Mbappe amlaumu Deschamps, awashushia lawama wenzake
Muktasari:
- Ufaransa ilikuwa ikipewa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa kutokana na kikosi chake chenye nyota kama Mbappe, Michael Olise wa Bayern Munich na mshindi wa Ballon d'Or, Ousmane Dembele.
DALLAS, MAREKANI: NAHODHA wa Ufaransa, Kylian Mbappe, amemlaumu kocha Didier Deschamps kwa mbinu alizozitumia pamoja na kuwakosoa wenzake kwa kushindwa kutekeleza majukumu yao, kufuatia kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Hispania kilichoiondoa timu hiyo katika nusu fainali ya Kombe la Dunia.
Ufaransa ilikuwa ikipewa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa kutokana na kikosi chake chenye nyota kama Mbappe, Michael Olise wa Bayern Munich na mshindi wa Ballon d'Or, Ousmane Dembele.
Hata hivyo, walishindwa kabisa kuhimili ubora wa Hispania, ambayo ilicheza kwa nidhamu na kutinga fainali ambako itakutana na mshindi wa mchezo kati ya England na Argentina.
Baada ya kipigo hicho mjini Dallas, gazeti la L'Equipe lilimpa Mbappe alama 3/10, moja ya alama za chini kabisa kwa wachezaji wa Ufaransa.
AICHAMBUA TATIZO
Mbappe amesema tatizo kubwa lilikuwa kwenye mfumo wa timu na kushindwa kuwasiliana vizuri uwanjani.
"Tulikuwa watatu dhidi ya wawili katikati ya uwanja na hilo ni gumu dhidi ya Hispania. Fabian Ruiz na Rodri walikuwa na muda mwingi wa kucheza mpira."
Aliongeza kuwa Ufaransa ilipaswa kutumia mfumo wa kumkaba kila mchezaji mmoja mmoja badala ya kuwapa nafasi wapinzani kutawala mchezo.
"Kulikuwa na ukosefu wa mawasiliano wakati wa kushinikiza. Tulipaswa kutumia presha ya mtu kwa mtu ili kuwafanya wakimbie pamoja nasi."
AMLAUMU DESCHAMPS KWA MBINU
Mbappe amesema Ufaransa haikucheza kwa kiwango kilichokuwa kimepangwa, akisisitiza kuwa walifeli kiufundi na kimkakati.
"Usipofanya kile unachotakiwa kufanya katika nusu fainali ya Kombe la Dunia, hushindi. Hispania iliheshimu mpango wake wa mchezo na ilisimamia vizuri falsafa yake." Aliendelea:
"Walitaka kutawala mpira na kasi ya mchezo. Mpango wetu ulikuwa kuwabana juu ili wasiweze kufanya hivyo, lakini hatukufanikiwa. Tulikuwa wazembe kiufundi na hatukuwadhuru pale tulipopata nafasi."
Mbappe alieleza kuwa hata waliporejesha umiliki wa mpira walishindwa kuutumia vizuri kutokana na kugusa vibaya mipira ya kwanza.
"Tulipoupata mpira, mguso wetu wa kwanza haukuwa mzuri. Hilo ndilo lililosababisha tushindwe. Ni maumivu makubwa, lakini ukweli ni kwamba hatukufanya kila kilichohitajika kufika fainali."
Kauli hizo zimeonekana kama ujumbe wa moja kwa moja kwa kocha Didier Deschamps na baadhi ya wachezaji waliokuwa uwanjani.
HAKWEPI LAWAMA
Pamoja na kuwakosoa wenzake na benchi la ufundi, Mbappe amesema kama nahodha yuko tayari kubeba lawama zote.
"Unaposhinda unapewa sifa zote. Usiposhinda, lazima ukubali lawama zote. Hivyo ndivyo ilivyo."
ENZI ZA DESCHAMPS ZAFIKIA MWISHO
Mechi dhidi ya Hispania ilikuwa ya pili kutoka mwisho kwa Didier Deschamps ambaye tayari amethibitisha ataondoka baada ya Kombe la Dunia kumalizika.
Atahitimisha safari yake kwa kuiongoza Ufaransa katika mechi ya kusaka nafasi ya tatu dhidi ya atakayepoteza mchezo wa England na Argentina.
Taarifa kutoka Ufaransa zinaeleza kuwa nguli Zinedine Zidane ndiye anayetarajiwa kurithi mikoba ya Deschamps.
Zidane, ambaye hajaifundisha timu yoyote tangu alipoondoka Real Madrid mwaka 2021, anaripotiwa kupanga kuingia na aliyekuwa kipa wa Ufaransa, Fabien Barthez, kwenye benchi lake la ufundi.
Inaelezwa pia kuwa Zidane ana uhusiano mzuri na Mbappe, jambo linaloweza kuwa mwanzo wa sura mpya ndani ya timu ya taifa ya Ufaransa baada ya maumivu ya kuondolewa katika Kombe la Dunia.