Mgombea Benfica amtaka Jurgen Klopp
Muktasari:
- Klopp, 58, amejiweka kando kwenye kazi ya ukocha tangu alipoachana na Liverpool mwishoni mwa msimu wa 2023-24.
LISBON, URENO: MMOJA wa wagombea urais kwenye klabu ya Benfica ametoa ahadi ya kumwajiri Jurgen Klopp kwenda kuwa kocha wa timu hiyo endapo kama ataibuka mshindi kwenye uchaguzi mwezi ujao.
Klopp, 58, amejiweka kando kwenye kazi ya ukocha tangu alipoachana na Liverpool mwishoni mwa msimu wa 2023-24.
Mjerumani huyo tangu kipindi hicho amekuwa akifanya kazi kama mkuu wa soka katika klabu za Red Bulls, lakini sasa ameibuka na kuhusishwa kwenye kazi ya ukocha wa timu.
Mgombea urais kwenye klabu ya Benfica, Cristovao Carvalho, ambaye ana nafasi kubwa ya kushinda kiti hicho na mpango wake ni kumvuta kocha huyo mshindi wa Ligi Kuu England na Ligi ya Mabingwa Ulaya kwenda kufanya kazi Ureno.
Kwenye kampeni zake, mgombea huyo ametoa ahadi atahakikisha timu hiyo inacheza fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ndani ya miaka mitano ijayo.
“Kwangu mimi, Bruno Lage (kocha wa sasa wa Benfica) hataendelea kubaki wakati mkataba wake utakapofika tamati,” alisema Carvalho katika kuelekea uchaguzi huo utakaofanyika Oktoba 25.
“Nataka kocha wa viwango vya dunia, mtu ambaye ameshashinda taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya, mtu ambaye atataka kushinda taji hilo la Ulaya akiwa na Benfica. Kuna jina moja tu akilini mwangu: Jurgen Klopp. Amesema pia Benfica ni klabu kubwa na angependa kuwa kocha wa timu hiyo siku moja. Mtu ambaye atasema atahitaji kuwa kwenye timu hiyo kuliko kwingineko.”
Carvalho aliongeza: “Kwa Benfica hii tuliyonayo kwa sasa, hatuwezi kushinda taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya. Ni mpango madhubuti wa kipesa wa kufikia melango. Ninachowaahidi mashabiki, ndani ya miaka minne au mitatu tutacheza fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.”
Hata hivyo, bado haijathibitishwa kama kocha huyo wa zamani wa Borussia Dortmund atakuwa tayari kwenda kufanya kazi kwenye klabu ya Benfica.