Messi ana jambo lake kwa England
Muktasari:
- Kwa muda ilionekana ndoto hiyo ingeahirishwa baada ya Uswisi kuonyesha ushindani mkubwa kwenye robo fainali dhidi ya Argentina, lakini mabingwa hao wa dunia walifanikiwa kushinda kwa mabao 3-1 baada ya dakika za nyongeza na kutinga hatua ya nne bora.
ATLANTA, MAREKANI: KUNA mambo machache sana ambayo Lionel Messi hajawahi kuyafanya ndani ya uwanja wa mpira. Hata hivyo, nusu fainali ya Kombe la Dunia kati ya Argentina na England, itakayochezwa Jumatano jijini Atlanta, itamletea uzoefu mpya kabisa.
Licha ya kucheza zaidi ya mechi 200 na kufunga mabao 125 akiwa na jezi ya Argentina, mshindi huyo wa Ballon d'Or mara nane hajawahi kukutana na England katika ngazi ya timu ya taifa.
Kwa muda ilionekana ndoto hiyo ingeahirishwa baada ya Uswisi kuonyesha ushindani mkubwa kwenye robo fainali dhidi ya Argentina, lakini mabingwa hao wa dunia walifanikiwa kushinda kwa mabao 3-1 baada ya dakika za nyongeza na kutinga hatua ya nne bora.
Katika ushindi huo, Messi alishindwa kufunga kwa mara ya kwanza kwenye Kombe hili la Dunia. Hata hivyo, bado anaongoza mbio za Kiatu cha Dhahabu akiwa amefunga mabao manane, idadi anayoshirikiana na Kylian Mbappe wa Ufaransa. Pia ndiye kinara wa mabao wa muda wote katika historia ya Kombe la Dunia.
'Messi ana kipaji cha kipekee'
Mchambuzi wa BBC na beki wa zamani wa England, Micah Richards, anaamini England inaweza kuwazidi Argentina kwa nguvu na kasi, lakini si kwa kipaji cha Messi.
"England inaweza kuwakimbiza Argentina, lakini wana huyo jitu la kipaji anayeitwa Messi. Timu nzima inamchezea yeye. Hili ni pambano ambalo kila mtu anatakiwa kulisubiri kwa hamu."
Richards alieleza kuwa kumdhibiti Messi ni kazi ngumu kutokana na namna anavyojitengenezea nafasi.
"Hamkabi kirahisi kwa sababu harudi sana kukaba. Anaingia kwenye maeneo madogo ambayo ni vigumu kumfuatilia. Anajua muda sahihi wa kuamka ndani ya mchezo, ana ufundi wa hali ya juu, anaelewa nafasi kuliko wengi na ana shuti kali."
Aliendelea kusema:"Kikubwa zaidi ni kwamba ana kile alicho nacho Jude Bellingham, haiba na kujiamini. Lakini Messi iko kiwango kingine kabisa. Itakuwa mechi ya kuvutia sana."
England isiogope?
Mshambuliaji wa zamani wa England, Chris Sutton, anaamini kikosi cha Thomas Tuchel hakina sababu ya kuingiwa na hofu.
"Nadhani Tuchel pamoja na wachezaji wake watafurahia kucheza dhidi ya Argentina ya sasa. Hii siyo Argentina bora kuwahi kutokea, lakini wana tabia ya kutafuta njia ya kushinda hata wanapokuwa hawachezi vizuri."
Kwa upande wake, mshambuliaji wa zamani wa England, Wayne Rooney amesema Messi anaweza kuwa udhaifu pale timu inapopoteza mpira, lakini uwezo wake wa kuamua mechi haupaswi kubezwa.
"Hakabi sana, hivyo anaweza kuwa udhaifu kwa Argentina. Lakini ana uwezo wa kubadili mchezo kwa dakika moja tu, kama alivyo Jude Bellingham."
Rooney aliongeza:"Siri ya kumkaba Messi ni umakini na mawasiliano ya mara kwa mara. Lazima wachezaji wajulishe wenzao kuhusu nafasi anazochukua kwa sababu mara nyingi anajitokeza sehemu ambazo hukutarajia."
Pambano lililosubiriwa kwa miaka mingi
Mtaalamu wa soka la Amerika Kusini, Tim Vickery, amesema huu ni mchezo ambao mashabiki wa Argentina wamekuwa wakiusubiri kwa muda mrefu.
"Haiwezekani Messi amalize zaidi ya mechi 200 za kimataifa bila kucheza dhidi ya England, timu ambayo mashabiki wengi wa Argentina wanaiona kama mpinzani wao mkubwa."
Alisema hata wakati wa robo fainali dhidi ya Uswisi, mashabiki wa Argentina walikuwa tayari wakiiwaza England, wakiruka na kuimba:
"Asiyeruka ni Mwiingereza."
Uhasama wenye historia ndefu
England na Argentina zina moja ya uhasama mkubwa zaidi katika soka la kimataifa.
Kuanzia bao maarufu la Diego Maradona la "Hand of God" kwenye robo fainali ya Kombe la Dunia mwaka 1986, hadi kadi nyekundu ya David Beckham kwenye Kombe la Dunia la 1998, mechi za mataifa haya mawili zimekuwa zikijaa drama na matukio yasiyosahaulika.
Hata hivyo, huu utakuwa mchezo wao wa kwanza kukutana ndani ya takribani miaka 21.
Cha kushangaza ni kwamba tangu Messi aanze kuchezea Argentina mwaka 2005, timu hizo zimekutana mara moja tu, lakini yeye hakushiriki.
Wakati huo alikuwa anatumikia adhabu ya kadi nyekundu aliyopata sekunde 30 tu baada ya kuingia uwanjani katika mechi yake ya kwanza ya kimataifa dhidi ya Hungary.
Katika mchezo huo dhidi ya Hungary, Messi aliingia kipindi cha pili lakini alionyeshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja baada ya kumpiga kiwiko beki Vilmos Vanczak.
Baadaye, England chini ya kocha Sven-Goran Eriksson iliifunga Argentina mabao 3-2 katika mechi ya kirafiki, huku Michael Owen akifunga mabao mawili ya dakika za mwisho.
Rekodi zinazomtisha kila mpinzani
Messi ndiye mchezaji aliyeichezea Argentina mechi nyingi zaidi na ndiye kinara wa mabao wa muda wote wa nchi hiyo. Hadhi yake iliongezeka zaidi baada ya kuiongoza Argentina kutwaa Kombe la Dunia mwaka 2022.
Takwimu zinaonyesha anapenda kufunga dhidi ya karibu kila timu anayokutana nayo.
Bolivia ndiyo timu anayoifunga zaidi, akiwa na mabao 11 katika mechi 12.
Ameifunga Venezuela na Ecuador mabao saba kila mmoja.
Amefunga mabao sita dhidi ya Uruguay na matano dhidi ya Brazil.
Barani Ulaya, amefunga mabao matatu dhidi ya Croatia, Uswisi na Ufaransa, huku mawili kati ya hayo dhidi ya Ufaransa yakija kwenye fainali ya Kombe la Dunia 2022.
Cha kushangaza zaidi, kati ya mataifa yote aliyokutana nayo zaidi ya mara moja, Qatar ndiyo pekee iliyofanikiwa kumzuia Messi kufunga, licha ya kucheza nayo mara mbili.
Sasa macho yote yataelekezwa Atlanta kuona kama nahodha huyo wa Argentina ataandika historia nyingine kwa kuikabili England kwa mara ya kwanza kabisa katika maisha yake ya kimataifa.