Prime
Straika awagawa mabosi Yanga
WAKATI mabosi wa Yanga wakianza kupanga sura ya kikosi cha msimu ujao, mshambuliaji wa kikosi hicho Laurindo Dilson Maria Aurélio 'Depu' ameibua mjadala mzito ndani ya klabu hiyo huku kukiwa na makundi mawili tofauti kuhusu mustakabali wake.
Depu alitua Jangwani kipindi cha usajili wa dirisha dogo Januari 2026 na kupewa mkataba wa miaka miwili, akitokea Radomiak Radom ya Poland ambapo mpaka sasa amefunga mabao sita na kutoa asisti mbili.
Ujio wake alionekana kama 'mwarobaini' na tiba ya kweli ya kuziba pengo la Fiston Mayele lililowasumbua Wananchi kwa muda mrefu.
Alianza kwa moto mkali, akitupia mabao mfululizo kwenye Ligi Kuu Bara. Hata hivyo, licha ya uwezo mkubwa wa kufunga, bado kuna vitu vinavyoonekana kumzuia straika huyo asifikie kilele cha hatari yake. Mpaka sasa ameshafunga mabao sita kwenye Ligi Kuu Bara.
Unaweza kusema Depu hakuwa na mwendelezo mzuri kwani ndani ya muda mfupi alikumbana na dhoruba kubwa ya majeraha iliyomrudisha nyuma wakati ambao alikuwa ameanza kuzoea kasi ya Ligi Kuu na kutengeneza kombinesheni nzuri na viungo kama Allan Okello.
Kuumia kwake kulikata ule mfululizo mzuri wa fomu yake kwani alikosa mechi tano mfululizo za ligi jambo lililompa kazi ya kuanza upya kujitafuta mara baada ya kupona na kurejea kikosini.
UPEPO UMEGEUKA
Baada ya rekodi zake kutowaridhisha baadhi ya viongozi wa Yanga zilianza hesabu za kusaka mshambuliaji mwingine kutoka nje ambaye mmoja wapo anayefahamika mpaka sasa ni Junior Koutiama anayeichezea Kenya Police FC.
Taarifa za ndani zilieleza kuwa, kuna kundi la viongozi wanaoliona eneo la ushambuliaji likihitaji maboresho zaidi, hivyo wanaamini muda umefika wa kuachana na straika huyo ili kupisha jina lingine lenye uwezo mkubwa wa kuongeza ushindani.
Hata hivyo, upande mwingine ndani ya klabu unaonekana kutokuwa tayari kufanya uamuzi wa haraka wakitaka kwanza kusubiri mwelekeo wa benchi jipya la ufundi kabla ya kufunga mjadala wa Depu.
Hoja kubwa inayotolewa ni kwamba huenda kocha mpya akahitaji aina yake ya uchezaji na akaweza kupata kile ambacho hakikuonekana chini ya mazingira yaliyopita.
“Wapo wanaosema aachwe kwa sababu bado hajafikia matarajio yaliyokuwepo wakati anasajiliwa, lakini wapo wanaotaka apewe nafasi kwanza kwa kuwa kocha mpya anaweza kumtumia tofauti na ilivyokuwa kabla,” kilisema chanzo hicho.
Kundi linalomtetea Depu pia linaangalia upande wa rekodi likiamini bado hajapata muda mkubwa wa kucheza lakini ameonyesha ishara za kuwa mchezaji anayeweza kutoa matokeo. Katika moja ya mechi muhimu za Ligi Kuu, bao lake dhidi ya Tanzania Prisons liliipa Yanga ushindi wa 1-0 huku likiwa bao lake la sita kwenye kampeni ya ligi kipindi hicho.
Kwa mujibu wa takwimu za msimu wake ndani ya Yanga, Depu amekuwa miongoni mwa washambuliaji waliochangia mabao licha ya kutokuwa na dakika nyingi za kucheza katika baadhi ya vipindi vya msimu.
Lakini kwa wanaotaka aondoke, wanaamini Yanga haiwezi kuingia msimu mpya kwa majaribio tena hasa ikizingatiwa malengo ya ndani na mashindano ya kimataifa.
“Wanaotaka aondoke wanasema kama kuna nafasi ya kupata mshambuliaji mwenye ubora mkubwa zaidi basi ifanyike sasa, si kusubiri baadaye, kwani hawataki kujaribu bahati tena msimu ujao,” kilieleza chanzo hicho.
Katika mechi 26 ambazo Yanga imecheza mshambuliaji huyo amecheza 12 sawa na dakika 512, huku anayecheza naye eneo moja, Prince Dube akifunga mabao 9, huku akikosa mechi nne za ligi tangu msimu uanze.
MSIKIE KOCHA
Aliyewahi kuzungumzia maendeleo ya mshambuliaji huyo kocha wa muda wa Yanga, Abdihamid Moalin alisema bado wana imani na mshambuliaji huyo hata baada ya kupata majeraha bado anajitafuta kurudi kuanza kufunga.
"Hakuna tatizo kwa Depu kwa sasa, unafahamu kwamba alipata majeraha akalazimika kuwa nje kwa muda mfupi, ameimarika ndio maana ameanza kucheza taratibu,” alisema Moalin.
"Kila mchezaji hapa ana umuhimu, bahati mbaya kwake (Depu) baada ya kupata majeraha sasa anaanza kutafuta kurudi kwenye kiwango chake, kabla ya kuumia unakumbuka alionyesha kitu kizuri amefunga mabao ya kutosha."