Mastaa wamwangukia Bruno Man United

Muktasari:
- Licha ya kukosolewa vikali kufuatia kipigo cha fainali ya Europa League dhidi ya Tottenham, Fernandes bado anachukuliwa kama mchezaji pekee wa kiwango cha dunia ndani ya kikosi hicho cha Man United.
MANCHESTER, ENGLAND: WACHEZAJI wa Manchester United wanadaiwa kumuomba kapteni wa timu hiyo, Bruno Fernandes abaki, baada ya ripoti kufichua kwamba staa huyo anaweza kuondoka katika dirisha hili kuhamia Saudi Arabia kujiunga na Al-Hilal.
Licha ya kukosolewa vikali kufuatia kipigo cha fainali ya Europa League dhidi ya Tottenham, Fernandes bado anachukuliwa kama mchezaji pekee wa kiwango cha dunia ndani ya kikosi hicho cha Man United.
Al-Hilal wanaripotiwa kuwa tayari kulipa hadi Pauni 100 milioni kwa ajili ya kumsajili Fernandes, mwenye umri wa miaka 30, pamoja na mshahara wa pauni 700,000 kwa wiki, ofa ambayo inaonekana kuwa ni ngumu kuikataa.
Kutokana na a hali ya kifedha ya Man United kuwa mbaya, hasa baada ya kushindwa kufuzu Ligi ya Mabingwa jambo la kuuzwa kwa Fernandes linaweza kuwa suluhisho la kuingiza fedha kwa ajili ya ujenzi wa kikosi.
Baada ya mechi ya Europa, Fernandes alizungumza kwa uwazi kuhusu uwezekano wa kuondoka akisisitiza kwamba ni klabu ndio itaamua kama anapaswa kuondoka au kubaki.
“Kama klabu inaona huu ni wakati wa kutengana kwa sababu wanataka kupata fedha, basi iwe hivyo.”
Kauli hiyo, japo ilionekana ya kiungwana, imezua taharuki kubwa kambini, kwani wachezaji wenzake wanamwona Fernandes kama mchezaji muhimu anayeweza kuwabeba.
Chanzo cha kuaminika kimeeleza: “Bruno anakosolewa mara kwa mara lakini wachezaji wanajua ana kipaji cha kipekee. Anaweza kuwapa ubora mkubwa kiwanjani, lakini wote wanamheshimu na wamemtumia jumbe wakimwomba abaki.”
Kocha Ruben Amorim, ambaye ameshindwa kupata wastani wa hata pointi moja kwa kila mechi tangu achukue usukani, pia alidaiwa kuwa huenda akaondoka lakini sasa amewaambia wachezaji kwamba ataendelea kuwa kocha wa United msimu ujao.
Al-Hilal wanataka jibu kutoka kwa Fernandes kufikia wiki ijayo kuhusu kama atajiunga nao msimu huu wa kiangazi.
Kobbie Mainoo, kijana aliyechipuka kutoka akademi ya Carrington, naye yumo kwenye orodha ya mastaa wanaoweza kuuzwa.
Mchezaji mwingine anayetajwa kuondoka ni Alejandro Garnacho, ambaye inadaiwa kocha Amorim amemwambia atafute timu nyingine kwa msimu ujao.