Mo Salah apandisha watu presha

Wednesday April 07 2021
mo salah pc

LIVERPOOL, ENGLAND. PRESHA inapanda, presha inashuka huko Anfield. Shida kubwa inasababishwa na wasiwasi kuhusu hatima ya supastaa matata Mohamed Salah kwamba anataka kwenda kukabiliana na changamoto mpya kwingineko.

Kwa mujibu wa ESPN, hali ya kwenda vyumba vya kubadilishia huko Anfield imejaa wasiwasi kwa sababu tu supastaa huyo wa Misri anataka kuondoka.

Tayari kumekuwa na maelezo kutoka kwa watu wa karibu na staa huyo kwamba suala la kuhama kwa pesa nyingi kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi lina uwezekano wa kutimia.

Salah, 28, amekuwa na kiwango bora miaka minne aliyokipiga Liverpool na msimu huu ameshafunga mabao 18 tayari licha yakikosi chake kushindwa kutetea ubingwa wa Ligi Kuu England.

Mkataba wa staa huyo huko Anfield utafika tamati 2023, lakini kama watashindwa kufuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao, basi kuna uwezekano mkubwa wakapoteza pia huduma ya staa huyo.

Kikosi hicho cha kocha Jurgen Klopp kimesogea na sasa kipo pointi mbili tu nyuma ya kuifikia Top Four baada ya kuwachapa Arsenal Jumamosi na wamepata nafuu kubwa baada ya Chelsea kuchapwa na West Brom.

Advertisement

Mo Salah alifunga bao katikati ya mabao mawili ya Diogo Jota kuipa Liverpool ushindi wa mabao 3-0, huku ikiwa ni ushindi wao wa pili mfululizo baada ya kuanza mwaka huu wa 2021 vibaya kwenye Ligi Kuu England.

Kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa msimu huu mambo yao si mabaya sana, wakifika robo fainali ambapo wakabiliwa na Real Madrid katika mechi ya kwanza itakayopigwa leo Jumanne uwanjani Bernabeu.

Real Madrid na Barcelona zimekuwa zikihusishwa na staa huyo na zitakuwa tayari kuweka ofa ya Pauni 100 milioni mezani kunasa huduma yake huku mchezaji mwenyewe akiweka milango wazi ya kwenda La Liga kwa siku za baadaye.

Advertisement