Mechi za ufunguzi zaitesa Hispania Kombe la Dunia
Muktasari:
- Suluhu iliyoipata leo katika mechi ya kundi H dhidi ya Cape Verde, imeifanya timu hiyo kushinda mechi moja ya ufunguzi ya Kombe la Dunia kati ya tano zilizopita.
ATLANTA, MAREKANI: REKODI za mechi za ufunguzi kwa timu ya Hispania zimeendelea kukitesa kikosi hicho katika michuano ya Kombe la Dunia.
Suluhu iliyoipata leo katika mechi ya kundi H dhidi ya Cape Verde, imeifanya timu hiyo kushinda mechi moja ya ufunguzi ya Kombe la Dunia kati ya tano zilizopita.
Katika fainali za Kombe la Dunia 2010 zilizofanyika Afrika Kusini, timu hiyo ilianza michuano hiyo kwa kichapo cha bao 1-0, dhidi ya Uswisi Juni 16, 2010.
Licha ya kuanza kwa kichapo 2010, lakini Hispania ilitwaa ubingwa wanKombe la Duniabaada ya kuifunga Uholanzi bao 1-0, Julai 11, 2010, lililofungwa na aliyekuwa kiungo nyota wa kikosi hicho, Andres Iniesta dakika ya 116.
Katika fainali za Kombe la Dunia la 2014 zilizofanyika Brazil, timu hiyo ilianza kwa fedheha baada ya kuchapwa mabao 5-1 na Uholanzi, Juni 13, 2014, ikiwa ni kisasi cha fainali ya 2010, Afrika ya Kusini.
Fainali za Kombe la Dunia 2018, zilizofanyika Russia, timu hiyo ilitoka sare ya mabao 3-3 dhidi ya Ureno katika mechi ya kwanza ya ufunguzi iliyopigwa, Juni 15, 2018, huku nyota wa Ureno, Cristiano Ronaldo akifunga mabao matatu (hat-trick).
Fainali zilizofuata 2022 zilizofanyika Qatar, Hispania ilianza vyema mechi ya kwanza ya hatua ya makundi baada ya kuifunga Costa Rica mabao 7-0 Novemba 23, 2022.
Katika fainali za mwaka huu wa 2026, zinazofanyika Marekani, Mexico na Canada, Hispania imeshindwa kutamba baada suluhu dhidi ya Cape Verde, huku kipa wa kikosi hicho, Josimar Jose Evora Dias 'Vozinha' akiwa shujaa kutokana na kuchomoa michomo mingi ya hatari.