Mrithi wa Edu kuleta mavitu ya Atletico Madrid

Muktasari:
- Washika mitutu hao wa London inadaiwa wamefikia makubaliano na mkurugenzi wa zamani wa michezo wa Atletico Madrid, Andrea Berta aliyeachana na klabu hiyo januari mwaka huu.
LONDON, ENGLAND: HATIMAYE baada ya mchakato wa muda mrefu wa kumsaka mrithi wa nafasi ukurugenzi wa michezo wa klabu ya Arsenal, iliyokuwa ikishikiliwa na Edu, sasa amepatikana.
Washika mitutu hao wa London inadaiwa wamefikia makubaliano na mkurugenzi wa zamani wa michezo wa Atletico Madrid, Andrea Berta aliyeachana na klabu hiyo januari mwaka huu.
Berta aliondoka Atletico ikiwa ni baada ya miaka 12 na amekuwa katika mazungumzo na viongozi wa juu wa Arsenal tangu wakati huo na walionyesha kuvutiwa na kazi nzuri aliyoifanya akiwa miamba hiyo ya Hispania hadi kuifanya kuwa timu shindani dhidi ya vigogo Real Madrid na Barcelona licha ya ukubwa wa timu hizo.
Mbali ya Atletico, Berta pia amewahi kuhudumu katika nafasi hiyo katika timu za Parma na Genoa za Italia.
Berta aliisaidia Atletico kupata mafanikio makubwa kuanzia ligi ya ndani na michuano ya kimataifa na katika kipindi chake, timu hiyo ilishinda mataji mawili ya La Liga, Europa League na kumaliza kama washindi wa pili wa Ligi ya Mabingwa Ulaya mara mbili.
Pia alinunua na kuuza nyota kama Antoine Griezmann na Rodri kwa kiasi kikubwa cha fedha na msimu uliopita alitumia Pauni 180 milioni kuwanunua Julian Alvarez, Conor Gallagher, Robin Le Normand na Alexander Sorloth ili kuimarisha tena kikosi cha Diego Simeone.
Edu aliondoka Emirates Novemba mwaka jana na inadaiwa alipata dili la kuwa mkurugenzi wa timu zinazomilikiwa na tajiri Evangelos Marinakis.
Moja ya timu zilizoko chini ya tajiri huyo ni Nottingham Forest ambayo imekuwa kivutio Ligi Kuu England msimu huu.