Mbadala wa Xabi Alonso kapatikana Real Madrid
Muktasari:
- Arbeloa alikuwa beki wa kulia wakati wa uchezaji wake na aliwahi kucheza kikosi kimoja na Alonso klabuni Liverpool, Real Madrid na timu ya taifa ya Hispania.
MADRID, HISPANIA: REAL Madrid imeanza tayari mchakato wa kutafuta kocha mpya ambaye atachukua mikoba ya Xabi Alonso endapo timu hiyo itaendelea kupata matokeo mabovu.
Alonso aliteuliwa kuwa kocha mkuu wa Real Madrid katika dirisha lililopita la majira ya kiangazi, baada ya kufanya vizuri akiwa na Bayer Leverkusen ya Ujerumani aliyoiwezesha kushinda ubingwa wake wa kwanza wa Bundesliga.
Kocha huyu ambaye aliwahi kuwa mchezaji wa Real Madrid, aliyejiunga na klabu hiyo mwaka 2009 kutoka Liverpool kwa ada ya uhamisho ya Pauni 30 milioni, na baadaye akashinda taji la La Liga na Ligi ya Mabingwa Ulaya, mambo hayaonekani kuwa mazuri kwake kwa sasa, huku baadhi ya ripoti zikidai kwamba kuna mpasuko katika timu.
Kwa sasa katika La Liga, Madrid inashikilia nafasi ya pili kwenye msimamo, nyuma ya vinara Barcelona.
Katika Ligi ya Mabingwa, Madrid inashika nafasi ya saba kwenye msimamo wa jumla wa timu zote zinazoshiriki baada ya mechi sita.
Alonso yupo chini ya shinikizo la kufukuzwa Santiago Bernabeu, ambalo limezidi baada ya kipigo cha 2-1 nyumbani dhidi ya Manchester City kwenye Ligi ya Mabingwa.
Jarida la habari la Cadena Ser linaripoti kuwa Alvaro Arbeloa, ambaye kwa sasa anasimamia timu ya vijana ya Real Madrid, anaweza kuwa kocha wa Real Madrid Alonso akiondolewa.
Alipohojiwa kuhusu uwezekano huo kabla ya mechi ya Alaves ugenini Jumapili jioni, Alonso amesema: “Kwa siku zijazo, sina shaka anaweza kuwa kocha wa timu hii, lakini kuhusu swali la endapo atachukua nafasi yangu, bado hatujazungumzia hilo.”
Jarida hilo pia linadai kuwa uongozi wa Madrid utamwondoa Alonso na kumpa Arbeloa nafasi ya kocha wa mpito ikiwa matokeo ya wikiendi iliyopita hayatawaridhisha.
Arbeloa alikuwa beki wa kulia wakati wa uchezaji wake na aliwahi kucheza kikosi kimoja na Alonso klabuni Liverpool, Real Madrid na timu ya taifa ya Hispania.