Mastaa wanaolipwa kibosi unaoweza kuwaona Afcon 2025
Muktasari:
- Mataifa shiriki kwa sasa yameanza mchakato wa kuita vikosi vyao vya awali kabla ya kuvichuja na kupata wale wachezaji ambao watakwenda kupeperusha bendera za nchi hizo kwenye mashindano hayo ya kusaka ubingwa wa Afrika.
RABAT, MOROCCO: MCHAKAMCHAKA wa mikikimikiki ya mashindano ya soka ya Afcon 2025 utarajiwa kuanza Desemba 21 huko Morocco, huku wengi wakisubiri kwenda kuona ni taifa gani litakaloibuka na ubingwa huo.
Mataifa shiriki kwa sasa yameanza mchakato wa kuita vikosi vyao vya awali kabla ya kuvichuja na kupata wale wachezaji ambao watakwenda kupeperusha bendera za nchi hizo kwenye mashindano hayo ya kusaka ubingwa wa Afrika.
Wakati mashabiki wakisubiri kwa hamu mastaa watakaotajwa kucheza kwenye mashindano hayo, kuna orodha hiyo ya wakali ambao ukweli watakwenda Afcon 2025 wakihesabika kama wanasoka matajiri kabisa, wakimiliki fedha za kutosha.
9. Edouard Mendy (Senegal / Al-Ahli)
Kipa wa Senegal Edouard Mendy alipata umaarufu alipojiunga na Chelsea na kuwasaidia kushinda taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2021, jambo lililomfanya ashinde tuzo ya Kipa Bora wa UEFA na Kipa Bora wa FIFA mwaka 2021.
Aliongoza pia Senegal kutwaa taji lao la kwanza la AFCON mwaka huo huo, na kufanikisha kuwa kipa wa kwanza kushinda taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya na Ligi ya Mabingwa wa Asia (2025).
Mendy pia alishinda Kombe la Dunia la Klabu la FIFA akiwa na Chelsea pamoja na Saudi Super Cup na Al-Ahli baada ya uhamisho wake mkubwa kwenda Saudi Arabia mwaka 2023, ambako pia alitajwa kuwa Kipa Bora wa Ligi ya Mabingwa wa Asia.
Katika klabu yake ya sasa, mchezaji huyo analipwa takribani Euro 211,538 kwa wiki sawa na Euro 11 milioni kwa mwaka.
8. Achraf Hakimi (Morocco / Paris Saint-Germain)
Nyota wa Morocco, Achraf Hakimi amekuwa mchezaji muhimu wa PSG tangu mwaka 2021 alipotoka Inter Milan.
Ni rahisi kumtaja Hakimi kama mmoja wa mabeki wa kulia bora duniani, akishika nafasi hiyo vyema kiasi cha kuisaidia timu yake kushinda taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya na UEFA Super Cup msimu wa 2024–25.
Beki huyo wa kulia alichaguliwa kuingia kwenye kikosi bora cha mashindano kutokana na kasi yake kubwa na uwezo wa kutoa krosi sahihi wakati wa safari ya kihistoria ya Morocco kufika nusu fainali ya Kombe la Dunia 2022.
Hakimi ameshinda taji la Ligue 1 kila msimu alioichezea PSG, pamoja na Coupe de France (2024–25), na Trophee des Champions. Pia anashikilia rekodi ya kutoa asisti nyingi za mabao kuliko beki yeyote katika historia.
Hakimi analipwa takribani Euro 253,846 kwa wiki, sawa na Euro 13.2 milioni kwa mwaka.
7. Franck Kessie (Ivory Coast / Al-Ahli)
Kiungo wa Ivory Coast, Franck Kessie, alijiunga na Al-Ahli ya Saudi Arabia mwaka 2023 akitokea Barcelona ya Hispania, ambako alishinda La Liga ya 2022–23.
Mchezaji huyo mwenye miaka 28 alikuwa muhimu katika ushindi wa Ivory Coast kwenye Afcon 2023, na tangu kujiunga na Al-Ahli, ameshinda taji la Ligi ya Mabingwa ya Asia msimu wa 2024–25.
Kwa mujibu wa ripoti, Franck Kessie kwa sasa anapata zaidi ya Euro 14 milioni kwa mwaka, au Euro 269,000 kwa wiki. Taarifa hizi zinatokana na mtandao wa Salary Leaks, zikionyesha malipo yake kamili Al Ahli SFC.
6. Omar Marmoush (Misri / Man City)
Akiwa amejiunga na Manchester City mapema mwaka huu akitokea Eintracht Frankfurt, Omar Marmoush ni nyota anayekua kwa kasi kwenye soka la dunia.
Alisajiliwa kwa Euro 70 milioni, kiasi kinachoonekana kustahili kutokana na mafanikio yake kwenye Bundesliga.
Mchezaji huyo alishinda tuzo ya Mchezaji Bora wa Bundesliga wa Mwezi, akaongoza ligi kwa asisti na kuchangia mabao mengi katika msimu fulani, akafunga bao muhimu dhidi ya RB Leipzig, na kupata nafasi ya kucheza Europa League 2024–25.
Katika msimu wake wa kwanza Frankfurt, alifunga mabao 16 katika mechi 37, mafanikio yaliyoongeza thamani yake na kuvutia klabu kubwa duniani. Marmoush analipwa takribani Pauni 295,000 kwa wiki, sawa na Pauni 15.3 milioni kwa mwaka katika klabu ya Manchester City kwa mujibu wa Goal.
5. Mohamed Salah (Misri / Liverpool)
Huwezi kuzungumza kuhusu soka la Afrika bila kumtaja Mohamed Salah, mchezaji wa Misri ambaye uwezo wake umemletea sifa nyingi.
Alijiunga na Liverpool mwaka 2017, ambako ametoa mchango mkubwa kwenye soka la dunia. Ameshinda ubingwa wa Ligi Kuu England, taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya, Kombe la Dunia la Klabu la FIFA, na makombe kadhaa kama FA Cup na League Cup.
Mo Salah ameshinda tuzo nyingi ikiwamo mfungaji bora wa muda wote wa Afrika katika EPL, mshindi mara nne wa Kiatu cha Dhahabu, mshindi wa tuzo nyingi za Mchezaji Bora wa Mwaka, ikiwamo ya Mchezaji Bora ya Chama cha Wanasoka (PFA), mshindi wa FIFA Puskas Award 2018 na mshindi wa Mwanasoka Bora wa Mwaka wa Afrika mara mbili. Ubora wake unamfanya alipwe Pauni 400,000 kwa wiki, sawa na Pauni 20.8 milioni kwa mwaka. Huu ndio mshahara mkubwa zaidi kwa mchezaji yeyote katika historia ya Liverpool.
4. Victor Osimhen (Nigeria / Galatasaray)
Straika wa Nigeria, Victor Osimhen alijitokeza kwenye anga la soka alipoibuka kwenye Kombe la Dunia la FIFA U-17 mwaka 2015 na kushinda tuzo ya Mfungaji Bora.
Baadaye alijiunga na Napoli mwaka 2020 na kuisaidia kushinda taji la Serie A kwa mara ya kwanza baada ya miaka 33 msimu wa 2022–23, na kushinda Kiatu cha Dhahabu cha Mfungaji Bora wa Ligi Kuu ya Italia (Serie A, 2022–23), pamoja na Mchezaji Bora Mwaka wa Ligi Kuu ya Serie A (2023). Alishinda pia tuzo ya Mwanasoka Bora wa Afrika mwaka 2023.
Baada ya kipindi cha mkopo Galatasaray ambako alimaliza kama mfungaji bora wa ligi kwa mabao 35 katika mechi 39, Osimhen alisaini mkataba wa kudumu wa miaka minne wenye thamani ya Euro 75 milioni.
Osimhen ana rekodi ya kuwa mmoja wa wachezaji wanaolipwa zaidi katika historia ya soka la Uturuki, akipata Euro 21 milioni kwa mwaka, sawa na Euro 404,000 kwa wiki. Hii ni pamoja na mshahara wa msingi wa Euro 15 milioni, bonasi ya uaminifu ya Euro 1 milioni kwa mwaka, na Euro 5 milioni za haki za kutumiwa kwa picha zake.
3. Kalidou Koulibaly (Senegal / Al Hilal)
Beki kisiki, Kalidou Koulibaly ni beki wa kati mwenye nguvu kubwa na nahodha wa Senegal. Aliiongoza nchi yake kushinda AFCON 2022.
Alichaguliwa kuwa Beki Bora wa Serie A mwaka 2019 alipokuwa Napoli na akashinda Coppa Italia mwaka 2020.
Mchezaji huyo aliingia pia kwenye Kikosi Bora cha Serie A mara nne na alishinda tuzo ya Golden Lion kama mchezaji bora wa Senegal.
Kutoka Napoli, alijiunga na Chelsea mwaka 2022 kwa muda mfupi kabla ya kuhamia Al Hilal kwa takribani Pauni 17 milioni. Ameshinda Saudi Pro League na Saudi Super Cup tangu kuwasili.
Koulibaly analipwa Euro 667,308 kwa wiki, sawa na Euro 34.7 milioni kwa mwaka, katika msimu wa 2025–26.
2. Sadio Mane (Senegal / Al-Nassr)
Sadio Mane ameacha alama kubwa kwenye historia ya soka, na haishangazi kuona jina lake kwenye orodha hii.
Alianza kung’ara akiwa Liverpool, ambako alishinda Ligi ya Mabingwa Ulaya na Ligi Kuu England. Alishinda pia Kiatu cha Dhahabu cha Ligi Kuu England 2018–19 na tuzo ya Socrates Award 2022 kutokana na kazi zake za kibinadamu.
Baadaye alijiunga na Bayern Munich na kushinda Bundesliga. Kisha alihamia Al-Nassr ya Saudi Arabia kwa Euro 30 milioni. Mane aliiongoza Senegal kushinda AFCON 2022 na ameshinda tuzo ya Mchezaji Bora wa Afrika mara mbili.
Mane analipwa Euro 769,231 kwa wiki, bila kujumuisha bonasi, sawa na Euro 40 milioni kwa mwaka, kulingana na mtandao wa Capology.
1. Riyad Mahrez (Algeria / Al-Ahli)
Mwishoni, mchezaji anayelipwa zaidi Afrika mwaka 2025 ni Riyad Mahrez.
Alipata umaarufu baada ya kujiunga na Leicester City, ambako alifunga mabao 39 na kutoa asisti 26 katika mechi 139 na kushinda Ligi Kuu England msimu wa 2015–16, jambo lililomfanya ashinde tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka wa Kulipwa.
Baadaye alijiunga na Manchester City kwa Pauni 60 milioni na kushinda taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya na mataji matano ya Ligi Kuu England kati ya 2018–2023 kabla ya kuhamia Al-Ahli.
Kwenye timu ya taifa, aliiongoza Algeria kushinda AFCON na kushinda tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka wa Afrika 2017. Mahrez analipwa takribani Euro 52.2 milioni kwa mwaka, sawa na Euro 865,495 hadi Euro 1 milioni kwa wiki.