Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mkeka wa kila timu itakavyomaliza Ligi Kuu England msimu huu

LONDON, ENGLAND. MCHAKAMCHAKA wa Ligi Kuu England umeanza na tayari mechi za wiki ya kwanza zimeshapigwa.

Aliyetamba katamba na aliyeshindwa kashindwa kwenye mechi hizo za wiki ya kwanza, lakini kumekuwa na utabiri wa namna msimu utakavyokuwa na kila timu itamalizaje.

Kwa mujibu wa gazeti la Mirror, huu hapa utabiri wao wa namna timu zitakavyomaliza msimu wa Ligi Kuu England kwenye vita ya kusaka ubingwa, kusaka tiketi ya michuano ya Ulaya na kukwepa kushuka daraja.


ARSENAL

Mzuka wao: Ben White amewasili kwenye kikosi kuimarisha beki. Bukayo Saka, Emile Smith Rowe na Kieran Tierney wamekuwa wakiibukia vizuri na kumpa kocha Mikel Arteta uhakika mkubwa wa kupata huduma bora kutoka kwao. Kutokana na kutoshiriki michuano yoyote ya Ulaya kutawafanya Arsenal kuwekeza akili yao kwenye ligi tu.

Hofu yao: Pierre-Emerick Aubameyang bado haonekani kuwa kwenye kiwango bora na amekuwa akihusishwa na mpango wa kuondoka, huku kiungo Thomas Partey akipata majeraha yanayomweka nje ya uwanja muda mrefu.

WATAMALIZA: Nafasi 7


ASTON VILLA

Mzuka wao: Emiliano Buendia anaweza kuja kuziba kabisa pengo la Jack Grealish. Tyrone Mings amekuwa na uimara mkubwa kwenye sehemu ya ulinzi, huku wakitarajia kupata mabao kutoka kwa washambuliaji wao Ollie Watkins na staa mpya Danny Ings.

Hofu yao: Walishinda mechi mbili tu kati ya 12 ambazo walicheza bila ya huduma ya Grealish kwenye ligi kwa msimu uliopita na balaa hilo limeanza kujionyesha msimu huu, ambapo wamepoteza mechi yao ya kwanza waliyocheza bila ya huduma ya kiungo huyo mshambuliaji aliyetimkia Manchester City.

WATAMALIZA: Nafasi ya 9


BRENTFORD

Mzuka wao: Rekodi za Ivan Toney zinaonyesha kwamba zitaisaidia timu hiyo kwenye kufunga mabao huku Frank Onyeka akitarajia kuweka nguvu kubwa kwenye kiungo. Wamekuwa wabunifu wakubwa sana wa mtindo wa kiuchezaji na mbinu. Wameshinda mechi yao ya kwanza dhidi ya Arsenal.

Hofu yao: Kikosi hicho hakina upana wa kutosha na hilo linaweza kuwa tatizo kubwa kwao kwenye Ligi Kuu England.

WATAMALIZA: Nafasi ya 19


BRIGHTON

Mzuka wao: Wamekuwa wakicheza soka maridadi sana na kuzipa wakati mgumu timu kubwa. Enock Mwepu ameongezwa kwenye kikosi kushirikiana na Yves Bissouma kutengeneza safu imara kabisa ya kiungo. Kocha Graham Potter anafahamu mfumo wake wa kuwasumbua wapinzani.

Hofu yao: Hakuna ubishi wataikumbuka zaidi huduma ya beki Ben White aliyetua Arsenal. Adam Lallana na Danny Welbeck wote wamekuwa majeruhi wa mara kwa mara huku wakifahamu wanahitaji straika ambaye atakuwa anawafungia mabao ya kutosha.

WATAMALIZA: Nafasi ya 14


BURNLEY

Mzuka wao: Nick Pope, James Tarkowski na Ben Mee wamekuwa kwenye kiwango kizuri. Uwanja wa Turf Moor utaendelea kuwa mahali pagumu kwa timu za kigeni na Sean Dyche anajua namna ya kuwakabili wapinzani wake wanapokuja kwenye uwanja huo.

Hofu yao: Kikosi hakikufanyiwa marekebisho ya kutosha kwa msimu wa pili sasa na jambo hilo linawafanya kuwa kwenye hatari ya kutamba ndani ya uwanja.

WATAMALIZA: Nafasi ya 16


CHELSEA

Mzuka wao: Romelu Lukaku atakuja kuwaongezea mabao 30 kwenye kikosi hicho ambacho kimekuwa na vijana wengi. Kocha wao Thomas Tuchel amekuwa na ujuzi mkubwa wa kucheza kimbinu na hilo linawapa matumaini makubwa ya kutamba kwenye Ligi Kuu England msimu huu.

Hofu yao: Wamemnasa Lukaku kwa pesa nyingi, lakini wasiwasi wao upo kama atakwenda Stamford Bridge na kuonyesha kiwango kile alichokuwa nacho Manchester United. Kingine ni kama Timo Werner ataanza kuonyesha makali ya kufunga.

WATA-MALIZA: Nafasi ya 3


CRYSTAL PALACE

Mzuka wao: Kikosi chao wanaamini wachezaji wenye uzoefu watawasaidia vijana kuonyesha kiwango bora na kutamba kwenye ligi. Kuna vijana wenye vipaji vikubwa kama Marc Guehi na Michael Olise walioongezwa kwenye timu huku wakiendelea kubaki pia na huduma ya Wilfried Zaha.

Hofu yao: Mwanzo mgumu kwa kocha mpya Patrick Vieira. Eberechi Eze amekuwa na majeruhi wa mara kwa mara na uteuzi wao wa kocha Vieira wanaona kama ni kamari.

WATAMALIZA: Nafasi ya 18


EVERTON

Mzuka wao: Rafa Benitez ni kocha mwenye uzoefu. Dominic Calvert-Lewin na Richarlison watapafanya Goodison Park paendelee kuwa mahali pazuri kwa mashabiki wa Everton kwenda kutazama mpira. Mechi yao ya kwanza ya ligi msimu huu wameanza kwa ushindi.

Hofu yao: Wamefanya usajili wa wachezaji wachache sana. Shida nyingine ni kuhusu kocha Rafa Benitez kushindwa kuungwa mkono na mashabiki na wamekuwa wakibeba mabango kumtaka aondoke.

WATAMALIZA: Nafasi ya 8


LEEDS

Mzuka wao: Hakuna shaka, kikosi hiki kitamaliza nafasi ya 10 kwenye msimamo wa Ligi Kuu England msimu huu. Kalvin Phillips na Raphinha wamebaki kwenye kikosi na Jack Harrison ameongezwa kwenye timu huku Marcelo Bielsa akifahamika kuwa ni kocha bora. Wameanza vibaya mechi yao ya kwanza baada ya kuchapwa 5-1 na Manchester United.

Hofu yao: Utakuwa msimu wa pili kwao mgumu kabisa baada ya ule wa kwanza, huku kikosi hicho kikihitaji uboreshaji mkubwa kushindana kwa viwango vya juu.

WATAMALIZA: Nafasi ya 10


LEICESTER

Mzuka wao: Patson Daka na Kelechi Iheanacho watampa sapoti ya kutosha Jamie Vardy kwenye fowadi ya timu hiyo huku kurejea kwa Harvey Barnes kunawapa uhakika mkubwa wa kutamba uwanjani. Ubingwa wa Kombe la FA Cup umewapa mzuka zaidi. Walianza vyema msimu wao kwa kushinda mechi ya kwanza.

Hofu yao: Wesley Fofana atakuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu kutokana na kuwa majeruhi na Jonny Evans bado hayupo fiti. Kwa misimu miwili wameshindwa kumaliza ndani ya Top Four.

WATAMALIZA: Nafasi ya 5


LIVERPOOL

Mzuka wao: Mohamed Salah na Sadio Mane watakuwa na wakati mzuri wa kufanya mambo kwenye fowadi yao hasa ukizingatia mabeki wao wamerudi. Thiago anaonekana sasa kulimudu soka la England na Harvey Elliott amepevuka na kuwa mchezaji wa maana kwenye kikosi hicho. Wameanza msimu wao kibabe kwa kushinda mabao matatu.

Hofu yao: Wamekuwa wakimya kwenye dirisha la usajili, huku Gini Wijnaldum akiwa ameachana na timu hiyo. Kingine ni kama Virgil Van Dijk atakuwa kwenye ubora wake wa awali kabla ya kuumia.

WATAMALIZA: Nafasi ya 2


MAN CITY

Mzuka wao: Jack Grealish ametua kwenye kikosi hicho, huku wakiwa kwenye mchakamchaka wa kufukuzia huduma ya straika Harry Kane. Wakimpata Kane watakuwa balaa zaidi kwa sababu atakwenda kucheza na wapishi moto wa mabao akiwamo Raheem Sterling, Kevin De Bruyne na Phil Foden. Wameanza vibaya msimu huu baada ya kuchapwa 1-0 na Tottenham Hotspur.

Hofu yao: Kukosekana kwa wachezaji wao kuliwatibulia kwenye maandalizi ya msimu mpya. Sergio Aguero ameondoka na wanapambana kutaka Ligi ya Mabingwa Ulaya.

WATAMALIZA: Nafasi ya 1


MAN UNITED

Mzuka wao: Jadon Sancho na Raphael Varane wametua kwenye kikosi hicho kuongeza nguvu. Mason Greenwood naye yupo kwenye wakati wa kuonyesha ubora wake halisi huku chama lao likiwa na wakali wote muhimu katika vita ya kukimbizia ubingwa. Kikosi hicho cha kocha Ole Gunnar Solskjaer kimeanza vizuri baada ya kuichapa Leeds United mabao 5-1 katika mechi yao ya kwanza ya ligi.

Hofu yao: Marcus Rashford atakuwa nje ya uwanja kwa miezi kadhaa na bado hawajamalizana na Paul Pogba, anayewaweka kwenye wasiwasi mkubwa wa kumpoteza. Kitu kingine ni kama Solskjaer atakuwa na uwezo wa kubeba mataji.

WATAMALIZA: Nafasi ya 4

NEWCASTLE

Mzuka wao: Kocha Graeme Jones ameonyesha dalili nzuri za kufanya timu kuwa na kiwango bora uwanjani. Timu hiyo imetumia Pauni 22 milioni kunasa huduma ya mfungaji Joe Willock kutoka Arsenal, huku ikifanikiwa pia kumbakiza kwenye kikosi chao mkali Allan Saint-Maximin. Wameanza vibaya kwa kuchapwa 4-2 na West Ham United.

Hofu yao: Mike Ashley bado yupoyupo sana kwenye mechi hiyo. Timu hiyo inahitaji uwekezaji mkubwa. Kocha Steve Bruce naye si kipenzi cha mashabiki wa Newcastle.

WATAMALIZA: Nafasi ya 12


NORWICH

Mzuka wao: Daniel Farke na wachezaji wengine kama Todd Cantwell, Max Aarons na yule waliyemnasa kwa mkopo Billy Gilmour wanawapa matumaini ya kupambana kwenye Ligi Kuu England kwa kiasi cha kutosha kukabiliana na changamoto zote. Mchezo wao wa kwanza walikubali kichapo nyumbani kutoka kwa Liverpool.

Hofu yao: Emiliano Buendia ni pigo kubwa kwao baada ya kuondoka. Bila shaka watakuwa wana udhaifu mkubwa kwenye kupata nguvu ya kuzitingisha ngome za wapinzani kama alivyokuwa akifanya Buendia.

WATAMALIZA: Nafasi ya 17


SOUTHAMPTON

Mzuka wao: Kinara wa kupiga mipira iliyokufa kwenye Ligi Kuu England ni James Ward-Prowse. Kocha Ralph Hassenhutl ameonyesha uwezo mkubwa wa kukiweka sawa kikosi hicho. Hata hivyo, hakijaanza vizuri, kikichapwa 3-1 na Everton.

Hofu yao: Wasiwasi wao upo kwa Adam Armstrong kama ataweza kufunga mabao kuziba pengo la Danny Ings, ambaye amechana na timu hiyo.

WATAMALIZA: Nafasi ya 15


TOTTENHAM

Mzuka wao: Dele Alli anaweza kuwa mtu muhimu tena kwenye kikosi hicho baada ya kocha Jose Mourinho kuondoka na Heung-Min Son atakuwa staa wa mchezo. Bryan Gil na Cristian Romero wanaonekana kuwa usajili mzuri na Spurs imeshinda mechi yake ya kwanza dhidi ya timu ngumu ya Manchester City.

Hofu yao: Ni ishu ya straika wao namba moja, Harry Kane kama atabaki au kuondoka kwenye timu hiyo. Spurs inahitaji kujijenga upya, huku ikiwa chini ya kocha mpya Nuno Espirito Santo, ambaye atahitaji kupewa muda.

WATAMALIZA: Nafasi ya 6


WATFORD

Mzuka wao: Walifanya usajili mapema sana, hivyo wamepata nafasi ya kufanya maandalizi ya kutosha ya msimu mpya. Kitu kingine wamefanikiwa kumbakiza Ismail Sarr na bado wanaendelea kupata huduma ya Troy Deeney. Walishinda mechi ya kwanza dhidi ya Aston Villa.

Hofu yao: Safu yao ya mabeki kama ina ubora kuliko ile iliyowafanya washuka daraja hivi karibuni. Kitu kingine ni kuhusu muda atakaodumu kocha wao Xisco Munoz chini ya uongozi wa Watford ambao suala la kufukuza makocha halijawahi kuwa gumu.

WATAMALIZA: Nafasi ya 20


WEST HAM

Mzuka wao: Kocha David Moyes amekuwa akifanya mapinduzi makubwa kwenye kikosi hicho. Wamerejea kwenye michuano ya Ulaya baada ya kumaliza namba sita msimu uliopita. Wamembakiza Declan Rice, Tomas Soucek na Vladimir Coufal wataendelea kucheza pamoja.

Hofu yao: Michuano ya Europa League inayochezwa Alhamisi usiku inaonekana kuwa na mkosi kwao. Kingine hawajafanya usajili mkubwa jambo linalowaweka kwenye wasiwasi mkubwa kama kikosi chao kitaweza kuwa na uwezo wa kupambana.

WATAMALIZA: Nafasi ya 11


WOLVES

Mzuka wao: Raul Jimenez amerejea kwenye kikosi cha kwanza, huku mkali wao mwi-ngine Adama Traore akione-kana kubaki kwenye timu yao akiachana na mpango wa kwenda Barcelona, huku Francisco Trincao waliomnasa kwa mkopo kutoka Nou Camp ameonyesha kiwango moto kabisa.

Hofu yao: Wolves hofu yao ni juu ya Jimenez kama atakuwa kwenye kiwango kilekile kabla hajapata majeraha ya kichwa. Wasiwasi mwingi-ne ni majeruhi Pedro Neto huku ni kama kocha wao Bruno Lage mfumo wake mpya utatiki kwa haraka kikosini.

WATA-MALIZA: Nafasi ya 13