Ubelgiji, Misri ngoma ngumu Kombe la Dunia
Muktasari:
- Mapema tu Misri ilifanikiwa kuwashtua Ubelgiji ikipata bao zuri dakika ya 19, mfungaji akiwa kiungo mshambuliaji Emam Ashour kwa shuti kali, akipokea asisti kutoka kwa nahodha wake, Mohammed Salah.
BAO la kujifunga kwa beki wa Misri, Mohammed Hany dakika ya 66, limetosha kuinusuru Ubelgiji kulala katika mechi ya kwanza kundi G katika Kombe la Dunia 2026, timu hizo zikitoka sare ya bao 1-1.
Mapema tu Misri ilifanikiwa kuwashtua Ubelgiji ikipata bao zuri dakika ya 19, mfungaji akiwa kiungo mshambuliaji Emam Ashour kwa shuti kali, akipokea asisti kutoka kwa nahodha wake, Mohammed Salah.
Bao hilo likatosha kuzipeleka timu hizo mapumziko, Misri ikitoka kifua mbele huku Ubelgiji ikionyesha kiwango kizuri cha umiliki wa mchezo.
Ubelgiji itajilaumu yenyewe kutokana na kutengeneza nafasi nyingi za kufunga lakini ikashindwa kuzitumia.
Baada ya kuikalia sana kooni Misri, Ubelgiji ikafanikiwa kupata bao hilo kwa kujifunga Hany wakati akipambana kuzuia shambulizi.
Kabla ya Hany kujifunga bao hilo, pongezi nyingi zitamuendea mshambuliaji wa Ubelgiji, Romelu Lukaku ambaye alikuwa ameingia wakati huo uwanjani na kuhusika kwenye shambulizi lake la kwanza.
Lukaku alifanikiwa kukaa katikati ya mabeki wa Misri hatua ambayo ikamlazimu Hany kujifunga wakati anapambana kudhibiti mpira wa krosi uliokuwa unamtafuta Lukaku.
Kipindi cha pili bado Ubelgiji iliikalia kooni Misri lakini ikakosa utulivu kumalizia nafasi ambazo imezitengeneza.
Mpaka mwisho wa mchezo huo uliochezwa Uwanja wa Seattle jijini Washington nchini Marekani, Ubelgiji ikamaliza kwa kugawana pointi moja moja dhidi ya Misri.