Mpango wa Cristiano Ronaldo kwenda India umeshindikana
Muktasari:
- Taarifa kutoka Saudia zinaeleza kuwa, Ronaldo, hatakuwa sehemu ya kikosi kitakachosafiri kwenda India kwa ajili ya mechi hiyo itakayopigwa keshokutwa Jumatano, Oktoba 22, 2025 kwenye Uwanja wa Pandit Jawaharlal Nehru.
Mpango wa mashabiki na uongozi wa mji wa Goa nchini India wa kutaka kumuona Cristiano Ronaldo akitua mjini humo kwa ajili ya mechi ya Ligi ya Mabingwa Asia (AFC Champions League Two) dhidi ya FC Goa, umegonga mwamba, baada ya kuthibitika mshambuliaji huyo hatasafiri na kikosi cha Al Nassr.
Taarifa kutoka Saudia zinaeleza kuwa, Ronaldo, hatakuwa sehemu ya kikosi kitakachosafiri kwenda India kwa ajili ya mechi hiyo itakayopigwa keshokutwa Jumatano, Oktoba 22, 2025 kwenye Uwanja wa Pandit Jawaharlal Nehru.
Awali mashabiki na uongozi wa mji wa Goa uliripotiwa kujipanga kwa ajili ya kumuwekea ulinzi maalum mshambuliaji huyo kutoka nchini Ureno, ili kuushawishi uongozi wa Al Nassr kuridhia Ronaldo awe sehemu ya wachezaji watakaosafiri kwa ajili ya mechi hiyo.
Al Nassr inajiandaa kwa mechi yao ya tatu ya Ligi ya mabingwa Asia (AFC Champions League Two), baada ya ushindi mnono dhidi ya Al-Fateh kwenye ligi ya Saudi Arabia, juzi Jumamosi Oktoba 18, 2025.
Hata hivyo, taarifa kutoka kwa chanzo cha klabu hiyo kupitia mtandao wa X (zamani Twitter) imefichua kuwa nahodha wa timu hiyo amepewa ruhusa kutosafiri katikati ya wiki.
Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 40, hatakuwa sehemu ya kikosi kitakachocheza kwenye Uwanja wa Pandit Jawaharlal Nehru mjini Goa jambo ambalo limekuwa la kawaida katika mashindano haya kwa Al-Nassr msimu huu.
Ronaldo bado hajacheza mechi yoyote ya AFC Champions League Two msimu huu, hali ambayo iliwaibua mashabiki na uongozi wa mji wa Goa kuonyesha hisia za kutaka kumuona mshambuliaji huyo akisafiri na timu yake hadi India.
Cristiano Ronaldo hajajumuishwa kwenye kikosi cha siku ya mechi kwa upande wa Al-Nassr (Knights of Najd) katika mashindano ya AFC Champions League Two, ngazi ya pili ya mashindano ya klabu barani Asia. Hata hivyo, kikosi cha Jorge Jesus kimeshinda mechi zote mbili dhidi ya Istiklol na Al-Zawraa bila ya kumtegemea mshambuliaji huyo maarufu.
Ronaldo amefunga mabao matano katika mechi tano za Ligi Kuu ya Saudi Arabia msimu huu, lakini hajashiriki kwenye mashindano mengine hadi sasa.
Al-Nassr imeshafunga mabao saba katika mashindano ya AFC Champions League Two bila kuruhusu bao lolote, ikionesha kiwango cha juu tangu kuanza kwa michuano hiyo.
FC Goa imepoteza mechi zote mbili katika mashindano hayo msimu huu dhidi ya Al-Zawraa na Istiklol bila kufunga bao lolote. Mashabiki wao walikuwa na matarajio ya kumuona Ronaldo akiwasili Goa, lakini inaonekana wazi kuwa hataweza kushiriki mechi za hatua ya makundi.