Mnyama Haaland huyoo anatua England

Muktasari:

SI unajua Pep Guardiola na Mino Raiola picha haziendi? Kuna ishu sasa hapa inaibuka, itakuwaje kuhusu mpango wake wa kumchukua straika wa mabao, Erling Haaland.

LONDON, ENGLAND

NI leo Jumanne, pale Pep Guardiola atakapokutana na mchezaji aliyeliteka soko la dunia la usajili kwa kuwa saini yake inawaniwa na timu zote kubwa barani Ulaya.

Huyu ni Erling Haaland ambaye kwake kukanyaga ardhi ya England itakuwa ni kurejea kwenye ardhi ambayo alizaliwa lakini wakati huu atakuwa amekuja kwa ajili ya tukio la kuitumikia Borussia Dortmund kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa hatua ya robo fainali dhidi ya vijana wa Pep Guardiola.

Lakini stori kubwa imekuwa sio mechi anayokwenda kuchezwa, ishu ni jinsi anavyosumbua kwenye soko la usajili ambapo yeye na staa wa Paris Saint-Germain, Kylian Mbappe wanaonekana kuwa ni Lionel Messi na Cristiano Ronaldo wajao, wakitabiriwa kutawala soka la dunia kwa zaidi ya miaka 10 ijayo.

Haaland amekuwa gumzo sana kuelekea dirisha lijalo la majira ya kiangazi wakati wakala wake Mino Raiola akiendelea kuwaweka watu njia panda kutokana na mazungumzo yake anayofanya na timu mbali mbali.

Hata hivyo, taarifa zinasema Haaland ana asilimia nyingi zaidi za kujiunga na moja ya timu nchini England kutokana na sababu nyingi ikiwamo kuzaliwa kwake nchini humo.

Jan Age Fjortoft, ambaye ni mtu wa karibu wa familia ya Haaland akiwa ni mmoja ya marafiki wa muda mrefu mdingi wa staa huyo, Alfe-Inge, anaelezea hali ilivyo juu ya uwezekano wa mchezaji huyo kujiunga na moja kati ya timu za England kwenye dirisha lijalo la majira ya kiangazi.

“Kuna asilimia nyingi sana za kujiunga na moja ya timu ndani ya England kwa sababu unajua Haaland alizaliwa Leeds na akakulia hapo, hivyo ana vinasaba vya England na naamini atapenda kucheza soka nchini humo

“Nafahamu kwamba klabu zinazoonekana zinamuhitaji katika dirisha hili, ziliwahi kuwasilisha ofa wakati anaichezea Salzburg lakini kutokana na ushauri wetu ilibidi ajiunge na Dortmund. kwa sababu tuliamini angeenda kukua zaidi, hivyo licha ya kuangalia upande wa maslahi dhumuni kubwa huwa ni kuona anajiunga na timu ambayo itamfanya akue kiwango siku hadi siku.”

Wiki ya juzi Raiola na baba mzazi wa Haaland, Alfe-Inge walikutana na wawakilishi wa Barcelona na Real Madrid ili kusikiliza ofa zao kwa ajili ya Haaland na baada ya hapo Raiola na Alfe-Inge walifunga safari hadi England kisha wakafanya mazungumzo na wawakilishi wa Manchester United, Man City na Chelsea.

Kati ya timu zote hizo Manchester City ndio inaonekana kuwa na nafasi kubwa ya kuipata saini yake kwa sababu ya kiwango chao kwenye ligi na uhitaji wao wa mshambuliaji kwani ipo kwenye mpango wa kumsaka mrithi wa Sergio Aguero ambaye ataondoka mwisho wa msimu.

Ingawa Pep Guardiola amefunguka kwamba hawana mpango wa kutafuta mbadala wa Aguero, inaaminika ni janja yao tu kwenye kuzilemaza timu nyingine kisaikolojia lakini ukweli ni kwamba wana uhitaji sana na Haaland.

Hata hivyo, Dortmund haionekani kuwa tayari kumuuza fundi huyo ambaye mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwaka 2024, lakini kiasi kikubwa cha pesa kutoka moja ya klabu hizo nne kinaweza kubadilisha msimamo wao.

Uwezekano wa Haaland kuondoka Dortmund unatajwa kuwa ni asilimia zaidi ya 90 kwa sababu kwenye mkataba wake kuna kipengele kinachoruhusu timu inayomuhitaji kutoa Euro 75 milioni ifikapo dirisha la majira ya kiangazi la mwakani ili kuinasa yake.

Hivyo, ikiwa Dortmund itagoma kumuuza katika dirisha lijalo itapata hasara ya kumuuza kwa kiasi kidogo cha pesa kwenye dirisha linalofuata jambo linaloashiria licha ya kwamba hawahitaji kuona anaondoka itawabidi wakubali ili kupata pesa nyingi kuliko kupata pesa kidogo na kumkosa kabisa.

Kiasi cha sasa kinachotajwa kuwa ni thamani yake na timu zinazomuhitaji ndio zinatakiwa kukiandaa ni Pauni 125 milioni

Kiwango cha Haaland kinazidi kukua siku hadi siku na hadi sasa ameshavunja rekodi kibao ikiwa pamoja na ile ya kufikisha mabao 100 kwenye maisha yake ya soka -na amefikisha mabao hayo kwa haraka zaidi kuliko Messi na Ronaldo.

Vilevile katika umri wake wa miaka 20, tayari amefikisha mabao 20 ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mapema zaidi akiwafunika nyota wote duniani wakiwamo kina Messi na Ronaldo na pia msimu huu amefunga mabao 33 katika mechi 32 za michuano yote alizocheza akiwa Dortmund.