LEBRON NA BRONNY: Baba, mwana walioanza na kupoteza pamoja NBA

Muktasari:
- Huo ulikuwa ni ushindi wa 4-1 wa Minnesota katika mechi za mchujo dhidi ya wapinzani wao hao katika ligi hiyo kutoka Kanda ya Magharibi.
LOS ANGELS, MAREKANI: MSIMU wa kwanza wa nyota mpya wa Los Angeles Lakers, Bronny James katika Ligi ya Kikapu Marekani (NBA) ulimalizika wiki hii kwa kichapo cha pointi 103-94 kwenye mechi ya mchujo kutoka kwa Minnesota Timberwolves.
Huo ulikuwa ni ushindi wa 4-1 wa Minnesota katika mechi za mchujo dhidi ya wapinzani wao hao katika ligi hiyo kutoka Kanda ya Magharibi.
Mechi hizo za mchujo ambazo zinaendelea, zimehitimisha msimu mwingine mbaya kwa Lakers waliokuwa wakipewa matumaini makubwa kufuzu robo fainali na hata fainali ya NBA msimu huu.
Bahati mbaya ilikuwa ni kwa Bronny ambaye ni mtoto wa LeBron James kumaliza mapema msimu, huku ukimwacha baba’ke akiachiwa mtihani wa kuamua kuhusu hatima yake, ingawa akiwa chaguo la mchezaji mwenye thamani ya Dola 52.6 milioni kwa msimu wa 2025.
Kwa upande wa Bronny sasa ni muda wa kutafakari ilikuwaje aweke historia kuwa sehemu ya chaguo la kwanza la baba na mwana katika NBA baada ya kukabiliana na mashambulizi ya vyombo vya habari na kuanza kujijenga upya katika G-League baada ya mwanzo mgumu.
Hata hivyo, alipoulizwa na FOX Sports kuhusu kucheza na baba yake katika kikosi kimoja wiki hii, Bronny alisema, “ni baraka kuweza kujifunza kutoka kwake, si tu kama mchezaji, bali pia kama baba. Ni aina tofauti kabisa ya uhusiano.
“Najaribu kutumia faida ya nafasi hii kwa sababu sio kila mtu anaweza kupata bahati kama hii. Umekuwa ni uzoefu wa kipekee sana kwangu kucheza naye katika kikosi kimoja.
“Na ninatarajia kujifunza zaidi kutoka kwake, iwe bado yupo hapa au la vyovyote vile. Lakini ninatarajia hilo.”
Huenda kukawa na faida kwa Bronny endapo LeBron ataamua kutoendelea kuichezea Lakers kwani ataendelea kukipiga bila kuwapo kwa kivuli kizito cha baba yake anayeelekea ‘Hall of Fame’.
Lakini, kijana huyo mwenye umri wa miaka 20 bado hajawa tayari kusimama peke yake akihitaji sapoti kubwa kutoka kwa mzazi huyo, japo anaweza kuipata kutoka kwake popote atakapokuwa.
“Ndiyo, bila shaka,” Bronny aliambia FOX alipoulizwa kama angependa kucheza msimu mwingine na baba yake.
“Kwa muda wote anaporejea huwa ni furaha kuwa naye karibu. Amejikita sana kwenye mchezo. Mambo anayofanya kwa ajili ya mwili wake, maandalizi yake na mambo mengine kama hayo — nataka kuyatumia vizuri kabisa.”
LeBron amekuwa akisisitiza kwa miaka kadhaa kwamba anatamani kucheza na mwanaye na ndoto hiyo ilitimia kupitia raundi ya pili ya drafti mwaka jana pale Bronny alipochaguliwa kuwa miongoni mwa machaguo mapya yatakayokipiga NBA.
Mfungaji bora huyo wa muda wote wa NBA na bingwa mara nne alipoulizwa kuhusu nafasi ya tukio hilo kwenye mafanikio yake ya kikazi na majibu yake yalikuwa ya moja kwa moja.
“Namba moja, bila shaka,” alisema LeBron na kuongeza: “Hilo ni wazi, halina hata mjadala. Kuweza kucheza mchezo ninaoupenda na kuwa na mwanangu mwaka mzima huu kumeweka historia kwenye maisha yangu. Imebaki kuwa moja ya safari zenye furaha na kufurahisha zaidi niliyowahi kupitia.”
Bronny alipata wastani wa pointi 21.9, rebounds 5.2 na asisti 5.4 katika G-League, lakini hakuweza kuwa na mchango mkubwa katika dakika chache alizopewa Lakers.
Kocha wa Lakers, Jonathan Clay “JJ” Redick anasema anaona uwapo wa mafanikio kwa Bronny katika siku za usoni.
“Kwa uwezo wake wa kimwili, kasi na mbinu tunaamini atakuwa mshambuliaji mzuri sana wa NBA. Ana nafasi nzuri ya kufanya mambo makubwa,” anasema Redick.
Baada ya Lakers kumsajili Luka Doncic wengi walihisi kuwa timu hiyo ingeweza kupambana kugombea ubingwa msimu huu, na Redick anatoa onyo kwa mastaa wa timu hiyo kwamba anatarajia zaidi msimu ujao utakuwa bora.
“Nitaanza na kipindi cha maandalizi kabla ya msimu mpya na kazi inayotakiwa kufanyika wakati wa kipindi hicho ili kuwa katika hali ya ushindani wa ubingwa,” anasema baada ya kupoteza katika mchujo.
“Tuna kazi kubwa kama kikosi. Bila shaka, wapo wachezaji walio kwenye hali bora ya kimwili, na pia wapo wengine ambao wangepaswa kuwa kwenye hali bora zaidi. Hapo ndipo akili yangu inaelekea moja kwa moja kwenye ubingwa — tunapaswa kuwa katika kiwango cha ubingwa.”
LeBron ana uhusiano wa karibu na Redick, huku wote wawili wakiwa wameanzisha podikasti ya Mind the Game, na anasema kocha wake ameanza vyema licha ya kukosa uzoefu.