Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Misri yazifuata Morocco, Tunisia Kombe la Dunia

MISRI Pict

Muktasari:

  • Mabao ya Ibrahim Adel na Mohamed Salah aliyepachika mawili yaliifanya Misri kuwa timu ya tatu kutoka Afrika kufuzu Kombe la Dunia 2026. Taifa Stars ilipoteza kupitia bao la Fashion Sakala.

MISRI imeungana na Morocco na Tunisia kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2026 baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Djibouti katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Larbi Zaouli, Casablanca nchini Morocco, huku Tanzania ikimaliza harakati za kufuzu kwa kufungwa bao 1-0 nyumbani dhidi ya Zambia, jana  Jumatano. Kabla ya mechi hizo, nchi mbili kutoka Afrika zilishafuzu Kombe la Dunia ambazo ni Morocco kutoka Kundi E na Tunisia ya Kundi H.

Mabao ya Ibrahim Adel na Mohamed Salah aliyepachika mawili yaliifanya Misri kuwa timu ya tatu kutoka Afrika kufuzu Kombe la Dunia 2026. Taifa Stars ilipoteza kupitia bao la Fashion Sakala.

Licha ya Burkina Faso kuibuka na ushindi wa bao 1-0 ugenini dhidi ya Sierra Leone, Misri imefikisha pointi 23 ambazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine kwenye kundi A la mashindano ya kuwania kufuzu kupitia kanda ya Afrika.

Kwenye Uwanja wa Ben M’Hamed El Abd, Jadida nchini Morocco, Ghana ilibuka na ushindi mnono wa mabao 5-0 dhidi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Mis 01

Matokeo hayo yameifanya Ghana ihitaji angalau pointi moja tu katika mechi yake ya mwisho nyumbani dhidi ya Comoro, Oktoba 12, 2025 ili itinge Kombe la Dunia ikiwa ni moja ya mataifa ambayo yalikuwa hayapewi nafasi kubwa zaidi ya kufuzu kwa michuano hii kutokana na jinsi ilivyoanza kwa kusuasua.

Kwa Ghana, sasa inaongoza msimamo wa kundi I ikiwa na pointi 22, huku Madagascar iliyoifunga Comoro kwa bao 1-0 inashika nafasi ya pili kwa pointi zake 19 na ina nafasi kubwa zaidi ya kufuzu kupitia best loser kutokana na kuwa na pointi nyingi zaidi kuliko timu nyingine zilizopo kwenye makundi mengine zinazoshika nafasi ya pili.

Timu nne za juu katika msimamo wa best loser zitapangiwa droo yake na kucheza mechi moja moja za mtoano. Zitakazopenya zitakutana katika fainali. Na mshindi wa fainali ataenda kucheza mtoano na wenzao wa CONCACAF kupata timu ya kwenda Kombe la Dunia.

Mis 02

Cape Verde ambayo juzi ilikuwa inapewa nafasi kubwa ya kufuzu kwenye fainali hizi kwa mara ya kwanza, ililazimika kutoka nyuma baada ya kutanguliwa kwa mabao matatu na Libya na kutoka sare ya mabao 3-3 katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Tripoli, Libya.

Sare hiyo imeifanya Cape Verde kuendelea kuongoza msimamo wa kundi D ikifikisha pointi 20 na sasa inahitaji ushindi wa nyumbani dhidi ya Eswatini, Oktoba 13, 2025 ili iandike historia ya kufuzu kwa mara ya kwanza Fainali za Kombe la Dunia.

Tayari mashabiki wa nchi hiyo walishaanza kufanya sherehe kwenye sehemu mbalimbali za taifa hilo, lakini sare hiyo imewafanya sasa wasubiri kuona nini ambacho kinaweza kutokea baadaye kwenye mechi ya mwisho ikiwa nyumbani.

Afrika Kusini ambayo imepokonywa pointi tatu, leo itajiuliza ugenini dhidi ya Zimbabwe katika Kundi C kwenye mechi ambayo inatakiwa kupata ushindi kutokana na upinzani mkubwa wanaokutana nao kutoka kwa Benin baada ya kila timu kuwa na pointi 14 zikiwa zimebakiza michezo miwili kila moja.

Benin ambayo inatafuta kufuzu kwa mara ya kwanza itakuwa nchini Rwanda kuvaana na wenyeji hao ambao wanatarajia kupata ushindi ili kufufua matumaini yao baada ya kukusanya pointi 11 kwenye mechi 8 sawa na Nigeria.

Senegal kutoka Kundi B, inatakiwa kupata ushindi leo dhidi ya Sudan ya Kusini na kuomba DR Congo idondoshe pointi ili iweze kufuzu moja kwa moja kwenye fainali hizo kwani itafikisha pointi 21 baada ya kucheza mechi nane, lakini vinginevyo inaweza kujikuta kwenye wakati mgumu endapo DR Congo itapata ushindi kwani kwa sasa ina pointi 16. Ivory Coast inapewa nafasi kubwa ya kuendelea kukaa kileleni leo itakapovaana na vibonde Shelisheli.

Ivory Coast yenye pointi 20 moja mbele ya Gabon, imekuwa ikionyesha kiwango cha juu, itakuwa ugenini dhidi ya timu hiyo ambayo haijashinda mechi yoyote wala kupata sare kwenye michuano hii.

Ushindi wa Ivory Coast hapa utategemea matokeo ya mechi ya Gabon dhidi ya Gambia itakayochezwa leo.