Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mokoena aiponza Afrika Kusini, yapokwa pointi kufuzu Kombe la Dunia 2026

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa taarifa ya Kamati ya Nidhamu ya FIFA, Afrika Kusini ilimchezesha Mokoena kinyume na kanuni katika mechi iliyozikutanisha taifa hilo dhidi ya Lesotho, Machi 21, 2025.

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu la Kimataifa (FIFA) limekiadhibu Chama cha Mpira wa Miguu Afrika Kusini (SAFA) kwa kosa la kumchezesha Teboho Mokoena katika mechi ya kufuzu Kombe la Dunia 2026 wakati hakuwa na sifa kikanuni.

Kwa mujibu wa taarifa ya Kamati ya Nidhamu ya FIFA, Afrika Kusini ilimchezesha Mokoena kinyume na kanuni katika mechi iliyozikutanisha taifa hilo dhidi ya Lesotho, Machi 21, 2025.

Nyota huyo alianza kikosi cha kwanza na kutumika kwa dakika 82 katika mechi hiyo ambayo Afrika Kusini ilishinda 2-0, licha ya kwamba alipaswa kutumikia adhabu ya kusimamishwa kutokana na kadi mbili za njano alizopata mechi dhidi ya Benin iliyochezwa Novemba 2023 na Zimbabwe Juni 2024.

Kanuni za kinidhamu za FIFA zinasema: “Iwapo timu itamchezesha mchezaji ambaye hana sifa za kushiriki (kwa sababu ya kufungiwa, matatizo ya usajili, uraia, n.k.), mchezo huo utahesabiwa moja kwa moja kuwa umepotezwa. Matokeo ya kawaida ni kichapo cha mabao 3–0, isipokuwa kama matokeo halisi yalikuwa mabaya zaidi kwa timu husika.”

Awali, Bafana Bafana ilikuwa ikiongoza Kundi C ikiwa na pointi 17, Benin ikifuatia kwa pointi 14, huku Nigeria na Rwanda zikiwa na pointi 11 kila moja. Kwa mujibu wa uamuzi wa FIFA, matokeo ya mchezo huo dhidi ya Lesotho yametangazwa kuwa yamefutwa na kuhesabiwa ushindi wa mabao 3–0 kwa Lesotho.

Adhabu hiyo inamaanisha kuwa, Afrika Kusini itapokwa pointi tatu na kubaki na pointi 14, sawa na Benin. Hatua hiyo imeufanya ushindani katika Kundi C kuwa wazi zaidi kwa Benin, Nigeria na Rwanda, kwani kila moja bado ina nafasi ya kufuzu kutokana na michezo miwili iliyosalia.

Mbali na kupokwa pointi, SAFA pia imepigwa faini ya takribani Sh30.4 milioni za Tanzania. Aidha, Mokoena amepewa onyo kali.

Kwa mujibu wa FIFA, pande husika zina siku kumi kuomba ufafanuzi wa kina au kukata rufaa, ingawa uamuzi wa kufuta matokeo ya mchezo huo utaendelea kusimama hadi pale rufaa itakaposikilizwa.

Kwa kuondolewa pointi hizo, Benin sasa ina matumaini makubwa ya kufuzu, huku Nigeria na Rwanda pia zikipewa nafasi kubwa ya kupigania tiketi ya moja kwa moja au kupitia hatua ya mchujo. Kila timu bado inapigania pointi sita katika michezo miwili ya mwisho.

Waziri wa Michezo, Sanaa na Utamaduni wa Afrika Kusini, Gayton McKenzie, amethibitisha kupokea taarifa ya adhabu hiyo na kusema kuwa ni tukio la fedheha kwa taifa na kwa mchezo wa soka.

Katika taarifa iliyotolewa Septemba 29, 2025, Serikali ya Afrika Kusini imesema: “Tukio hili ni la kusikitisha sana na limeiletea fedheha nchi yetu na mchezo wa soka. Tunatambua makosa yaliyotokea na tunawajibika kuhakikisha suala hili linashughulikiwa.”

Hata hivyo, Waziri McKenzie amesisitiza kuwa bado wana imani kubwa kwa kikosi cha Bafana Bafana na watahakikisha timu inaandaliwa ipasavyo kwa michezo miwili ijayo muhimu itakayopigwa Durban na Mbombela.

Ameongeza kuwa, serikali itafuatilia kwa karibu ili kubaini chanzo cha tukio hili na kuhakikisha halijirudii.

“Tumefanya kitu kibaya, tumefanya jambo ambalo hatukutakiwa kufanya, lakini hakukuwa na malalamiko,” amenukuliwa kocha mkuu wa Afrika Kusini, Hugo Broos, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari Septemba 2025 kupitia ESPN.

Benin walikuwa watu wa kwanza kubaini tukio hilo ambapo Kocha wao, Gernot Rohr, alinukuliwa na vyombo vya habari vya ndani akisema: “FIFA sasa inapaswa kutoa uamuzi haraka sana.”

Ikumbukwe kuwa, katika kufuzu Kombe la Dunia 2026, vinara wa kila kundi katika makundi tisa barani Afrika watafuzu moja kwa moja michuano hiyo.

Timu zitakazomaliza nafasi ya pili zikiwa na alama nyingi zaidi katika makundi hayo tisa, zitashiriki hatua ya mchujo maalum. Timu moja tu kati ya hizo ndiyo itakayopata nafasi ya ziada ya kufuzu kwenye michuano hiyo.

Afrika Kusini itakutana na Zimbabwe Oktoba 10, na Rwanda Oktoba 14, wakati Benin itakutana na Rwanda Oktoba 10 na Nigeria Oktoba 14. Nayo Nigeria itachuana na Lesotho Oktoba 10.