Mourinho apigwa rungu Uturuki

Muktasari:
- Kocha huyo Mreno alitoa maneno baada ya mechi dhidi ya Galatasaray, aliposema mbele ya waandishi wa habari kwamba beki la wapinzani katika mechi hiyo "walirukaruka kama nyani".
ISTANBUL, UTURUKI: JOSE Mourinho amekutana na adhabu ya kufungiwa mechi nne na kupigwa faini ya Pauni 35,000 baada ya kocha huyo wa Fenerbahce kutoa kauli iliyozua utata dhidi ya wapinzani wake.
Kocha huyo Mreno alitoa maneno baada ya mechi dhidi ya Galatasaray, aliposema mbele ya waandishi wa habari kwamba beki la wapinzani katika mechi hiyo "walirukaruka kama nyani".
Galatasaray ilitafsiri hayo maneno kama ubaguzi wa rangi na kutishia kumfungulia mashtaka.
Mourinho alisema mechi hiyo ilikuwa nzuri kwa sababu haikuchezeshwa na refa Mturuki, ikiwa ni kuendelea na malalamiko yake juu ya ubora wa waamuzi kwenye Super Lig na huko nyuma alisema asingekubali kuinoa Fenerbahce kama angefahamu mapema hakuna usawa kiasi hicho.
Mwamuzi wa Slovenia, Slavko Vincic alialikwa kuchezesha mechi hiyo ya mahasimu wawili wakubwa kwenye soka la Uturuki.
Kiwango cha mwamuzi huyo kilisifiwa na refa Mourinho na mechi hiyo ilimalizika kwa matokeo ya 0-0 na kadi za njano saba zilionyeshwa. Mourinho alisema mambo yangekuwa mabaya kama refa angekuwa Mturuki.
Kauli zake hizo mbili ndizo zilizomfanya apigwe faini na kufungiwa mechi mbili, kitu ambacho kwa jumla yake na kosa la mwanzo, kocha huyo wa zamani wa Chelsea na Manchester United atafungiwa mechi nne.