Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mpango wa Villarreal vs Barcelona kuchezwa Marekani wafutwa

Muktasari:

  • Taarifa ya Relevent, iliyochapishwa kwanza na The Athletic Jumanne jioni Oktoba 21, 2025 imesomeka: “Relevent imeiarifu La Liga kuhusu haja ya kuahirisha mpango wa mechi kati ya Villarreal CF na FC Barcelona jijini Miami tarehe 20 Desemba.

MADRID, HISPANIA: Mechi ya La Liga kati ya Villarreal na Barcelona iliyokuwa ichezwe jijini Miami imeahirishwa, huku waandaaji wa tukio hilo, Relevent, wakisema hakuna muda wa kutosha kuandaa hafla hiyo.

Taarifa ya Relevent, iliyochapishwa kwanza na The Athletic Jumanne jioni Oktoba 21, 2025 imesomeka: “Relevent imeiarifu La Liga kuhusu haja ya kuahirisha mpango wa mechi kati ya Villarreal CF na FC Barcelona jijini Miami tarehe 20 Desemba.

“Kutokana na hali ya kutokuwa na uhakika nchini Hispania, hakuna muda wa kutosha wa kutekeleza tukio la ukubwa huu ipasavyo. Pia itakuwa ni kutowajibika kuanza kuuza tiketi bila uhakika wa mechi kuthibitishwa.”

Relevent Sports, kampuni ya haki za matangazo na matukio iliyoanzishwa na kumilikiwa na bilionea Stephen M. Ross, mmiliki wa timu ya Miami Dolphins, ina ushirikiano na La Liga kukuza soko la ligi hiyo Amerika Kaskazini. Mechi hiyo ilikuwa ifanyike kwenye uwanja wa Hard Rock, Miami Gardens, Florida.

Ingawa Relevent waliita mechi hiyo imeahirishwa, taarifa ya La Liga yenyewe imesema uamuzi umefikiwa kufuta tukio hilo, na kuongeza kuwa ligi hiyo inasikitika sana kuhusu habari hizo, ikieleza ni pigo kwa taswira ya kimataifa ya ekosistemu nzima ya soka.

“La Liga inatangaza kwamba, kufuatia mazungumzo na mwandaaji wa mechi rasmi ya La Liga jijini Miami, uamuzi umefikiwa kufuta maandalizi ya tukio hilo kutokana na hali ya kutokuwa na uhakika iliyojitokeza nchini Hispania katika wiki za hivi karibuni,” imesomeka taarifa ya ligi hiyo.

“La Liga inasikitika kwamba mradi huu, ambao ungekuwa fursa ya kihistoria na ya kipekee ya kimataifa kwa soka la Uhispania, hauwezi kuendelea.

“Kucheza mechi rasmi nje ya mipaka yetu kungekuwa hatua muhimu katika upanuzi wa kimataifa wa mashindano yetu, na kungeimarisha uwepo wa klabu, wachezaji na chapa ya soka la Kihispania katika soko muhimu kama Marekani.”

La Liga imeongeza kuwa mradi huo ulizingatia kikamilifu kanuni za shirikisho na haungeathiri uadilifu wa mashindano, ila ulipingwa kwa sababu nyingine.

Taarifa hiyo pia imesema kwamba kukosa fursa kama hizi kunapunguza uwezo wa ligi kuzalisha mapato mapya, kuwekeza, na kushindana kimataifa.

Agosti 2025, Shirikisho la Mpira wa Miguu Hispania (RFEF) lilikubali ombi la La Liga la kuruhusu mechi ya Desemba 2025 kati ya Villarreal na Barcelona kuchezwa Miami.

Awali, mechi hiyo ilikuwa ichezwe kwenye uwanja wa nyumbani wa Villarreal, Estadio de la Cerámica, mashariki mwa Hispania, Desemba 20 au 21, 2025.

Kama ingefanyika, ingekuwa mara ya kwanza kwa mechi ya ligi kuu ya Ulaya kuchezwa Marekani, ingawa Kombe la Super la Hispania limekuwa likifanyika Saudi Arabia katika misimu minne kati ya mitano iliyopita.

Mnamo Oktoba 6, 2025, UEFA iliidhinisha ligi za Hispania na Italia kucheza mechi za ndani nje ya nchi katika uamuzi wa kihistoria, lakini ikasisitiza upinzani wake wazi dhidi ya mpango huo, ikisema ruhusa hiyo ilitolewa kwa misingi ya kipekee kutokana na mapungufu ya kisheria duniani.

Rais wa UEFA, Aleksander Ceferin, aliuita uamuzi huo wa kusikitisha na akaonya kuwa usitafsiriwe kama mfano, akisisitiza kuwa mechi za ligi zinapaswa kuchezwa katika ardhi ya nyumbani.

Wakati huohuo, Serie A (Ligi Kuu ya Italia) inapanga kuandaa mechi kati ya AC Milan na Como nchini Australia, mazungumzo yanaendelea kuhusu uwezekano wa mechi hiyo kuchezwa mjini Perth mnamo Februari 7–8, 2026.

Mpango wa La Liga ulikumbana na upinzani mkali, hasa kutoka kwa mashabiki. Mashirikisho ya mashabiki wa Villarreal, Barcelona, na Chama cha Mashabiki wa Soka Hispania (FASFE) yalitoa tamko la kupinga kwa ukamilifu, uthabiti na msimamo mkali mpango huo.

Mwisho wa wiki iliyopita, timu za La Liga zilichelewesha kuanza mechi kwa sekunde 15 za mwanzo kama ishara ya kupinga mpango huo, baada ya Chama cha Wachezaji wa Hispania (AFE) kusema wachezaji hawakuridhishwa na mpango wa kucheza Miami.Hata hivyo, televisheni hazikuonyesha wazi matukio hayo baada ya La Liga kuomba zisionyeshe sekunde hizo 15 za mwanzo, kulingana na vyanzo kadhaa.

Katika mechi za Oviedo na Barcelona, kamera zilionyesha mandhari ya nje ya viwanja kabla ya kurejea uwanjani mechi zilipoanza. Kwenye mechi zingine, kamera za juu zilionyesha duara la katikati pekee badala ya wachezaji wote waliokuwa wamesimama bila kufanya kitu.

Real Madrid iliomba FIFA kuzuia mechi hizo kuchezwa Miami, ikisema mpango huo unadhoofisha uadilifu wa La Liga na unaweza kuwa mgeuko usiopendeza katika dunia ya soka.

Kamishna wa Umoja wa Ulaya anayehusika na haki kati ya vizazi, vijana, utamaduni na michezo, Glenn Micallef, amesema kuhamishia mechi hiyo nje ni usaliti kwa jumuiya za klabu za Kihispania na akatoa wito wa kufanyika kwa majadiliano ya pamoja kuhusu suala hilo na mengine tata katika soka.

La Liga kwa mara ya kwanza ilijaribu kuandaa mechi nje ya nchi mwaka 2018, kwa kupendekeza mechi ya Girona dhidi ya Barcelona ichezwe Miami, mpango uliopingwa na RFEF na FIFA. Pendekezo lingine la mwaka uliofuata kwa mechi ya Atlético Madrid dhidi ya Villarreal pia lilikataliwa.

Tangu wakati huo, uhusiano kati ya La Liga na RFEF umeimarika, na uwezekano wa mechi za ligi kuchezwa nje ya nchi umeongezeka baada ya FIFA kuondolewa katika kesi ya kihistoria iliyofunguliwa na Relevent mnamo Aprili 2024.