Mkosi bado unamwandama Dele Alli

Muktasari:
- Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 28 alitoka kwenye benchi Jumamosi kwenye mechi dhidi ya AC Milan, ambapo ilikuwa ni mara yake ya kwanza kucheza mechi ya kimashindano tangu Februari 2023.
COMO, ITALIA: MAJANGA yanazidi kumwandama straika wa zamani wa Tottenham, Dele Alli anayekipiga Como ya Ligi Kuu ya Italia, Serie A baada ya kutolewa kwa kadi nyekundu katika mchezo dhidi ya AC Milan.
Dele, 28, alitolewa ikiwa ni dakika 10 tu tangu aingie kuchukua nafasi ya Lucas Da Cunha mfungaji pekee wa bao la Como ikichapwa mabao 2-1 na miamba hiyo ya jiji la Milan, ikiwa ni mchezo wake wa kwanza wa kimashindano tangu Februari 2023.
Dele alisajiliwa na Como kwa uhamisho wa bure kwa mkataba wa miezi 18 na mara ya mwisho alicheza katika Ligi Kuu ya Uturuki akiwa na Besiktas.
Kadi hiyo nyekundu ni baada ya awali kuonyeshwa ya njano kwa kumchezea vibaya Ruben Loftus-Cheek wakati akijaribu kumkaba, ingawa wachezaji wa Milan walilalamika wakidai mwamuzi Matteo Marchetti akatazame VAR na baada ya kujiridhisha akamtoa nje ya uwanja.
Uamuzi huu ulizua hasira kwenye benchi la Como, kiasi cha kusababisha kocha mkuu wa timu hiyo, Cesc Fabregas naye kuonyeshwa kadi nyekundu muda mfupi baadaye.
Kabla ya kuonyeshwa kadi nyekundu, beki wa Milan Kyle Walker ambaye aliwahi kucheza na Dele Alli Spurs na timu ya taifa ya England, alionekana akimuomba mwamuzi asiomuonyeshe Dele kadi nyekundu.
Dele alianza maisha yake ya soka akiwa na MK Dons kabla ya kusajiliwa na Tottenham mwaka 2015.
Tangu wakati huo alioyesha kiwango bora kiasi cha kuichezea England mechi 37 za kimataifa, lakini mambo yamemharibikia sana katika miaka mitano iliyopita.
Alicheza kwa miaka mitatu akiwa Everton, kabla ya kutua kwa mkopo Besiktas mwaka 2023.