MCHUANO: Diego Costa katika vita ya Lukaku na Torres

Muktasari:
Vita ya namba sasa kwenye kikosi hicho katika safu ya ushambuliaji imebaki kwa wakali watatu; Costa, Torres na Lukaku.
CHELSEA imemnyakua straika Diego Costa na kumsainisha mkataba wa miaka mitano. Ni muda mrefu na kama staa huyo Mhispaniola atakuwa kwenye ubora wake, basi Chelsea watamfaidi kwelikweli.
Hata hivyo, kutua kwake Stamford Bridge kunamfanya kwenda kuungana na mastraika Fernando Torres na Romelu Lukaku.
Samuel Eto’o na Demba Ba hawatakuwapo kwenye kikosi hicho msimu ujao. Eto’o ameachwa huru baada ya mkataba wake kumalizika na Ba ametimkia Uturuki kwenye klabu ya Besiktas.
Vita ya namba sasa kwenye kikosi hicho katika safu ya ushambuliaji imebaki kwa wakali watatu; Costa, Torres na Lukaku.
Kwa msimu uliopita, Lukaku alikuwa akicheza kwa mkopo Everton. Lakini, mastraika watatu waliokuwa kwenye kikosi cha Chelsea, Torres, Eto’o na Ba kwa ujumla mabao yao yote hawakumfikia Costa.
Akiwa na kikosi cha Atletico Madrid msimu uliopita, Costa aliyezaliwa Brazil na kisha kuchukua uraia wa Hispania amefunga mabao 36, mabao matano zaidi ya yale yaliyofungwa na mastraika watatu wa Chelsea kwa msimu uliopita, Ba, Torres na Eto’o. Mastraika hao butu walifunga mabao 31.
Kwa kuzitazama takwimu za washambuliaji hao kwa mabao yao ya msimu uliopita, Costa anawafunika wote akiwamo Lukaku aliyekuwa kwenye kikosi cha Everton.
Kwenye Ligi ya La Liga pekee, Costa, 25, alifunga mabao 27, wakati Lukaku alifunga mabao 15 kwenye Ligi Kuu England na Torres amefunga mabao matano tu.
Ni kitu kisichopingika kwamba Lukaku atafunga mabao mengi kama atapewa muda wa kutosha wa kucheza kwenye kikosi hicho cha Chelsea kwa msimu ujao hasa akiwa na uhakika wa kupata mipira kutoka kwa viungo matata, Eden Hazard, Oscar, Willian na Cesc Fabregas.
Tofauti ya washambuliaji hao ni uwezo wa kufunga kwa nafasi walizopata. Costa alifunga karibu robo ya nafasi zote alizopata msimu uliopita, wakati Lukaku umakini wake kwenye kutumia nafasi ni asilimia 15 na Torres ni asilimia 8.2.
Torres ana faida moja kwamba amefunga kutokana na mashuti machache sana aliyopiga golini ukilinganisha na Costa na Lukaku.
Kutokana na kucheza kwa kujiamini zaidi, Torres wakati mwingine amekuwa akicheza pembeni na kurudi katikati kuchukua mipira na kupanda nayo mbele, wakati Costa na Lukaku staili yao ya kucheza ni kwamba hawaondoki kwenye boksi la lango la wapinzani.
Kutokana na Mourinho kusajili wachezaji wenye uwezo wa kuwachezesha washambuliaji, mastraika kama Lukaku na Costa watakuwa na nafasi kubwa ya kung’ara tofauti na Torres ambaye anacheza mbali sana na goli. Lukaku na Costa uchezaji wao ni kama alivyokuwa akicheza Didier Drogba klabuni hapo.
Kwa hesabu za kwenye karatasi, Costa anatazamwa kama moja ya usajili makini uliofanywa na kocha Jose Mourinho licha ya kwamba kila kitu kinasubiriwa wakati msimu mpya utakapoanza na kila atakachokionyesha ndani ya uwanja.