Mikel Arteta ana kazi kubwa ya kufanya Arsenal
Muktasari:
- Bao la kusawazisha la Sunderland la dakika za majeruhi kwenye mchezo wa Ligi Kuu England, Jumamosi iliyopita lilitibua rekodi ya Arsenal ya kushinda mechi tisa mfululizo.
LONDON, ENGLAND: KWA mara ya kwanza baada ya wiki kadhaa, Mikel Arteta ataketi kitako kuchambua mechi ya Arsenal ambayo imeshindwa kupata ushindi.
Bao la kusawazisha la Sunderland la dakika za majeruhi kwenye mchezo wa Ligi Kuu England, Jumamosi iliyopita lilitibua rekodi ya Arsenal ya kushinda mechi tisa mfululizo.
Arsenal imekuwa ikisifiwa siku za karibuni kwa kiwango bora, lakini kuteleza huko na kisha ushindi wa kibabe iliyopata Manchester City saa zisizozidi 24 baadaye, kimefanya vita ya kusaka ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu kuwa tamu kwelikweli.
Sasa kusuasua kwa Liverpool kwenye mbio za ubingwa, inafanya mchakato huo sasa kuonekana ni mbio za farasi wawili tu licha ya kwamba ndio kwanza zimechezwa mechi 11.
Arsenal imefanya uwezekaji mkubwa kwenye kikosi chake dirisha lililopita na hakika timu hiyo imejaa vipaji vya hali ya juu, aina ya wachezaji ambayo hawajawahi kuwa nao kwa karibu miongo miwili iliyopita.
Pengo la pointi lililopo baina ya Arsenal na Man City si kubwa, hivyo kocha Arteta anapaswa kuchanga vyema karata zake kama anahitaji kushinda taji.
Arsenal ipo kwenye ligi msimu huu kuusaka ubingwa kama ilivyokuwa msimu uliopita, japo ilishindwa kwenye dakika za mwisho na kupigwa kikumbo na Liverpool.
Misimu miwili nyuma, ilipambana kwenye mbio hizo za ubingwa, lakini ilikuwa na kasoro nyingi na ndiyo maana Man City ilitumia fursa hiyo kubeba mataji.
Kutimiza lengo la kunyakua ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu, Arteta kuna mambo manne anapaswa kufanya ili kumaliza ukame wa taji hilo na mara ya mwisho ililibeba 2004.
1. Kuichapa Man City; Inaonekana jambo gumu, lakini kwa Arteta kama anahitaji kuipa Arsenal taji la Ligi Kuu England msimu huu, basi ni lazima ahakikishe anapata matokeo mazuri dhidi ya timu pinzani kwenye mbio za ubingwa huo. Kunyakua pointi kutoka Man City au kuigomea timu hiyo kuchukua pointi tatu dhidi yao. Arsenal ilichapwa na Liverpool, lakini kushinda ubingwa, unahitaji kuwabana wapinzani wako kwenye mbio hizo.
2. Kutumia mastaa wote; Arsenal imeboresha kikosi chake ili kukifanya kuwa kipana chenye uwezo mkubwa wa kushindania mataji.
Kikosi cha Arteta kwa sasa kimesheheni mastaa wa maana kuanzia kwa wanaoanzishwa na wale wanaosubiri kwenye benchi, huku kuwa na vipaji vya hali ya juu kama Declan Rice, David Raya, Viktor Gyokeres, Eberechi Eze na Martin Zubimendi wanaongeza kitu kikubwa kwenye timu na uwepo wa mabeki kama William Saliba wanafanya Arsenal kuwa timu bora ndani ya uwanja. Arteta anapaswa kuwatumia wanajeshi wake wote kwa usahihi katika mbio za ubingwa huo.
3. Kuongeza ukatili; Kilichotibua msimu uliopita na mingine iliyotangulia, Arsenal ilikosa ukatili kwenye mechi ilizocheza dhidi ya timu zenye ubora wa kawaida. Ilipambana kupata matokeo mazuri dhidi ya Man City, Manchester United na hata Liverpool, lakini kuangusha pointi kwenye mechi za timu za kawaida kama Brighton, Nottingham Forest na Everton zilitibua mipango yao.
Arsenal inahitaji kutengeneza moyo wa ukatili wa kuhakikisha inapata matokeo bora dhidi ya timu hizo za viwango vya kawaida, kukusanya pointi kwa kadri inavyowezekana. Kile kilichotokea dhidi ya Sunderland, hakipaswi kujirudia ili kutimiza malengo ya kubeba taji hilo.
4. Kuzingatia mataji mengine; Arsenal inapaswa kuweka mkazo kwenye kubeba mataji mengine pia, ikiwamo Kombe la Ligi. Kuwajenga wachezaji kwenye hali ya kutaka ubingwa, bila ya kujali ni aina gani ya kombe wanakwenda kulibeba, hilo linaweza kuwapa hamasa ya kuchuana katika kupambana na kubeba taji gumu zaidi la Ligi Kuu England.
Kwa Arteta kukifanya kikosi chake kuwa cha kibingwa, anahitaji kukiunda kwenye ubora wa kushindana kuanzia kwenye michuano ya makombe ya kawaida, ikiwamo Kombe la Ligi.