Kipa babu Cape Verde aikazia Hispania
Muktasari:
- Kama kuna mchezaji wa Cape Verde atakumbukwa na Hispania basi ni kipa mkongwe Josimar José Évora Dias 'Vozinha' ambaye amekuwa na dakika 90 bora za kulinda vyema lango la Taifa lake.
HISPANIA imeanza Fainali za Kombe la Dunia 2026 kwa matokeo ya kushtua baada ya kushindwa kufungana na Cape Verde, kwenye mchezo ilioutawala kwa muda wote wa dakika 90.
Kama kuna mchezaji wa Cape Verde atakumbukwa na Hispania basi ni kipa mkongwe Josimar José Évora Dias 'Vozinha' ambaye amekuwa na dakika 90 bora za kulinda vyema lango la Taifa lake.
Vozinha aliyezaliwa miaka 40 iliyopita huko Mindelo nchini Cape Verde, amekuwa mwiba kwa Hispania, akizima mashambulizi yao ya wazi ambapo aliokoa michomo sita ya wazi.
Cape Verde ilitumia muda mwingi kujilinda ikicheza na wachezaji 10 wakati ikizuia, huku ikishambulia kwa mashambulizi ya kushtukiza.
Hispania ikianza na mastaa wake Rodrigo Hernandez 'Rodri', Pedro Lopez 'Pedri', Pablo Gavira 'Gavi' ikashindwa kufungua ukuta huo mgumu wa Cape Verde licha ya kuwashambulia karibu muda wote wa mchezo.
Kipindi cha pili licha ya Hispania kuwaingiza mastaa wengine wakali kama Lamine Yamal na Dani Olmo, bado Cape Verde ilikomaa na kumaliza dakika tisini bila ya kuruhusu bao ikionyesha uimara mkubwa wa kuzima mashambulizi hayo.
Mpaka mwisho wa mchezo huo wa Kundi H, timu hizo zilishindwa kufungana lakini Cape Verde ndio ikageuka kama washindi kwa kupata pointi moja dhidi ya Hispania yenye mastaa wakubwa duniani.