Merino: Sina wasiwasi na Gyökeres, atafunga sana
Muktasari:
- Gyökeres raia wa Sweden, alijiunga na Arsenal msimu huu wa majira ya joto akitokea Sporting CP ya Ureno kwa dau la Pauni 63.5 milioni, lakini bado hajatimiza matarajio ya mashabiki na klabu hiyo. Akiwa na Sporting msimu uliopita, Gyökeres alifunga mabao 54 katika mashindano yote, lakini hajafanikiwa kuendeleza makali hayo nchini England.
Nyota wa Arsenal, Mikel Merino anaamini kuwa mshambuliaji wa timu hiyo, Viktor Gyökeres, atang'ara klabuni hapo ikiwa atapewa muda zaidi, licha ya kuwa hajafunga bao katika mechi tisa mfululizo kwa klabu na timu ya taifa.
Gyökeres raia wa Sweden, alijiunga na Arsenal msimu huu wa majira ya joto akitokea Sporting CP ya Ureno kwa dau la Pauni 63.5 milioni, lakini bado hajatimiza matarajio ya mashabiki na klabu hiyo. Akiwa na Sporting msimu uliopita, Gyökeres alifunga mabao 54 katika mashindano yote, lakini hajafanikiwa kuendeleza makali hayo nchini England.
Mshambulaiji huyo mwenye umri wa miaka 27, alishafunga mabao mawili dhidi ya Leeds United katika ushindi wa 5-0 mwezi Agosti 2025, na pia bao moja kwenye ushindi wa 3-0 dhidi ya Nottingham Forest. Hata hivyo, tangu katikati ya Septemba 2025, hajafunga katika mechi saba mfululizo alizocheza.
Kwa upande wa timu ya taifa ya Sweden, hali haijawa bora zaidi akiwa amerudi kutoka mapumziko ya kimataifa bila bao, baada ya kupoteza 2-0 dhidi ya Uswisi na 1-0 dhidi ya Kosovo.
Hii inaashiria mechi tisa mfululizo bila bao kwa Gyökeres, lakini kwa mujibu wa Merino, amesema hali hiyo inapaswa kuvumiliwa, kwani anaamini mshambuliaji huyo atafanya vizuri.
"Nina uhakika mabao yatakuja, nina hakika yeye mwenyewe anataka kufunga kama mchezaji yeyote yule. Pia nina hakika anatoa mchango mkubwa kwa wachezaji wenzake, hata bila mpira.
"Kila mmoja hapa Arsenal anahitaji upendo, anahitaji kuhisi yuko kwenye mazingira mazuri. Viktor ni mfano tu, lakini kila mtu anatamani aendelee kufanya anachofanya. Cha muhimu zaidi ni kwamba timu inashinda.
"Ana uwezo, ana nguvu za kimwili, na ana wachezaji bora pembeni yake. Lakini hatuwezi kuangalia tu takwimu. Ukiangalia mechi zake utaona ni kiasi gani anavyotupatia," amesema Merino.
Licha ya kukosekana kwa mabao kutoka kwa Gyokeres, Arsenal kwa sasa inaongoza Ligi Kuu ya EPL, ikiwa na pointi tatu zaidi ya Manchester City na pointi nne mbele ya mabingwa watetezi Liverpool.
Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta kwa sasa anageuza mawazo yake katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, ambapo Arsenal inajiandaa kuikaribisha Atletico Madrid kwenye Uwanja wa Emirates, leo Jumanne Oktoba 21, 2025.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari, Arteta amefafanua kile Arsenal inatarajia kukikabili dhidi ya kikosi cha Diego Simeone akisema: "Kwanza kabisa, ni ile hamu ya kushinda. Unaweza kuhisi hilo katika kila mpira, kila umbali wanaokimbia. Ni kuhusu ushindani wao, na baada ya hapo jinsi wanavyocheza.
"Nadhani kuna tofauti kati ya hayo mawili, na ili kuelewa kikamilifu wanachokifanya, ni lazima kutambua kiwango chao cha nidhamu na mpangilio. Wamekuwa wakikusanya vipaji kwa miaka mingi, vipaji ambavyo vinaendana kikamilifu na mbinu zao, na wana uwezo mkubwa wa kutumia fursa hizo vizuri."