Mechi tano muhimu Ulaya zitakazoamua mbio za ubingwa
Muktasari:
- Lakini, ukweli ni soka si kila mara linatoa hadithi za kusisimua. Mara nyingi baadhi ya timu hushinda mataji mapema kwa sababu zinakuwa zimewaacha wapinzani wao mbali sana kwenye msimamo wa ligi.
LONDON, ENGLAND: HAKUNA kitu kinachovutia zaidi katika mchezo wa soka kama mbio za ubingwa zinapoamuliwa katika dakika za mwisho za msimu. Unakumbuka lile tukio la bao la la Sergio Aguero lililowapa Manchester City ubingwa kwa namna ya kusisimua?
Lakini, ukweli ni soka si kila mara linatoa hadithi za kusisimua. Mara nyingi baadhi ya timu hushinda mataji mapema kwa sababu zinakuwa zimewaacha wapinzani wao mbali sana kwenye msimamo wa ligi.
Kwa sasa, wastani wa tofauti ya pointi kati ya vinara wa ligi na timu za nafasi ya pili katika ligi tano kubwa barani Ulaya ni takribani pointi 7.2, huku takribani mechi tisa zikiwa zimebaki kumaliza msimu.
Bayern Munich tayari inaonekana kukaribia kutwaa ubingwa wa Bundesliga, kwani inaongoza kwa pointi 11 mbele ya Borussia Dortmund, ambao hawatakutana nao tena katika mechi zilizobaki.
Hata hivyo, kuna baadhi ya mechi za moja kwa moja kati ya wapinzani wa ubingwa ambazo zinaweza kufanya mbio za ubingwa ziendelee kuwa na ushindani mkubwa. Hizi hapa ni baadhi ya mechi muhimu.
Polish Ekstraklasa: Zaglebie Lubin vs Lech Poznan
Mechi: Machi 15
Pointi kwa sasa: Lubin 41, Poznan 38
Nchi ya Poland mara nyingi haipati sifa kubwa katika soka la Ulaya, lakini ligi yake ya Ekstraklasa inaweza kuwa moja ya ligi zinazopuuzwa zaidi barani humo.
Kwa kuwa mabingwa wa mara kwa mara Legia Warsaw wanapambana kukwepa kushuka daraja, mbio za ubingwa zimekuwa wazi zaidi, huku timu nne za juu zikitofautiana kwa pointi nne tu.
Jumapili ijayo, Lech Poznan itasafiri kucheza dhidi ya vinara Zaglebie Lubin.
Ikiwa Poznan itashinda, itafikisha pointi sawa na wapinzani wao na hapo mbio za ubingwa zitakuwa zimekaa patamu.
Ligue 1: Lens vs PSG
Mechi: Aprili 11
Pointi kwa sasa: PSG 57, Lens 56
Kwa kawaida ni rahisi kutabiri mshindi wa Ligue 1, kwa sababu mara nyingi Paris Saint-Germain huwa na nguvu kubwa kuliko wapinzani wao.
Lakini, msimu huu mambo yanaweza kuwa tofauti, kwani RC Lens iko karibu sana, wakitofautiana kwa pointi moja tu. Haya ni mafanikio makubwa ukizingatia msimu uliopita Lens ilimaliza ikiwa nyuma ya PSG kwa pointi 32, na msimu uliotangulia ilikuwa nyuma kwa pointi 25.
Lens iliwahi kushinda ubingwa wa Ufaransa mara moja tu mwaka 1998, na wakati huo walitwaa taji kwa tofauti ya mabao.
Premier League: Man City vs Arsenal
Mechi: Aprili 19
Pointi kwa sasa: Arsenal 67, Man City 60
Arsenal inaongoza mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England baada ya kumaliza nafasi ya pili kwa misimu mitatu mfululizo.
Huenda huu ukawa mwaka ambao hatimaye wakatwaa ubingwa kwa mara ya kwanza katika kipindi cha zaidi ya miaka 22.
Hata hivyo, pengo lao la pointi saba halimaanishi ushindi tayari. Manchester City ina mechi moja mkononi na bado watakutana ana kwa ana na Arsenal mwezi ujao.
Ikiwa Man City itashinda kiporo chake na kisha kuwafunga Arsenal, tofauti ya pointi inaweza kupungua hadi moja tu.
Zaidi ya hayo, Man City ina uzoefu mkubwa wa kushinda mataji katika miaka ya hivi karibuni, jambo linalowafanya kuwa tishio kubwa kwa kikosi cha kocha Mikel Arteta.
Turkish Super Lig: Galatasaray vs Fenerbahce
Mechi: Aprili 26 (inaweza kubadilika)
Pointi kwa sasa: Galatasaray 61, Fenerbahce 57
Derby ya Istanbul kati ya Galatasaray na Fenerbahce daima huwa na ushindani mkali.
Msimu uliopita Galatasaray ilitwaa ubingwa wa Turkish Super Lig kwa tofauti ya pointi 11. Kwa sasa inaongoza kwa pointi nne juu ya Fenerbahce.
Msimu huu Fenerbahce bado hawajapoteza hata mechi moja ya ligi na zitakutana zenyewe mwezi ujao katika moja ya mechi itakayotoa taswira halisi ya mbio za ubingwa kwenye Ligi Kuu Uturuki.
LaLiga: Barcelona vs Real Madrid
Mechi: Mechi 10 (inaweza kubadilika)
Pointi kwa sasa: Barcelona 67, Real Madrid 63
Hatimaye, wapinzani wakubwa wa kihistoria watakutana katika mechi ambayo inaweza kuamua ubingwa wa La Liga.
Kwa sasa Barcelona inaongoza kwa pointi nne juu ya Real Madrid huku mechi 11 zikiwa zimebaki.
Kabla ya El Clasico, timu zote mbili pia zitacheza dhidi ya Atletico Madrid, jambo ambalo linaweza kubadilisha hali ya mbio za ubingwa.
Msimu uliopita zilikutana katika hatua kama hii ya msimu na Barcelona ilishinda 4–3, ushindi uliowasaidia sana kutwaa ubingwa. Safari hii pia El Clasico inaweza kuwa mechi ya kuamua hatma ya ubingwa wa ligi hiyo.