Kuna jambo Morocco inayoendelea ilipoishia
Muktasari:
- ACHANA na mechi zilizopigwa usiku wa kumkia leo, kama uliwafuatilia Morocco uliona namna walivyokomaa na safari yao waliyoianzisha miaka minne iliyopita kule Qatar walikotinga robo fainali ya Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza.
OTTAWA, CANADA: ACHANA na mechi zilizopigwa usiku wa kumkia leo, kama uliwafuatilia Morocco uliona namna walivyokomaa na safari yao waliyoianzisha miaka minne iliyopita kule Qatar walikotinga robo fainali ya Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza.
Na juzi, kwenye Uwanja wa Monterrey, Canada walifanya kilekile wakiendelea na walipoishia walioifunga Uholanzi kwa penalti 3-2 baada ya kumalizana dakika 120 kwa sare ya bao 1-1.
Kocha mpya Mohamed Ouahbi, ameendelea kusimamia maendeleo ya Morocco katika Kombe la Dunia, huku falsafa yake ya wazi na matumizi ya vipaji kutoka diaspora ikiweka msingi wa uwezekano wa kubadili viwango vya soka la Afrika na pengine duniani na haishangazi kwamba huenda safari hii wakafika mbali zaidi.
Baada ya mtangulizi wake, Walid Regragui kuhitimisha safari ya Morocco kwenye Kombe la Dunia 2022 kwa kumaliza nafasi ya nne, alitoa ujumbe wa matumaini kwa siku zijazo akisisitiza ndoto ya taifa hilo kufikia ubingwa wa dunia siku moja iko karibu.
Alisema: “Tunataka kuwapa watoto wetu DNA ya soka na siku moja tutaweza kushinda Kombe la Dunia. Tunaijenga DNA hiyo hatua kwa hatua ili timu iweze kutimiza ndoto ya Afrika.”
Wakati huo, mafanikio ya Morocco yalionekana kama muujiza wa muda mfupi baada ya kuifunga Ubelgiji na Croatia na kuziondoa Hispania na Ureno, ingawa walifunga mabao mawili tu katika mechi nne za mwisho Qatar. Miaka minne baadaye, Morocco imeendelea kuonyesha kuwa mafanikio hayo hayakuwa ya bahati. Ikiwa safari yao ya sasa itaishia hatua ya 16, bado itaonekana kama timu inayoimarika kwa muda mrefu. Timu hiyo kwa sasa imeorodheshwa nafasi ya sita na saba kwa viwango vya Shirikisho la Soka Duania (Fifa), ikionyesha kuwa bado ni miongoni mwa mataifa makubwa yanayoinukia kwa kasi.
Tofauti na historia ya awali ambapo timu za Afrika zilizofika robo fainali zilishindwa kuendeleza mafanikio, Morocco inaonekana kujenga mfumo endelevu wa ushindani.
Katika mabadiliko ya uongozi, Regragui ameondoka na nafasi yake kuchukuliwa na Ouahbi, ambaye ameendeleza falsafa ya ushindani na mchezo wa wazi zaidi, ikiwemo mechi dhidi ya Brazil iliyoisha kwa sare ya bao 1-1, kisha ikaichapa Scotland bao 1-0 na kuhitimisha safari ya makundi kwa ushindi wa mabao 4-2 dhidi ya Haiti.
Morocco pia imebadilisha kikosi chake kwa kiasi kikubwa. Wachezaji muhimu wa 2022 kama Hakim Ziyech na Sofiane Boufal hawapo tena, huku Romain Saiss akiwa amestaafu soka la kimataifa, na Youssef En-Nesyri akiondolewa kwenye kikosi.
Hata hivyo, wachezaji kama Yassine Bounou, Achraf Hakimi, Noussair Mazraoui na Azzedine Ounahi bado wana nafasi muhimu ndani ya timu.
Mfumo wa Morocco pia unaendelea kunufaika na wachezaji wanaozaliwa au kukulia Ulaya kutokana na kuwa na nasaba (DNA) za taifa hilo.
Wachezaji kama Mazraoui na Sofyan Amrabat walizaliwa Uholanzi, huku wengine wakizaliwa ama Ufaransa, Hispania au Ubelgiji.
Miongoni mwa vipaji vipya tofauti na 2022 ni Brahim Diaz, Ismael Saibari, na viungo chipukizi kama Ayyoub Bouaddi na Neil El Aynaoui, wanaoonyesha uwezo mkubwa katika soka la Ulaya.
Hatua hii imeifanya Morocco kuwa na kikosi chenye mchanganyiko wa uzoefu na vipaji vya kimataifa, huku pia kikionyesha mabadiliko ya kimkakati katika soka la Afrika.
Kwa sasa, Morocco inaendelea kuonekana kama moja ya mataifa yanayoweza kuandika upya historia ya Afrika kwenye Kombe la Dunia, huku safari yao hatua ya 16 bora ikitarajiwa kuwa kipimo kingine muhimu cha maendeleo hayo.
VS UHOLANZI
Morocco walizalisha wastani wa mabao yanayotarajiwa 1.4 kutokana na mashuti 11, matano kati ya hayo yakihesabiwa kama “nafasi kubwa”, huku Hakimi akiwa tishio la mara kwa mara.
Morocco sasa wameshinda mikwaju yote miwili ya penalti katika Kombe la Dunia, pia wakiifunga Hispania katika hatua ya 16 bora ya 2022, na bila shaka watajiona wana nafasi dhidi ya Canada katika hatua inayofuata.
Uholanzi, kwa upande mwingine, walianza mchezo wakiwa na safu ya mabeki watano kwa mara ya kwanza tangu Machi 2024 (kwenye kipigo cha mabao 2-1 dhidi ya Ujerumani), wakicheza mechi 31 zilizofuata wakiwa na mabeki wanne.
Uholanzi walionekana kukosa mwelekeo, wakipiga mashuti sita tu yenye thamani ndogo zaidi katika dakika 120 za mchezo, lakini kiungo Cody Gakpo aliwaweka mbele kama kawaida kwa bao lake.
Ni Dennis Bergkamp (10) pekee aliyeifungia Uholanzi mabao mengi zaidi katika mashindano makubwa (Euro au Kombe la Dunia) kuliko Gakpo (9), huku Johnny Rep pekee (7) akimzidi Gakpo mwenye mabao sita katika Kombe la Dunia.
Katika mchezo huo kipa wa Uholanzi, Bart Verbruggen alijitahidi kuokoa mchezo, akifanya sevu tano na kukaribia sana kuokoa penalti ya Rahimi, lakini haikutosha kwa kikosi hicho wakati huu.
NAMBA HIZI HAPA
Katika mchezo huo, kiungo wa Morocco, Neil El Aynaoui alikamilisha pasi 134 dhidi ya Uholanzi na katika Kombe la Dunia 2026 ni Leandro Paredes pekee aliyekamilisha pasi nyingi zaidi katika mchezo mmoja (153 dhidi ya Jordan).
Bao la Morocco lililofungwa na Issa Diop dakika ya 90:05 lilikuwa bao la pili la kuchelewa zaidi katika mechi ya Kombe la Dunia, baada ya lile la Zakaria Aboukhlal la dakika 91:51 dhidi ya Ubelgiji 2022.
Uholanzi sasa wana wachezaji saba waliofunga angalau mabao sita katika Kombe la Dunia tangu 1966. Hiyo ni sawa na Brazil kwa idadi ya pili kubwa ya wachezaji wenye mabao angalau sita katika rekodi, nyuma ya Ujerumani wenye wanane.
Bao la sita la Gakpo katika Kombe la Dunia limefanya afungane kwa nafasi ya pili kwa mabao mengi zaidi kwa Uholanzi katika historia, nyuma ya Johnny Rep mwenye saba.
Ukiachana na hayo, Hakimi alifungana na Ismael Saibari kwa miguso mitano ndani ya boksi la wapinzani, Uholanzi, katika mchezo huo, ikiwa ni idadi kubwa zaidi kwa mchezaji wa Morocco.
Hakimi kwa jumla ana miguso 30 ndani ya boksi katika mechi za Kombe la Dunia, ikiwa ni mingi zaidi kwa mchezaji wa Morocco katika historia.
Na Uholanzi katika mchezo huo waliuanza wakiwa na mabeki watano kwa mara ya kwanza tangu Machi 26, 2024 (walipochapwa 2-1 na Ujerumani), wakicheza mechi 31 zilizofuata wakiwa na wanne.
MAAJABU MECHI MBILI ZINGINE
Kabla ya Morocco na Uholanzi kumaliza baadaye, timu hizo zilitanguliwa na wababe wengine wakianza Brazil dhidi ya Japan na hizi ndizo zilizokuwa takwimu zao.
Kwa wastani wa umri wa kikosi cha kwanza cha Brazil (miaka 29 na siku 245) kilikuwa ndicho chenye umri mkuwa zaidi kwa mechi ya hatua ya mtoano ya Kombe la Dunia tangu walipofungwa na Ufaransa 2006 (miaka 30 na siku 31).
Ni Pele pekee 970 (6) aliyetoa pasi za mwisho nyingi zaidi kwa Brazil katika shindano moja la Kombe la Dunia kuliko Bruno Guimaraes 2026 (4).
Hata hivyo, Casemiro (miaka 34 na siku 126) ni mfungaji wa pili mwenye umri mkubwa zaidi kwa Brazil katika Kombe la Dunia, nyuma ya Bebeto dhidi ya Denmark 1998 (miaka 34 na siku 137).
Japan kwa upande wao wameongeza rekodi ya kucheza mechi nyingi zaidi za hatua ya mtoano katika Kombe la Dunia bila kufuzu hata mara moja (0/5).
Huu ulikuwa ushindi wa pili tu kwa Brazil katika mechi tisa zilizopita za Kombe la Dunia walizokuwa wakicheza wakiwa nyuma (sare moja na vipigo sita) na ushindi wao wa kwanza tangu mchezo wa ufunguzi wa 2014 dhidi ya Croatia (3-1).
Mbali ya mchezo huo, wababe Ujerumani walikula za uso mbele za Paraguay walipofungwa kwa penalti 4-3 baada ya kutoshana jasho kwa bao 1-1 ndani ya dakika 120.
Kitakwimu Ujerumani wameondolewa katika mechi ya pili tu kati ya 10 za mwisho za hatua ya mtoano ya Kombe la Dunia, baada ya pia kufungwa na hispania (1-0) katika nusu fainali ya 2010.
Paraguay wamefuzu katika droo yao ya pili tu ya hatua ya mtoano ya Kombe la Dunia, zote zikipatikana kupitia ushindi wa penalti (walishinda 5-3 dhidi ya Japan katika hatua ya 16 bora 2010).
Ujerumani walipoteza mikwaju yao ya kwanza kabisa ya penalti katika Kombe la Dunia (mikwaju yao ya tano), na pia ni kipigo chao cha pili tu katika mashindano makubwa (Kombe la Dunia na Euro), pia wakifungwa na Czechoslovakia katika fainali ya Euro 1976.
Kuna tofauti ya nafasi 31 katika viwango vya Fifa kabla ya mashindano kati ya Ujerumani (iliyopo nafasi ya 10) na Paraguay (41), ikiwa ni mojawapo ya tofauti kubwa zaidi katika matokeo ya kuondolewa katika hatua ya mtoano tangu 1994.
Na Ujerumani walikuwa na umiliki wa mpira wa asilimia 75.4 katika mchezo huo, ikiwa ni kiwango cha tatu cha juu zaidi kwenye rekodi tangu 1966 katika mechi ya Kombe la Dunia ya mtoano huku wakifungwa mabao katika mechi 10 mfululizo za Kombe la Dunia ukiwa ni mfululizo wao mrefu zaidi kuwahi kutokea katika historia ya mashindano.
Julio Enciso amehusika moja kwa moja katika mabao yote matatu ya Paraguay katika Kombe la Dunia 2026 (bao moja, asisti mbili za mwisho), na ni Oleg Salenko wa Russia pekee (mabao saba 1994) aliyekuwa na mchango mkubwa zaidi kwa mabao ya timu yake katika asilimia 100 ya mabao ya taifa katika shindano moja.
Ni Bruno Guimaraes (4) pekee aliyetoa pasi nyingi zaidi za mabao katika Kombe la Dunia 2026 kuliko Florian Wirtz wa Ujerumani (3), huku mchezaji wa mwisho wa taifa hilo kufanya hivyo zaidi katika shindano moja moja akiwa Michael Ballack 2002 (4).
Pamoja na hayo kumekuwapo na mabao 33 ya kichwa katika Kombe la Dunia 2026 (kabla ya mechi za jana usiku), ikiwa ni chini kidogo ya rekodi ya 2002 (35).
Mshambuliaji wa Ujerumani, Kai Havertz alifunga bao lake la 25 la kimataifa katika mechi yake ya 62; pia amefunga mabao mengi zaidi kwa nchi hiyo chini ya kocha Julian Nagelsmann kuliko mchezaji mwingine yeyote (12).
Lakini, bao la Julio Enciso lilikuwa la kwanza kabisa la Paraguay katika hatua ya mtoano ya Kombe la Dunia, baada ya kushindwa kufunga katika mechi zao tano zilizopita za mtoano.
Na kwa kipa wa Ujerumani, Manuel Neuer alicheza mchezo wake wa 23 akianzia katika Kombe la Dunia, huku ni Lionel Messi (26) pekee aliyefanya zaidi yake katika historia ya mashindano hayo.