Mbappe apiga mbili, PSG ikiitwanga Bayern

Thursday April 08 2021
mbape pc

MUNICH, UJERUMANI. MSHAMBULIAJI wa PSG,  Kylian Mbappe ameibuka shujaa usiku wa jana, Jumatano kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya  dhidi ya  Bayern Munichi.

Mbappe ambaye aliipachikia PSG  mabao mawili kwenye mchezo huo, mchango wake uliifanya  miamba hiyo ya soka la Ufaransa kuibuka na ushindi wa mabao 3-2 wakiwa ugenini huko Ujerumani  kwenye uwanja wa Allianz Arena.

Mfaransa huyo, alianza kutupia dakika ya tatu tu  ya mchezo huo baada ya kumalizia pasi ya Neymar aliyekuwa kwenye msitu wa mabeki wa Bayern Munich, PSG ilifanya shambulizi la kustukiza ambalo liliwafanya kupata uongozi wa mabao la mapema.

Licha ya Mbappe ambaye alitupia mabao mawili, Neymar naye alionekana kuwa kwenye kiwango kizuri, dakika ya 28, alifanya maajabu yake kwa kupiga pasi ya mbali iliuyonaswa na Marquinhos kisha kuifungia PSG bao la pili.

Bayern Munich walipambana na kurejea mchezo dakika ya 37 baada ya kupata bao la kwanza la kusawazisha, lililofungwa kwa kichwa na Mcameroon, Choupo-Moting. Mchezo huo ulienda mapumziko PSG wakiwa mbele kwa mabao 2-1.

Dakika ya 60 ya mchezo huo, Bayern Munich walisawazisha bao la pili kupitia kwa Thomas Muller, wakati wakiwa kwenye harakati za kusaka bao la ushindi ndipo PSG walipotumia nafasi hiyo kuwaadhibu wenyeji wao kupitia Mbappe.

Advertisement

Mabao mawili ambayo Mbappe alitupia jana, yamemfanya kufikisha jumla ya mabao manane msimu huu kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Advertisement