Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Argentina yatinga nusu fainali Kombe la Dunia, Uswisi ikiaga mashindano

Muktasari:

  • Mechi hiyo ya hatua ya robo fainali iliyopigwa kwenye Uwanja wa Kansas City uliopo katika Jimbo la Missouri, Marekani, ililazimika kuchezwa dakika 30 za muda wa nyongeza baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare ya bao 1-1.

KANSAS CITY, MAREKANI: MABAO mawili ya dakika ya 112 na 120+1, yaliyofungwa na Julian Alvarez na Lautaro Martinez yametosha kuihakikishia Argentina kufuzu hatua ya nusu fainali ya Kombe la Dunia 2026, baada ya kushinda 3-1 dhidi ya Uswisi.

Mechi hiyo ya hatua ya robo fainali iliyopigwa kwenye Uwanja wa Kansas City uliopo katika Jimbo la Missouri, Marekani, ililazimika kuchezwa dakika 30 za muda wa nyongeza baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare ya bao 1-1.

Katika mechi hiyo iliyokuwa ya kasi, ilishuhudiwa Argentina ikipata bao la mapema dakika ya 10, kupitia kwa kiungo, Alexis Mac Allister.

Mac Allister alifunga bao hilo kwa kichwa akitumia vyema pasi ya kona iliyopigwa na Lionel Messi na kuipatia uongozi Argentina hadi dakika 45 za kipindi cha kwanza licha ya Uswisi kutawala zaidi mechi hiyo ya kuvutia.

Asisti ya bao la Mac Allister iliyopigwa na Lionel Messi imemfanya kuandika rekodi mpya ya Kombe la Dunia ya  mchezaji anayeongoza kwa kupiga pasi nyingi zaidi za mwisho katika fainali hizo akifikisha 10.

Pasi hizo 10 za Messi zinamfanya aongoze katika historia ya Kombe la Dunia na kuwazidi mastaa wengine wakiwemo Edson Arantes do Nascimento 'Pele' wa Brazil na Fritz Walter wa Ujerumani ambao kila mmoja ana asisti tisa.

Wakati Uswisi ikiendelea kutengeneza mashambulizi, ilisawazisha bao hilo dakika ya 67, kupitia Dan Ndoye aliyetumia vyema pasi iliyopigwa na Ricardo Rodriguez.

Bao hilo liliipa nguvu Uswisi ingawa dakika ya 72, nyota wa timu hiyo, Breel Embolo alionyeshwa kadi ya pili ya njano iliyozalisha nyekundu na kikosi hicho kucheza pungufu kwa muda mrefu.

Licha ya Uswisi kumaliza mechi hiyo kwa sare ya bao 1-1 katika dakika 90 za kawaida, ila Argentina ilitumia vyema upungufu wa wapinzani wao na dakika ya 112, ilipata bao la pili lililofungwa na Julian Alvarez, kisha Lautaro Martinez akaongeza la tatu dakika ya 120+1 na kuihakikishia kikosi hicho kufuzu hatua ya nusu fainali.

Argentina ilifika hatua ya robo fainali ya Kombe la Dunia baada ya kuifunga Misri mabao 3-2, huku kwa upande wa Uswisi ikiitoa Colombia kwa mikwaju ya penalti 4-3, kufuatia suluhu ya (0-0) katika dakika 120, za mechi hiyo kali.

Ushindi huu kwa Argentina unaipeleka nusu fainali ya Kombe la Dunia 2026 na sasa itakutana na England iliyoitoa Norway kwa kuifunga mabao 2-1, baada ya mechi hiyo kuchezwa kwa dakika 120.

Katika mechi hiyo ya nusu fainali kati ya England dhidi ya Argentina ambayo inasubiriwa kwa hamu kubwa zaidi na mashabiki wa soka, itapigwa Julai 15, kwenye Uwanja wa Atlanta, Marekani.

Argentina ni timu yenye mafanikio makubwa katika historia ya Kombe la Dunia, ambapo kikosi hicho kimefika fainali sita na kuchukua ubingwa huo mara tatu ikianza mwaka 1978, ikiwa wenyeji kwa kuifunga Uholanzi mabao 3-1 katika muda wa nyongeza.

Ubingwa wa pili iliouchukua Argentina ni katika fainali za mwaka 1986, zilizofanyika Mexico, baada ya kuifunga Ujerumani Magharibi mabao 3-2, huku aliyekuwa nyota na gwiji wa kikosi hicho, Diego Maradona akiibuka mchezaji bora wa mashindano hayo.

Katika fainali za mwaka 1986, zinakumbukwa na mashabiki wa soka duniani, kwani ndizo zilizoibua bao la 'Mkono wa Mungu' (Hand of God) na 'Bao la Karne' (Goal of the Century) ya Diego Maradona aliyofunga dhidi ya England kwenye hatua ya robo fainali.

Taji la tatu la Kombe la Dunia ililochukua Argentina ni mwaka 2022, katika fainali zilizofanyika Qatar, ambapo kikosi hicho kiliichapa Ufaransa kwa penalti 4-2, baada ya sare ya mabao 3-3, kwenye mechi kali iliyopigwa Desemba 18, 2022.

Katika Kombe la Dunia 2022, nyota wa Argentina, Lionel Messi alikuwa mchezaji bora, baada ya kufunga mabao mawili kwenye fainali na moja likifungwa na Angel Di Maria huku Kylian Mbappe akiifungia Ufaransa mabao yote matatu yaani hat-trick.

Argentina pia imemaliza nafasi ya pili mara tatu, ikianza mwaka 1930, ilipochapwa na wenyeji Uruguay mabao 4-2 na fainali za mwaka 1990 nchini Italia ilichapwa na Ujerumani Magharibi bao 1-0, huku mwaka 2014 fainali zilizofanyika Brazil ikapoteza pia kwa bao 1-0 dhidi ya Ujerumani.

Kwa upande wa historia ya Uswisi katika Kombe la Dunia ni ndefu na yenye mafanikio ya kawaida ambapo timu hiyo inashiriki kwa mara ya 13 hadi sasa tangu ilipoanza mwaka 1934, 1938, 1950, 1954, 1962, 1966, 1994, 2006, 2010, 2014, 2018, 2022 na sasa 2026.

Katika Kombe la Dunia lililofanyika Ujerumani mwaka 2006, Uswisi ilitolewa katika hatua ya 16 bora bila ya kufungwa bao katika muda wa kawaida, kwani ilitolewa kwa penalti 3-0 dhidi ya Ukraine baada ya suluhu ya (0–0) dakika 120.

Uswisi ilikuwa ni timu ya kwanza katika historia ya Kombe la Dunia kuondolewa mashindanoni bila kufungwa bao kwa muda wa kawaida au nyongeza, ikiwa ni rekodi pia iliyotokea kwenye michuano hiyo iliyofanyika Ujerumani mwaka 2006.

Mbali na hilo, Uswisi iliandika rekodi mbovu pia kwani ilikuwa ni timu ya kwanza katika historia ya Kombe la Dunia kushindwa kufunga hata penalti moja baada ya sare kwenye mechi ya mtoano, kufuatia kukosa zote tatu dhidi ya Ukraine.

Mafanikio makubwa kwa Uswisi ni kufika hatua ya robo fainali ya Kombe la Dunia mara nne, ikiwemo lililofanyika mwaka 1934 nchinj Italia, 1938 (Ufaransa), 1954, ilipokuwa mwenyeji na sasa 2026 linalofanyika nchi za Marekani, Canada na Mexico, haijawahi kuvuka hapo.