man United imebadili makocha sita ndani ya miaka 11, lakini Old Trafford pamekuwa mahali pepesiii kwenda kuchukua pointi.

Man United ilipokumbana na kipigo Jumapili, Gary Neville na Roy Keane walitoa maneno makali, huku kila mmoja alianza kuzungumzia hatima ya kocha Ten Hag ilipofika Jumatatu. Chini ya Ten Hag ambaye uwezo wake wa kuongoza ni mdogo siku mbaya zimeongezeka zaidi Man United.

Yalikuwa makosa makubwa kwa Sir Jim Ratcliffe na wasaidizi wake kutoka kampuni ya Ineos kuweka imani na kocha huyo wa zamani Ajax baada ya kushinda Kombe la FA msimu uliopita. Kisha ikaendelea kusajili kwa gharama kubwa wachezaji wengine wa Kiafrika.

Ratcliffe atakuwa ameshaelewa kwa sasa, hivyo haitachukua muda mrefu, Ten Hag atafunguliwa mlango uliandikwa ‘exit’.

Lakini, sehemu ya pili ya sinema hiyo, ambayo ni ngumu zaidi. Nani atakuja kuchukua mikoba? Kwa hali ilivyo, nani atataka kwenda kuinoa Man United?

Unai Emery hawezi kukubali kibarua cha kuinoa Man United - hawezi kujiripua. Man United ya sasa imekuwa timu ya nafasi za katikati kwenye msimamo. Ina wachezaji wengi wasiohitajika na imewasajili kwa pesa nyingi. Na bilionea Ratcliffe anachotaka kwa sasa ni kupunguza matumizi, hivyo hatamlipa pesa nyingi kocha ajaye. Kama hii klabu isingeitwa ‘Manchester United’, bilionea huyo bila shaka asingekubali kuwekeza.

Habari njema kwa Man United ni mkurugenzi wao mpya wa michezo, Dan Ashworth, yupo vizuri kwenye uchaguzi wa makocha.

Amefanya vizuri kwenye uteuzi wa makocha mara tatu alizofanya huko nyuma — kumteua Gareth Southgate kwenye kikosi cha England, Graham Potter kwenye kikosi cha Brighton na Eddie Howe katika kikosi cha Newcastle United. Anaweza kuamua vizuri juu ya kocha mpya wa Man United.

Kinachovutia ni Ashworth chaguo lake la kwanza alipokuwa Newcastle United alikuwa Unai Emery, ambaye alikataa na kubaki zake Villarreal, lakini imeonyesha alikuwa sahihi kutokana na kile anachofanya huko Aston Villa tangu alipotua Villa Park.

Na sasa Emery anaweza kuhitimisha maisha ya Ten Hag huko Man United, Jumapili  — hasa ukizingatia miamba hiyo ya Old Trafford haitakuwa na huduma ya nahodha wao Bruno Fernandes mwenye kati nyekundu na huenda isiwe na Kobbie Mainoo kutokana na kuumia.

Na kama atafanikiwa kuichapa Man United — kutakuwa na nafasi finyu kwake kuachana na Aston Villa, ambayo ipo kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya kwenda kukubali kibarua cha huko Old Trafford, kwa kipindi hiki, litakuwa anguko kwake.

Howe linaweza kuwa chaguo jingine zuri kumrithi Ten Hag, lakini shida Waarabu wa Saudi Arabia wanaweza wasiruhusu Ratcliffe amchukue na Howe pia baada ya kumchukua bosi wao Ashworth. Potter anapatikana kirahisi, lakini kwa kile alichofanya Chelsea na namna anavyoshindwa kufanya maamuzi magumu kwenye mechi ngumu, hilo litamnyima nafasi ya kupata kazi Old Trafford. Kitu ambacho kitamfanya Southgate apate kazi Man United ni ukaribu wake na Ashworth, lakini kingine ni uwezo wake wa kuongoza na ndiyo Man United ilipigania nafasi ya kumchukua mwishoni mwa msimu uliopita.

Mauricio Pochettino, ambaye alihusishwa na Man United mara kadhaa, ameondoka kwenye mpango baada ya kuchukua kibarua cha kuinoa Marekani. Thomas Tuchel linaweza kuwa chaguo maarufu, lakini licha ya ubora wake kama kocha, anatazamwa kama amepoteza makali. Kuna Roberto De Zerbi, yupo Marseille kwa sasa baada ya kufanya vizuri Brighton. Kieran McKenna — kocha wa zamani wa Man United yupo Ipswich Town — amafaa, lakini si kwa sasa.

Marco Silva, hapewi nafasi kubwa akiwa anainoa Fulham, aliwahi kuwekwa kwenye rada za Man United, lakini kwa sasa hajadiliwi. Kocha wa Sporting Lisbon, Ruben Amorim, alikuwa gumzo msimu uliopita, alikoswa na West Ham na Liverpool, hivyo si mtu unayeweza kumpata kirahisi.

Zinedine Zidane, ni kocha mzuri, lakini si aina ya watu ambao Ashworth anawataka. Ruud van Nistelrooy, mtambo wa mabao wa zamani wa Man United yupo kwenye benchi la Ten Hag akimsaidia kocha huyo na kama mabadiliko yatafanyika, basi anaweza kuwa kocha wa kipindi cha mpito.

Kwa machaguo yaliyopo kwa sasa na mwenendo wa Man United ulivyo, ishu ya kumfuta Ten Hag si kitu kigumu kabisa kukifanya kwa kipindi hiki.

Kwa bilionea Ratcliffe, Ashworth na mabosi wengine kwenye kikosi cha Man United, sehemu ngumu zaidi kwenye sinema yao ni nini kitakachofuata?

Chochote kitakachoamriwa, wanahitaji kukitafakari kwa umakini mkubwa.