Mbappe aacha msala Ligue 1

Muktasari:

  • Ligi Kuu Ufaransa imepoteza jina la staa mkubwa kabisa kwenye soka wiki iliyopita baada ya Mbappe kuthibitisha kujiunga na Real Madrid.

PARIS, UFARANSA: KIMENUKA. Ligue 1 inahaha kutafuta mtangazaji mpya kwa ajili ya msimu ujao, mambo yakiwa magumu kutokana na Kylian Mbappe kuondoka.

Ligi Kuu Ufaransa imepoteza jina la staa mkubwa kabisa kwenye soka wiki iliyopita baada ya Mbappe kuthibitisha kujiunga na Real Madrid.

Jambo hilo limezua kizaazaa kwenye ishu ya kupata mtangazaji wa ligi hiyo ya Ufaransa kutokana na televisheni nyingi kugoma, hakuna mvuto.

Kwa mujibu wa Sport Business, mpango mbadala unaandaliwa ambapo mabosi wa Ligue 1 wanatazama uwezekano wa kutengeneza chaneli yao wenyewe ya ligi hiyo ambayo itakuwa na majukumu ya kurusha matangazo ya mechi za ligi hiyo kama hakutakuwa na mtangazaji aliyepatikana.

Chaneli hiyo itakuwa ikitoa huduma zake za kuhusu ligi hiyo kwa kulipia.

Suluhisho la haraka linahitajika kwa ajili ya kuitangaza ligi hiyo hasa kwa timu zilizorejea kwenye Ligue 1, Auxerre, Angers na Saint-Etienne.

Ripoti ya RMC Sport, timu hizo tatu hazina pesa za kufanya usajili wa mastaa wapya, kutokana na mdhamini wa Ligue 1 kwa upande wa haki ya kurusha matangazo, ambaye angelipa pesa timu shiriki, kushindwa kupatikana.

Kwenye Ligue 1 kwa sasa hakuna mtangazaji mwenye haki ya kurusha ligi hiyo, hivyo timu zinashindwa kuwa na pesa ya kufanya usajili, hasa kwa timu ambazo zimepanda daraja, zinahitaji kupata sapoti hiyo ya pesa ili kuingia sokoni kujenga vikosi vyao.

Mbappe limekuwa jina la staa mkubwa kwenye Ligue 1 kuondoka kwa miaka ya karibuni, huku jambo hilo likidaiwa kusababisha kuzorota kwa ligi hiyo, ambayo inatajwa kama moja ya Ligi Kuu tano bora za Ulaya.

Mastaa wengine wenye majina makubwa walioachana na ligi hiyo miaka ya hivi karibuni ni pamoja na Lionel Messi, Neymar, Aurelien Tchouameni, Victor Osimhen, Jeremy Doku, Mauro Icardi na Lucas Paqueta.

Paris Saint-Germain, ambayo ni timu ya zamani ya Mbappe, ndiyo iliyoshinda ubingwa wa Ligue 1 msimu uliopita, ilimaliza ligi pointi tisa juu ya timu iliyoshika nafasi ya pili, AS Monaco.

PSG ilishinda mataji 10 ya ligi katika misimu 12 iliyopita, huku miaka ambayo ilikosa, timu zilizobeba taji hilo ni AS Monaco 2017 na Lille 2021.

Lakini, PSG bado haijaonja utamu wa kubeba taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya, ambapo hatua za juu kabisa kwenye michuano hiyo iliwahi kufika fainali mwaka 2020, ambapo ilichapwa na Bayern Munich 1-0.

Msimu uliomalizika hivi karibuni, ilikubali kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa Borussia Dortmund katika mechi za mikondo miwili katika hatua ya nusu fainali, ambapo hiyo ilikuwa mchezo wa mwisho wa michuano ya Ulaya kwa Mbappe kuitumikia miamba hiyo ya Parc des Princes.

Mbappe ameondoka PSG akiwa kinara wa mabao wa muda wote, akifunga mabao 256 katika mechi 308.