Kisa Kudus Spurs waambiwa “uweni siriazi basi”

Muktasari:
- Spurs imemfanya Kudus kuwa kipaumbele chao kwenye usajili wa dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi baada ya kuweka kando mpango wa kuwasajili Eberechi Eze na Bryan Mbeumo, ambaye anataka kujiunga na Manchester United.
LONDON, ENGLAND: MABOSI wa West Ham United wamewaambia Tottenham Hotspur wanapaswa kuwa siriazi kama kweli wanahitaji huduma ya supastaa Mohammed Kudus baada ya kugomea ofa yao ya kwanza.
Spurs imemfanya Kudus kuwa kipaumbele chao kwenye usajili wa dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi baada ya kuweka kando mpango wa kuwasajili Eberechi Eze na Bryan Mbeumo, ambaye anataka kujiunga na Manchester United.
Tottenham inahusishwa pia na mpango wa kumsajili staa wa Bournemouth, Antoine Semenyo, lakini tatizo limeibuka baada ya mchezaji huyo kusaini mkataba wa miaka mitano kubaki Cherries.
Kudus sasa amekuwa kwenye rada za miamba hiyo ya London na West Ham imekataa kupokea ofa yao ya Pauni 50 milioni.
Ripoti zinafichua kwamba, West Ham haikufurahishwa na ofa ya nyongeza iliyowekwa na Spurs na kwamba wanachokitaka wao ni uhakika wa kupata Pauni 60 milioni. Kilichoelezwa ni kwamba Spurs imeweka kipengele cha kuongeza pesa kama tu watashinda taji la Ligi Kuu England au Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Msimu uliopita, Spurs ilihitimisha ukame wa miaka 17 ya kusubiri taji baada ya kunyakua Europa League, ambapo lilikuwa taji lao la kwanza la Ulaya tangu mwaka 1984 na haijabeba ubingwa wa ligi tangu 1961. Kutokana na hilo, West Ham United imeiambia Spurs waende na ofa yenye kueleweka na si hizo ndoto zao. Hata hivyo, Spurs inaweka vipengele hicho kwa sababu inaamini kwenye uwezo wa kocha wao mpya, Thomas Frank, kwamba mataji ni kitu kitakachowezekana.