Mbappe, Real Madrid wavutana mashati
Muktasari:
- Mvutano huu umeibuka katika wakati mbaya kwa vigogo hao wa Hispania, ambao bado wanakumbwa na maumivu ya kipigo cha kushtukiza cha nyumbani dhidi ya Getafe kilichopunguza kwa kiasi kikubwa matumaini yao ya ubingwa wa La Liga msimu huu.
MADRID, HISPANIA: REAL Madrid imeingia kwenye mvutano wa ndani baada ya kuzuka kwa tofauti kubwa ya maoni kati ya uongozi wa klabu na watu wa karibu wa Kylian Mbappe kuhusu muda sahihi wa mshambuliaji huyo kupona majeraha yanayomsumbua kwa sasa.
Wakati Madrid ikitamani sana nyota wao namba 10 awe tayari kwa mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Manchester City ambayo ni muhimu, watu wa karibu na Mbappe wameripotiwa kushtushwa na wazo hilo kwani wanaamini bado atakuwa hajapona kikamilifu.
Mvutano huu umeibuka katika wakati mbaya kwa vigogo hao wa Hispania, ambao bado wanakumbwa na maumivu ya kipigo cha kushtukiza cha nyumbani dhidi ya Getafe kilichopunguza kwa kiasi kikubwa matumaini yao ya ubingwa wa La Liga msimu huu.
Licha ya Madrid kutamka hadharani haitolazimisha kumrudisha Mbappe mapema katika majukumu yake, watu wa karibu na Mbappe wanadai hali ya kiafya ya staa huyo ni tete zaidi kuliko ilivyoelezwa.
Ripoti ya mwandishi wa habari, Anton Meana wa kituo cha Cadena SER, inaeleza jeraha la Mbappe ni kubwa sana tofauti na inavyodhaniwa, hivyo itamchukua muda mrefu kabla ya kurudi uwanjani.
Tofauti kati ya taarifa ya kitabibu ya klabu na tathmini ya watu wa karibu na mchezaji imeacha moshi wa sintofahamu juu ya lini Mbappe ataonekana uwanjani.
Real Madrid ilitoa taarifa rasmi Jumanne ya wiki hii ikisema: "Baada ya vipimo kufanywa kwa mchezaji wetu Kylian Mbappe na madaktari bingwa wa Ufaransa, chini ya usimamizi wa Kitengo cha Madaktari cha Real Madrid, imethibitishwa ana shida katika goti lake na kwa sasa matibabu yanaendelea, tunangoja kuona itakavyokuwa.”
Watu wa karibu na Mbappe wana wasiwasi mkubwa ikiwa Mbappe atacheza katika kikosi cha Madrid katika siku za hivi karibuni, inaweza kusababisha asipone kikamilifu au akaongeza ukubwa wa jeraha hivyo asiwe tayari kucheza Kombe la Dunia ambalo imebaki siku 99 kabla ya kuanza.
"Jeraha ni kubwa sana. Zimebaki siku 100 kuelekea Kombe la Dunia na Mbappe hana muda wa kupoteza. Anahitaji siku zote 100 ili apone kabisa,” kilisema chanzo kimoja kilichozungumza na Meana.