Mastaa waliopiga bao 100 fasta Ligi Kuu England

Wednesday September 22 2021
MASTAA PIC

LONDON, ENGLAND. UKIWA na huduma ya Mohamed Salah kwenye kikosi chake, basi una uhakika wa mabao.

Supastaa huyo wa kimataifa wa Misri, Mo Salah amewasha moto huko Anfield, akiwa mtambo wa mabao wa miamba ya soka England, Liverpool.

Bao lake alilofunga dhidi ya Leeds United uwanjani Elland Road, imemfanya Mo Salah kuweka rekodi ya kufikisha mabao 100 kwenye Ligi Kuu England baada ya kucheza mechi 162.

Wakati Mo Salah akifikisha mabao 100 kwenye Ligi Kuu England baada ya kucheza mechi 162, jambo hilo limemwingiza kwenye orodha ya mastaa waliofikisha mabao 100 haraka kwenye mikikimikiki ya ligi hiyo.

Mastaa wengine walioingia kwenye orodha ya kufunga mabao 100 fasta kwenye Ligi Kuu England hawa hapa.


Advertisement

Alan Shearer- mechi 127

Anakuwa mchezaji wa kwanza kuweka historia Ligi Kuu England ya kufunga mabao 100 katika michezo 127 tu alizocheza tofauti na Salah aliyecheza michezo 162.

Shearer alifikisha idadi hiyo ya mabao akicheza timu za Blackburn Rovers na Newcastle, ambayo haijawaji kuvunjwa na mchezaji yoyote.


Harry Kane

– mechi 141

Kane, nyota wa mabao wa Tottenham alifanya hivyo ndani ya misimu sita aliyocheza akifunga mabao hayo 100 katika mechi 141 alizocheza. Alihitaji mechi nyingi zaidi kufikisha idadi hiyo ukilinganisha na Shearer.


Sergio Aguero

- mechi 147

Nyota wa zamani Manchester City ambaye anaichezea Barcelona kwa sasa, alifunga mabao 100 ndani ya misimu mitano aliyocheza Etihad akiwa amecheza mechi 147, ikiwemo kubeba mataji mawili ya Ligi Kuu England.


Thierry Henry – mechi 160

Licha ya kufunga mabao 100+ Ligi Kuu England, mkongwe huyu alishindwa kufunga mabao katika mechi zake nane za kwanza alizocheza Arsenal, lakini baadaye kiwango chake kikaimarika.

Henry alifunga mabao 24+ ndani ya msimu sita aliyocheza akiwa Arsenal, ikiwemo kubeba kiatu cha dhahabu cha mfungaji bora mara nne mfululizo.


Robbie Fowler -

mechi 163

Mkongwe mwingine aliyeweka rekodi ya kufunga mabao 100 ya Ligi Kuu England mapema zaidi ni Robbie Fowler, aliyefanya hivyo baada ya kucheza mechi 163.

Fowler anakuwa mchezaji wa sita kwenye orodha hiyo ya mabao akipita kwenye timu za Liverpool, Leeds United, Manchester City, na Blackburn Rovers.


Les Ferdinand –mechi 178

Ili kufikisha mabao 100, Ferdinand alicheza mechi 178 za Ligi Kuu ya England akipita timu za QPR, Newcastle United, Tottenham Hotspur, West Ham United, Leicester City, Bolton Wanderers.

Aidha, Ferdinand alikuwa na rekodi nzuri ya mabao Newcastle kuanzia mwaka 1996 hadi 1997, akifunga mabao 41 katika mechi 68 alizocheza.


Andy Cole – mechi 185

Cole alicheza mechi 185 akiwa na timu saba tofauti za Ligi Kuu England ndio akafikisha idadi ya mabao 100 akipitia timu za Newcastle United, Manchester United, Blackburn Rovers, Fulham, Manchester City, Portsmouth, Sunderland.

Cole alikuwa kinara wa mabao alipokuwa akicheza Man United akiwa na kumbu-kumbu ya kucheka na nyavu mara 93 akiwa na klabu hiyo na kubeba mataji kadhaa ya Ligi Kuu England.


Michael Owen – mechi 185

Michael Owen ni kati ya wachezaji bora waliopata kukipiga kwenye Ligi Kuu England. Alitesa sana wakati anaichezea Liverpool. Mkali huyo wa kucheka na nyavu alihitaji mechi 185 kufikisha mabao 100 ya Ligi Kuu ya England. Mbali na Liverpool, Owen katika soka la England, alichezea Newcastle United, Manchester United na Stoke City.


Robin Van Persie-

mechi 196

Baada ya kufunga mabao 96 ndani ya miaka nane aliyocheza Arsenal, Robin Van Persie alikuwa anahitaji mabao manne tu kufikisha mabao 100 ya Ligi Kuu ya England kabla ya kutimka na kwenda kujiunga na miamba ya EPL, Manchester United mwaka 2012.

Van Persie ana kumbumbu nzuri ya ‘hat-trick’ aliyofunga kwenye mechi Man United ilipomenyana na Southampton na kuipa ushindi wa mabao 3-2, iliyoenda sambamba na rekodi hiyo akifanya hivyo mwaka 2013.


Advertisement