Mnamtaka Bruno? Mtasumbuka tu

Muktasari:
- Miamba ya soka ya Hispania, Real Madrid imeripotiwa kuwa tayari kulipa Pauni 90 milioni kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi ili kupata huduma ya nahodha huyo wa Man United, Fernandes.
MANCHESTER, ENGLAND: KOCHA wa Manchester United, Ruben Amorim amemwambia kiungo Bruno Fernandes hatauzwa kwa bei yoyote ile licha ya miamba hiyo ya Old Trafford kuhitaji pesa kwa nguvu zote.
Miamba ya soka ya Hispania, Real Madrid imeripotiwa kuwa tayari kulipa Pauni 90 milioni kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi ili kupata huduma ya nahodha huyo wa Man United, Fernandes.
Lakini, kocha Amorim alisema: “Haendi kokote kwa sababu ni’shamwambia hilo.”
Mmiliki mwenza wa Man United, bilionea Sir Jim Ratcliffe amekuwa akipunguza matumizi kwenye kikosi hicho baada ya kuondoa wafanyakazi 450 - baada ya kudaiwa kwamba timu hiyo ipo kwenye hatari ya hesabu zake kuvuka kiwango. Na hapo, Amorim alikiri kuna wachezaji watauzwa kwenye dirisha lijalo.
Makinda Kobbie Mainoo na Alejandro Garnacho wanaweza kupigwa mnada dirisha lijalo kutokana na Man United kutokuwa vizuri kwenye hesabu za kifedha kwenda sambamba na kanuni ya matumizi ya Ligi Kuu England.
Wachezaji hao walioibuliwa kwenye kikosi hicho wanaweza kuipa Man United faida ya walau ya Pauni 100 milioni. Lakini, kabla ya mechi ya Jumanne, Aprili 1 dhidi ya Nottingham Forest, Amorim aliamua kuzizima habari za kumuhusu Fernandes kama atauzwa, aliposema:
“Hapana. Hilo haliwezi kutokea. Tumekusanya pointi chache msimu huu, lakini namtaka Bruno awepo hapa kwa sababu tunataka kushinda tena ubingwa wa ligi.” Fernandes, 30, Agosti mwaka jana alisaini mkataba mpya unaomweka Old Trafford hadi 2027, huku kukiwa na kipengele pia cha kuongezewa mmoja zaidi ambao utamfanya awepo hadi 2028.