Tanzania, Kenya mzigoni Cecafa nusu fainali leo
Muktasari:
- Wenyeji Tanzania watavaana na Sudan Kusini katika mechi inayotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa huku mashabiki wa nyumbani wakitarajia kuona timu yao ikisonga mbele hadi hatua ya mwisho ya mashindano hayo.
BAADA ya wiki moja ya ushindani mkali katika michuano ya Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) kwa wasichana chini ya miaka 17 inayoendelea jijini Dar es Salaam, macho yote sasa yataelekezwa Uwanja wa KMC Complex ambako nusu fainali mbili zitachezwa leo kuamua timu zitakazofuzu kucheza fainali.
Wenyeji Tanzania watavaana na Sudan Kusini katika mechi inayotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa huku mashabiki wa nyumbani wakitarajia kuona timu yao ikisonga mbele hadi hatua ya mwisho ya mashindano hayo.
Tanzania imeingia nusu fainali ikiwa na rekodi nzuri baada ya kumaliza kileleni mwa Kundi A kwa pointi saba. Timu hiyo imefunga mabao 15 na kuruhusu bao moja pekee, ikionyesha makali makubwa katika safu ya ushambuliaji pamoja na uimara wa safu ya ulinzi.
Takwimu hizo zinaifanya Tanzania kuwa miongoni mwa timu zinazotajwa kuwania ubingwa.
Hata hivyo, Sudan Kusini haitakuwa mpinzani wa kubezwa. Timu hiyo imefuzu kama mshindi wa pili wa Kundi B ikiwa na pointi sita na imeonyesha uwezo wa kupambana hadi dakika za mwisho pamoja na kupata matokeo muhimu katika mechi ngumu.
Katika nusu fainali ya pili, Uganda itakutana na Kenya katika pambano linalotajwa na wengi kuwa “fainali kabla ya fainali” kutokana na kiwango bora kilichoonyeshwa na timu zote mbili tangu kuanza kwa mashindano.
Uganda ndiyo timu iliyovutia zaidi hadi sasa baada ya kushinda mechi zake zote tatu za hatua ya makundi, kufunga mabao 20 na kutoruhusu bao hata moja. Rekodi hiyo inaifanya Teen Cranes kuingia nusu fainali kama miongoni mwa timu zenye nafasi kubwa ya kutwaa taji la mwaka huu.
Kwa upande wa Kenya, timu hiyo pia imeonyesha kiwango kizuri kwa kumaliza Kundi A ikiwa na pointi saba, sawa na Tanzania. Kikosi hicho kina safu ya ushambuliaji yenye uwezo mkubwa wa kutengeneza nafasi na kuzitumia ipasavyo mbele ya lango.
Kwa mujibu wa ratiba ya waandaaji, mechi zote mbili za nusu fainali zitachezwa katika Uwanja wa KMC Complex, huku washindi wakijihakikishia nafasi ya kucheza fainali ya michuano hiyo ya wanawake chini ya miaka 17.
Tanzania itakuwa ikitafuta kutumia faida ya kucheza nyumbani, Uganda ikisaka kuendeleza ubabe wake, huku Kenya na Sudan Kusini zikitarajia kuandika historia mpya kwa kufuzu hatua ya mwisho.
Michuano ya Cecafa U-17 Wanawake 2026 ilianza ikiwa na timu nane ambazo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Sudan Kusini, Zanzibar, Djibouti, Somalia na Sudan. Hata hivyo, safari sasa imebaki kwa timu nne pekee zinazowania nafasi ya kutwaa ubingwa wa Cecafa U-17 mwaka 2026.