Mawakala wa wanasoka walivyozipiga hesabu klabu za England

LONDON, ENGLAND


UMEKUWA mwaka mwingine mzuri kwa mawakala wa wachezaji kwenye soka kwa kuweka kibindoni karibu Pauni 300 milioni kutokana na dili mbalimbali za kuwauzia wachezaji klabu za soka.

Chama cha soka cha England kimefichua ripoti ya pesa zilizotumika na klabu kulipa mawakala kwa wachezaji iliowanasa katika msimu huu.

Ripoti hiyo ilifichua klabu kutoka Ligi Kuu nne kubwa zimetoa Pauni 317.1 milioni kuwalipa mawakala kwa msimu huu wa 2020/21. Hata hivyo, kiwango hicho kimeshuka kwa Pauni 600,000 kulinganisha na mkwanja waliokunja mawakala msimu uliopita, huku janga la virusi vya corona likidaiwa kutibua hesabu za msimu huu.

Kwenye Ligi Kuu England, Chelsea ndiyo iliyolipa pesa nyingi zaidi ada za mawakala, wakati jambo hilo halikuziacha timu nyinne kama Southampton (Pauni 6,804,154), Crystal Palace (Pauni 6,760,093), Burnley (Pauni 4,458,520) na West Brom (Pauni 4,222,059) zikiwa zimelipa pesa nyingi kulipia gharama za mawakala.

Wakati mashabiki wa soka wakisubiri kwa hamu dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi, hizi hapa timu za Ligi Kuu England zilizolipa mkwanja mrefu kulipia ada za mawakala wa wachezaji kwa msimu huu wa 2020-21, huku Jorge Mendes na Mino Raiola wakiripotiwa kutesa kisawasawa.


Chelsea -

Pauni 35.2 milioni

Haishangazi kuona Chelsea inashika namba moja kwenye orodha ya timu zilizolipa ada kubwa kuwalipa mawakala wa wachezaji.

Chelsea ndiyo timu iliyotumia pesa nyingi kwenye usajili wa dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi, wakati ilipotumia Pauni 220 milioni.

Kwenye dili hizo ilimnasa Kai Havertz kwa ada ya Pauni 72 milioni kutoka Bayer Leverkusen, Timo Werner kutoka RB Leipzig kwa ada ya Pauni 47.5 milioni na Ben Chilwell kutoka Leicester City kwa ada ya Pauni 45 milioni.

Hakim Ziyech na Edouard Mendy nao walitua Stamford Bridge kwa pesa kubwa huku chama hilo kwa sasa likiwa chini ya kocha Mjerumani, Thomas Tuchel.

Kwenye dili zake zote, Chelsea imetumia Pauni 35.2 milioni kulipa ada za mawakala wa wachezaji hao.


Man City- Pauni 30.2 milioni

Manchester City haikufanya usajili wa mastaa wengi kuimarisha kikosi chao kwenye majira ya kiangazi ya mwaka jana. Kikosi hicho kinachonolewa na Mhispaniola, Pep Guardiola kiliwanasa beki wa kati Ruben Dias, ambaye ni usajili wa rekodi kwenye klabu hiyo wakati aliponyakuliwa kwa Pauni 61 milioni kutoka Benfica. Beki huyo wakala wake ni Jorge Mendes.

Miamba hiyo ya Etihad ilimnasa pia beki wa kati Nathan Ake kutoka Bournemouth kwa ada ya Pauni 41 milioni na straika Ferran Torres kwa ada ya Pauni 20 milioni huku usajili wao wote ukigharimu Pauni 160 milioni.

Hata hivyo, kwenye dili hizo, Man City imejikuta ikitumia pesa nyingi kulipa mawakala wa wachezaji hao, ambapo Pauni 30.2 milioni zimetumika kwenye dili hizo kulipa tu kamisheni za mawakala hao.


Man United -

Pauni 29.8 milioni

Ni kitu kinachoshangaza kuona Manchester United ni moja ya timu iliyopigwa pesa nyingi na mawakala kwenye dili za usajili wa mastaa msimu huu.

Kwenye dirisha la uhamisho wa majira ya kiangazi la mwaka jana, Man United ilitumia Pauni 35 milioni kunasa huduma ya kiungo wa Uholanzi, Donny van de Beek kutoka Ajax ukiwa ni uhamisho wao mkubwa waliofanya kwenye dirisha hilo la majira ya kiangazi.

Bosi anayefanya usajili, Ed Woodward alitoa pia Pauni 19 milioni kunasa saini ya winga kinda Amad na beki wa pembeni Alex Telles kutoka FC Porto kwa ada ya Pauni 13.5 milioni, huku Jorge Mendes ikiaminika kwamba alimsaidia wakala mwenzake Pinhas Zahavi kukamilisha dili hilo la Telles.

Katika msimu, Man United ilimwongeza mkataba kiungo Paul Pogba na Jesse Lingard kitu ambacho mawakala wa wachezaji hao, hasa Mino Raiola anayemsimamia Pogba kuweka mkwanja mfukoni. Kwenye dili zote hizo, Man United imetumia Pauni 29.8 milioni kulipa mawakala.


Liverpool -Pauni 21.7 milioni

Liverpool ilifanya usajili wa kiungo wa kati Thiago kutoka Bayern Munich na straika Diogo Jota kutoka Wolves, ambaye ni mchezaji wa Mendes.

Staa Thiago ametua kwenye kikosi hicho cha Anfield kwa ada ya Pauni 20 milioni, wakati Jota saini yake imenaswa kwa Pauni 40 milioni, huku mchezaji mwingine waliyemnasa kwenye dirisha hilo la uhamisho wa majira ya kiangazi, Kostas Tsimikas walilipa Pauni 11.7 milioni.

Baada ya kuandamwa na majeruhi mengi kwenye safu yake ya ulinzi, Liverpool iliingia tena sokoni kwenye dirisha la Januari kuwanasa mabeki wa kati Ben Davies na Ozan Kabak kwa mkopo ambao umewagharimu Pauni 2 milioni.

Lakini, kwenye dili zote walizofanya kwa msimu huu, kikosi hicho cha kocha Jurgen Klopp kililipa mkwanja wa Pauni 21.7 milioni kulipia ada za mawakala wa wachezaji hao.


Tottenham -

Pauni 16.5 milioni

Tottenham Hotspur ilikaribia kutumia Pauni 100 milioni kwenye dirisha la uhamisho wa majira ya kiangazi mwaka jana baada ya kufanya usajili wa mastaa wanne.

Spurs iliwasajili Giovani Lo Celso na Sergio Reguilon kwa ada ya Pauni 27 milioni, wakati wachezaji wanaosimamiwa na wakala Jorge Mendes, Matt Doherty na Pierre-Emile Hojbjerg - ambaye wakala wake ni Zahavi - walitua kwenye timu hiyo kwa ada ya Pauni 15 milioni kila mmoja.

Jose Mourinho aliboresha pia safu yake ya mabeki akimsajili Joe Rodon kutoka Swansea kwa ada ya Pauni 11 milioni, wakati Carlos Vinicius - ambaye pia yupo chini ya kampuni ya Mendes ya GestiFute alijiunga na timu hiyo kwa mkopo.

Miamba hiyo ya London imemnasa pia kwa mkopo Gareth Bale, huku staa huyo akisimamiwa na wakala Jonathan Barnett, huku dili hizo zote zikiwagharimu miamba hiyo inayonolewa na Jose Mourinho kutumia Pauni 16.5 milioni kulipia ada za mawakala.


Arsenal - Pauni 16.5 milioni

Kwenye dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi la mwaka jana, kocha Mikel Arteta aliimarisha timu yake kwenye sehemu ya kiungo kwa kumsajili Thomas Partey na beki kwa kumnasa Gabriel kwa ada za Pauni 45 milioni na Pauni 23 milioni mtawalia.

Lakini, kwenye dili hizo na nyingine ilizofanya, Arsenal imetumia pesa nyingi kulipa ada za mawakala, ikitumia Pauni 16.5 milioni. Staa mwingine iliyemsajili ni Mbrazili, Willian ambaye anasimamiwa na wakala Kia Joorabchian - ambaye anadaiwa alihitaji kulipwa ada kubwa sana.

Kwenye dirisha la Januari, Arsenal iliwafungulia mastaa kibao kuondoka akiwamo Mesut Ozil, Sokratis Papastathopoulos na Shkodran Mustafi, lakini ilimwongeza kwenye kikosi chao kiungo Martin Odegaard kwa mkopo kutoka Real Madrid.


Everton - Pauni 14.1 milioni

Kama ilivyo kwa Mikel Arteta, kocha wa Everton, Carlo Ancelotti aliweka nguvu zaidi kwenye kusajili mabeki na viungo wa kati kwenye dirisha la uhamisho wa majira ya kiangazi la mwaka jana.

Miamba hiyo ya Goodison Park ilinasa saini ya Ben Godfrey kutoka Norwich City kwa ada ya Pauni 25 milioni, Allan kutoka Napoli kwa ada ya Pauni 23 milioni na Abdoulaye Doucoure kutoka Watford kwa Pauni 20 milioni.

Kwenye dili zao, Everton pia walilipa pesa nyingi kwa mawakala, wakitumia Pauni 14.1 milioni. Nyota wengine iliyowanasa ni James Rodriguez, anayesimamiwa na wakala Jorge Mendes na staa mwingine ni Robin Olsen huku kwenye dirisha la Januari ilinasa saini ya Joshua King.


Wolves

Pauni 12.6 milioni

Kwenye namba nane, wapo vijana wa Nuno Espirito Santo, Wolverhampton Wanderers. Kwenye dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi, miamba hiyo ya Molineux ilivunja rekodi yake ya usajili wakati ilipomnasa mshambuliaji Fabio Silva kutoka FC Porto kwa mkwanja wa Pauni 36 milioni.

Wolves pia ililipa Pauni 27 milioni kupata huduma ya Nelson Semedo kutoka Barcelona na ilimnasa kwa mkopo Vitinha kutoka Porto.

Kama hufahamu wachezaji wote hao watatu wanasimamiwa na wakala mmoja, Jorge Mendes, ambaye anatajwa kuwa mshauri wa mmiliki wa klabu ya Wolves.

Wolves ilimsajili pia Ki-Jana Hoever kutoka Liverpool kwa Pauni 9 milioni, huku kwenye dili zao zote wakilipa ada za mawakala Pauni 12.6 milioni.