Perez anavyoitazama saa yake na kumtazama Alonso usoni
Muktasari:
- Lengo lake kubwa litakuwa kuja kumtazama usoni, Xabi Alonso, huku pia akiitazama saa yake ya kifahari aina ya Rolex yenye thamani ya Pauni 120,000. Perez atakuwa akitazama jinsi mshale wa saa unavyosogea na muda unavyoitupa mkono timu yake chini ya Alonso.
VALDEBEBAS karibu na Uwanja wa Ndege wa Madrid Barajas ndipo viwanja vya mazoezi vya Real Madrid vilipo. Florentino Perez ana ofisi yake ndogo katika viwanja hivyo na huwa anakuja mara chache. Natabiri siku chache zijazo anaweza kuja katika ofisi hiyo.
Lengo lake kubwa litakuwa kuja kumtazama usoni, Xabi Alonso, huku pia akiitazama saa yake ya kifahari aina ya Rolex yenye thamani ya Pauni 120,000. Perez atakuwa akitazama jinsi mshale wa saa unavyosogea na muda unavyoitupa mkono timu yake chini ya Alonso.
Alonso ameanza kupokea vipigo juu ya vipigo pamoja na sare za kijinga. Iwe katika La Liga au Ligi ya Mabingwa wa Ulaya amekuwa akipokea kichapo baada ya kichapo. Alichapwa na Liverpool kisha akaenda La Liga akatoa suluhu ya bila kufungana na Rayo Vallecano.
Akaenda kucheza na Elche iliyo pungufu, lakini pambano likaishia kwa sare ya 2-2. Akaenda ugenini kucheza na Olympiacos akashinda 3-4 na nusura pambano liishe kwa sare. Akarudi La Liga akatoka sare ya 1-1 na Girona. Akarudi La Liga akapumua kwa kushinda 0-3 dhidi ya Atheltic Bilbao ugenini.
Mechi iliyofuata Madrid akachapwa nyumbani 0-2 na Celta Vigo na mechi nyingine iliyofuata akachapwa na Man City katika Ligi ya Mabingwa Jumatano usiku. Mwendo huu wa kinyonga sio aina ya maisha ambayo Perez aliyatarajia kutoka kwa Alonso.
Majuzi nilikuwa namsikia sehemu akisema kwamba amewekeza kiasi cha Euro 1.347 bilioni kwa ajili ya kuufanyia matengenezo Uwanja wa Santiago Bernabeu ambao kwa sasa umekuwa wa kisasa zaidi. Lazima atakuwa amechukua mkopo benki. Namna gani atarudisha pesa hizo? Ni kwa Madrid kupata mafanikio ndani na nje ya uwanja.
Ndani ni zaidi. Timu ishinde ili mashabiki waendelee kufurika uwanjani kuwashangilia kina Vinicius Junior, Kylian Mbappe, Jude Bellingham na mastaa wengine aliowakusanya katika muundo ule ule wa Galacticoz. Lakini anataka kuuza jezi zao kwa wingi.
Anataka kuchukua La Liga na ubingwa wa Ulaya kwa ajili kutengeneza pesa zaidi, huku akiongeza pesa kwa watu wanaiodhamini Real Madrid. Haya yote hayatawezekana kama Madrid wataendelea na mwendo huu wa kinyonga wa kutoka sare na Girona nyumbani.
Haya yote hayatawezekana kama ataendelea kutawaliwa na timu za England katika michuano ya Ligi ya Mabingwa kama inavyotokea. Msimu uliopita bila ya Carlo Ancelotti alitiwa aibu ya kuchapwa ugenini na nyumbani na Arsenal. Alonso aliletwa kwa ajili ya kukabiliana na aibu huu.
Hata hivyo, msimu huu bado inaonekana hakuna kinachobadilika kutoka kwa timu za England. Vichapo vimeendelea huku Mbappe na Vinicius Junior wakiwa uwanjani. Fikiria, eti dhidi ya Liverpool ambayo inasuasua katika Ligi Kuu ya England.
Naamini falsafa za Alonso. Naamini yeye ni mkumbo ule ule wa kina Mikel Arteta, Cesc Fabregas, Vincent Kompany na Luis Enrique Martinez. Watu wanaojaribu kucheza mpira wa Pep Guardiola. wanahitaji muda kuziweka akili za wachezaji sawa na wafuate kile ambacho kocha anataka.
Mpira wa pasi nyingi, mpira wa kukaba kwa pamoja kutoka juu na katika kila maeneo ya uwanja. Mpira ambao hautaki uvivu wa wachezaji na unahitaji nidhamu ya hali ya juu. Tayari alishaonyesha hivyo akiwa na Bayer Leverkusen na akachukua ubingwa wa Bundesliga kwa mara ya kwanza katika historia ya klabu hiyo.
Nadhani hilo ndilo ambalo lilimvutia Perez. Timu kama Real Madrid inatazamiwa kucheza kama ambavyo Manchester City au Arsenal zinavyocheza. Inatamani kucheza kama Como ya Italia inavyocheza. Inatamani kucheza kama Bayern Munich inavyocheza.
Chini ya Ancelotti walikuwa wametegemea zaidi uwezo wa mchezaji mmoja mmoja. Labda Perez alitaka mpira wa uhakika wa kitabuni ambao utaitofautisha timu kubwa kama Real Madrid dhidi ya timu ndogo kama Girona.
Hata hivyo, hadi sasa Alonso ameshindwa kupeleka mpira huo Madrid. Binafsi sioni tatizo kwa sababu nimeshuhudia kina Arteta wakichukua muda kubadili mambo. Hata hivyo, hilo la kusubiri muda halipo kwa Perez.
Endapo matokeo yakiendelea kuwa mabovu halafu pengo la Madrid na Barcelona iliyo kileleni likaendelea kuwa juu basi Perez ataiangalia saa yake kwa makini kuona kama ana muda wa kusubiri. Endapo hili litatokea huku Madrid pia wakitolewa katika michuano ya Ulaya katika hatua ya mtoano au robo fainali sioni kama Perez ni mvumilivu wa kiasi hiki.
Majuzi tu kulikuwa na kikao ambacho kilijadili hatma ya Alonso na imeamuriwa aendelee kupewa muda. Usiamini sana walichomwambia Alonso kwa sababu Perez sio aina ya matajiri wavumilivu. Anachojua ni kwamba timu yake inahitaji matokeo mazuri sasa. Wazungu wanasema ‘Big Results Now’.
Perez ananikumbusha Roman Abramovich. Huwa hawajui kitu kinachoitwa mipango ya muda mrefu katika timu. Wanachojua ni kuweka pesa ndefu kwa wachezaji na kusubiri matokeo. Basi. Kinyume cha hapo kocha unaonyeshwa mlango wa kutokea.
Sijui kwanini Alonso bado anachelewa, lakini nadhani kuna ugumu pia wa mifumo hii kueleweka unapokuwa na wachezaji wakubwa. Ndio maana tuliona kiburi cha Vinicius alipombwatukia Alonso wakati alipotolewa uwanjani kipindi cha pili katika pambano dhidi ya Barcelona.
Anahitajika kocha mwenye maamuzi magumu kuweka mambo sawa pindi unaposimamia wachezaji wenye majina makubwa na pesa. Pale Bayer Leverkusen ilikuwa rahisi kwa Alonso kwa sababu wachezaji hawakuwa na majina makubwa na wengi aliwapita mafanikio wakati akiwa kama mchezaji.
Tusubiri na kuona, lakini Alonso analazimika kurekebisha mambo kwa haraka. Yupo katika timu ambayo unapaswa kuijenga huku ukipata mafanikio hapo hapo. sio timu ambayo inaweza kukusubiri endapo itaambulia patupu.