Mastraika wanne ubaoni Man United

Muktasari:
- Man United imekuwa na wakati mgumu kwenye fowadi yao msimu huu, ikifunga mabao 37 tu katika mechi 29 ilkizocheza kwenye Ligi Kuu England, huku ikiishia kushika nafasi ya 13 kwenye msimamo wa ligi hiyo.
LONDON, ENGLAND: MANCHESTER United imeweka ubaoni majina ya mastraika wanne inayohitaji huduma zao kwa ajili ya msimu ujao.
Man United imekuwa na wakati mgumu kwenye fowadi yao msimu huu, ikifunga mabao 37 tu katika mechi 29 ilkizocheza kwenye Ligi Kuu England, huku ikiishia kushika nafasi ya 13 kwenye msimamo wa ligi hiyo.

Man United ilishinda dhidi ya Leicester City wikiendi iliyopita, ambapo ilimshuhudia straika Rasmus Hojlund akimaliza ukame wake wa kucheza mechi 21 bila ya kufunga baada ya kupachika nyavuni bao la kwanza kati ya matatu katika ushindi wa 3-0.
Ishu ya mshambuliaji wa kati mpya imekuwa kwenye mjadala wa klabu hiyo tangu Kocha Ruben Amorim alipowasili.
Kutokana na pesa kushindwa kupatikana dirisha la Januari, Man United iliishia tu kwenye usajili wa mabeki Patrick Dorgu na Ayden Heaven.

Licha ya klabu hiyo kukabiliwa na wakati mgumu wa kifedha, lakini kuna dhamira kubwa ya kumsapoti Amorim kwenye kuhakikisha inanasa straika mpya, huku ikifahamika wazi nafasi hiyo ni ghali.
Ripoti zinafichua Hugo Ekitike wa Eintracht Frankfurt, straika wa RB Leipzig, Benjamin Sesko na mkali anayecheza kwa mkopo Galatasaray, Victor Osimhen ni miongoni mwa wanaopigiwa hesabu sambamba na straika wa Sporting CP, Viktor Gyokeres.

Gyokeres ana nafasi kubwa kutokana na kuwahi kufanya kazi na Amorim. Kocha huyo Mreno na straika huyo wa Sweden walishinda ubingwa wa ligi huko Ureno msimu uliopita na alikuwa kiboko kwa kufunga mabao.
Fowadi huyo wa zamani wa Coventry ameendelea kuwasha moto msimu huu, akifunga mabao 40 na asisti 10 katika mechi 41, ikiwa ni wastani wa zaidi ya bao moja kwa kila mechi ya Liga.
Rais wa Sporting, Frederico Varandas ameshafichua bayana uwezekano wa mshambuliaji huyo kuondoka dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya Kiangazi.

Hata hivyo, A Bola linaripoti Gyokeres huenda mipango yake haipo kabisa Old Trafford. Fowadi huyo mwenye umri wa miaka 26 imeelezwa anavutiwa zaidi na klabu za Liverpool, Arsenal na Manchester City kwa sababu ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Mmiliki mwenza wa Man United, bilionea Sir Jim Ratcliffe anafahamu wazi kocha Amorim anahitaji sapoti kubwa ya kuletewa mastaa wa maana kutokana na waliopo kwenye kikosi hicho wengi wao kuwa ni wachezaji wa kawaida.