Mbappe akabidhiwa chumba maalumu

Muktasari:

  • Winga huyo wa zamani wa Paris-Saint Germain amepewa chumba maalumu kabisa chenye hadhi kubwa chenye kibaraza kinachoangalia kwenye viwanja vya mazoezi vya Real Madrid, huku eneo hilo likijengwa kwa zaidi ya Pauni 100 milioni.

MADRID, HISPANIA: KYLIAN Mbappe ameduwazwa baada ya kukabidhiwa chumba maalumu chenye hadhi kubwa huko kwenye uwanja wa mazoezi wa Real Madrid, ambacho atakitumia kwa ajili ya kupumzika na shughuli nyingine.

Winga huyo wa zamani wa Paris-Saint Germain amepewa chumba maalumu kabisa chenye hadhi kubwa chenye kibaraza kinachoangalia kwenye viwanja vya mazoezi vya Real Madrid, huku eneo hilo likijengwa kwa zaidi ya Pauni 100 milioni.

Mbappe, 25, alijiunga na Los Blancos kwa uhamisho wa bure, lakini pesa aliyolipwa kwa ajili ya usajili, imeweka rekodi ya kuwa mchezaji wa bure aliyelipwa ada kubwa zaidi ya usajili kwenye historia ya mchezo wa soka.

Na sasa akiwa bado hajaanza kuvaa jezi za Real Madrid na kuitumikia timu hiyo, ameduwazwa na chumba chake binafsi alichokabidhiwa huko kwenye eneo la mazoezi, ambapo kumejengwa hoteli yenye hadhi ya nyota tano.

Real Madrid imekuwa na kawaida ya kugawa chumba vyenye hadhi ya juu kwa mastaa wake katika eneo hilo la mazoezi, ambapo kila mchezaji anakuwa kwenye chumba chake binafsi, ambapo hata milango inafunguka kwa alama za vidole za mchezaji husika.

Ndani ya jumba hilo linalofanana na hoteli ya nyota tano kuna mabwawa ya kuogelea, vyumba vya michezo ya kompyuta, sinema na vyumba vingine 57 huku jengo hilo likijengwa kwenye eneo linalozidi mita za mraba 7,800. Mbappe anakaa kwenye chumba chenye namba 103.

Eneo hilo la mazoezi la Valdebebas Park lilifunguliwa mwaka 2005 na linaripotiwa kugharimu Pauni 100 milioni.

Mbappe aliripotiwa kuchukua chumba ambacho awali alikuwa akikaa kiungo Toni Kroos.

Kiungo Mjerumani, Kroos, 34, aliondoka kwenye timu hiyo mwishoni mwa msimu huu, akitangaza kustaafu soka.