Milan yazitajia, Madrid, Bayern bei ya Leao

Muktasari:
- Ripoti zinaeleza Bayern ndio inaonekana kuwa na nafasi kubwa ya kumsajili staa huyu wakihitaji akacheze sambamba na Harry Kane kwa msimu ujao.
MILAN, ITALIA: AC Milan wamewaambia wawakilishi wa Real Madrid na Bayern Munich kuwa inahitajika Euro 130 milioni ili kuipata saini ya mshambuliaji wao Rafael Leao katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Ripoti zinaeleza Bayern ndio inaonekana kuwa na nafasi kubwa ya kumsajili staa huyu wakihitaji akacheze sambamba na Harry Kane kwa msimu ujao.
Kwa mujibu wa tovuti ya Corriere dello Sport, AC Milan wameweka bei hiyo ya Euro 130 milioni kwa ajili ya kumuuza mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Ureno kutokana na wingi wa timu zinazomhitaji ambazo, mbali ya Madrid na Bayern kuna tetesi za , Arsenal, na baadhi ya timu za Saudi Arabia kumhitaji.
Licha ya mkataba wa fundi huyu kuwa na kipengele kinachoeleza kuwa anaweza kununuliwa kwa Euro 175 milioni, inaelezwa mabosi wa Milan watakuwa tayari kumwachia hata kwa pesa pungufu ya hapo kufikia Euro 130 milioni.
Winga huyo mwenye umri wa miaka 25 alicheza mechi 50 katika mashindano yote msimu uliopita, akifunga mabao 12 na kutoa pasi za mabao 13 .
Bayern ambao wamechukua ubingwa wa Bundesliga msiumu uliopita, wanatafuta winga wa kushoto bila atakayemsaidia Leroy Sane na watasajili ikiwa fundi huyo ataondoka au atabakia.
Klabu tatu kubwa za Saudi Arabia ambazo ni Al Nassr, Al Hilal, na Al Ittihad pia zinaonyesha nia kubwa kwa mchezaji huyo wa kimataifa wa Ureno na zinaripotiwa kuwa tayari kumpa mshahara wa kuvutia wa wa hadi Euro 25 milioni kwa mwaka.
Leao alijiunga na Milan mwaka 2019 na ana mkataba wa kuitumikia timu hiyo hadi mwaka 2028.