Mike Dean...Nani Ferguson? mtata Wenger
Muktasari:
- Lakini, mwamuzi huyo mkongwe wa England, alisema kocha mtata alikuwa Arsene Wenger, ambaye aliongoza Arsenal kunyakua mataji matatu ya Ligi Kuu England.
LONDON, ENGLAND: MWAMUZI, Mike Dean amefichua kwamba Sir Alex Ferguson wala hakuwa kocha mtata kwa waamuzi waliochezesha mechi za timu yake licha ya wengi kuamini alikuwa moto kwa marefa.
Lakini, mwamuzi huyo mkongwe wa England, alisema kocha mtata alikuwa Arsene Wenger, ambaye aliongoza Arsenal kunyakua mataji matatu ya Ligi Kuu England.
Dean alistaafu kazi za kuchezesha mechi uwanjani kama mwamuzi wa kati mwaka 2022 na kuhamia kwenye VAR, ambako pia aling'atuka miezi 12 baadaye, alipohitimisha miaka yake 28 ya kazi hiyo ya urefa.
Dean alisema kocha Ferguson hakuwahi kumuwakia kwa chochote katika mechi zote alizowahi kuichezesha Manchester United. Lakini, alisema uhusiano wake ulikuwa mbaya sana na gwiji wa Arsenal, Mfaransa Wenger.
Akizungumza katika kipindi cha The Overlap Fan Debate, mwamuzi Dean alisema: “Sijawahi kuelewana na Arsene Wenger.
“Sijui tatizo lilikuwa nini. Sijui pengine ni kwa sababu kila wakati nilipokwenda kuchezesha mechi zao, walipoteza.
“Kila wakati niliokwenda Arsenal, hawakuwa wakijisikia vizuri. Nilizungumza na watu wachache nilikuwa nikifanya nao kazi, ambao kwa sasa wamestaafu, waliniambia mara zote ratiba ilipotoka na kisha jina langu likaonekana naenda kuchezesha mechi zao, basi walijiona hawakuwa na nafasi ya kushinda. Ilikuwa ngumu sana.
“Kulikuwa na dhana kuhusu Sir Alex Ferguson kwamba alikuwa mkali kwa waamuzi muda wote, hakuwa hivyo. Alikuwa akifanya hivyo mbele ya kamera, lakini hajawahi kuja kwenye vyumba vya waamuzi.
“Kwa namna alivyokuwa akizungumza kwenye televisheni, alionekana kama kocha mtata sana kwa waamuzi, lakini wale Wenger na Ferguson walikuwa kama chokaa na siagi.”
Waamuzi wa Ligi Kuu England wamekuwa wakikosolewa sana tangu VAR ilipotambulishwa kwenye ligi hiyo. Na Dean, 57, alibainisha wasiwasi wake juu ya ubora wa waamuzi kwenye ligi hiyo.
Alisema: “Orodha ya waamuzi kwenye Ligi Kuu England hawana nguvu kama ilivyokuwa huko nyuma. Ukiwaondoa waamuzi wanne tu, basi hali inakuwa mbaya. Waamuzi mahiri watatu kwa mujibu wa Fifa na Uefa ni Anthony Taylor, Michael Oliver na Chris Kavanagh, hao ndio waamuzi wakubwa wenye uwezo wa kuchezesha mechi kubwa.”