Mastaa NBA wanaobeba timu mabegani 2025
Muktasari:
- Lakini ni nani ndiye mchezaji bora zaidi katika mpira wa kikapu duniani kwa sasa? Wakati Michael Jordan, Kobe Bryant na Kareem Abdul-Jabbar wanatawala mijadala ya wachezaji bora wa NBA wa wakati wote, majina hayo hayapo tena uwanjani.
MIAMI, MAREKANI: VICTOR Wembanyama, LeBron James na Stephen Curry wanapambana kuwa mchezaji bora zaidi wa mpira wa kikapu duniani. Wachezaji hao wa Ligi ya Kikapu Marekani (NBA) ni miongoni mwa wanamichezo bora duniani kwa sasa. Kuorodheshwa miongoni mwa bora zaidi katika ligi ni kuwa juu ya mlima wa mpira wa kikapu.
Lakini ni nani ndiye mchezaji bora zaidi katika mpira wa kikapu duniani kwa sasa? Wakati Michael Jordan, Kobe Bryant na Kareem Abdul-Jabbar wanatawala mijadala ya wachezaji bora wa NBA wa wakati wote, majina hayo hayapo tena uwanjani.
Awali, wachezaji warefu walikuwa kila kitu katika kikapu, lakini kuna baadhi ya mastaa wakubwa hawajawahi kushinda ubingwa licha ya kwamba wamewahi kutamba vilivyo.
LeBron James, Stephen Curry na Kevin Durant bado wanacheza mchezo huo unaodaiwa kwamba umeingia katika zama mpya kama ilivyo soka. Lakini, Wembanyama anaendelea kuibadilisha NBA akiipa upya kutokana na staili ya uchezaji wake hususan anapodanki, kushambulia na kutoa asisti, huku Shai Gilg-eous-Alexander ndiye MVP mpya wa msimu uliopita na mshindi wa fainali iliyopita ilhali Luka Doncic ni ‘uso mpya’ wa Los Angeles Lakers katika uchezaji timu akipigiwa upatu wa kunyakua u-MVP msimu huu.
Wamekuwa sehemu magumu zaidi ya mafanikio ya timu na wao pia. Tayari wana nyuso za kubeba timu zao baada ya LeBron,†mwandishi wa NBA, Marc Stein aliiambia talkSPORT katika moja ya mahojiano juu ya ubora wa wachezaji wa NBA msimu huu.
Alperen Sengun, Jimmy Butler, Zion Williamson, Paolo Banchero, Evan Mobley, Bam Adebayo na Trae Young ni wakali wapya wanaotarajiwa kuonekana katika orodha kutokana ubora wao. Jayson Tatum, Tyrese Haliburton, Kyrie Irving na LeBron wapo sana. Hii ndiyo orodha ya talkSPORT ya wachezaji bora wa NBA 2025/26.
Lauri Markkanen (Utah Jazz)
Mchezaji mwenye futi 7 kutoka Finland anarudisha matumaini kwa Jazz. Timu hiyo ilishinda mechi 17 pekee msimu uliopita na kuwa na rekodi mbaya zaidi kutoka Ukanda wa Magharibi. Kabla ya msimu huu, Markkanen alihusishwa na uhamisho kwenda Golden State Warriors. Tayari ameshajibu kuwa wa sita kwa wastani wa pointi (28.3) na kuiweka Jazz kwenye nafasi nzuri katika mbio za mchujo (play-in) za Magharibi.
Austin Reaves (Los Angeles Lakers)
Nani asiyetaka kumuona LeBron James Lakers? Mbali ya mkongwe huyo kuna mchezaji asiyechaguliwa kutoka Arkansas, Reaves mwenye rekodi za juu katika takwimu nyingi na wastani wake wa pointi 28.3 ni wa kushangaza. Reaves amegeuka kuwa chaguo la pili la ufungaji wakati LeBron akiwa majeruhi, na amekuwa mchezaji bora anayemsaidia Luka Doncic katika nyakati ngumu.
Chet Holmgren (Oklahoma City Thunder)
Shai Gilgeous-Alexander (SGA), anapata sifa nyingi kikosini, lakini Holmgren ni staa mmwenye umuhimu katika timu hiyo. Akiwa na futi 7 na inchi 1 aling’ara katika Chuo Kikuu cha Gonzaga kabla ya kuumia msimu wake wa kwanza. Alimaliza nafasi ya pili kwenye ‘Rookie of the Year 2023–24’ na alishinda ubingwa akiwa na Thunder mwaka jana. kwa sasa ana rekodi ya wastani bora wa pointi (18.7) na ribaundi 8.2.
Pascal Siakam (Indiana Pacers)
Siakam alitaka awe ‘mchungaji’ kanisani. Badala yake akiwa na futi 6 na inchi 8 amekuwa staa na bingwa NBA mwenye thamani ya Dola 230 milioni. Msimu uliopita nusura ashinde taji lake la pili. Kwa sasa ana wastani bora katika uchezaji kikapu akiwa na pointi 24.6.
Anthony Davis (Dallas Mavericks)
Davis ni tishio. Uhamisho wake kwenda Dallas ulitikisa NBA msimu huu. Alicheza vizuri mechi yake ya kwanza, lakini akakumbwa na jeraha. Alikuwa wa tano kwa kipimo cha ufanisi wa mchezaji (PER) msimu uliopita kwa alama 26.3.
PER inajumuisha takwimu nyingi kama pointi alizofunga, ribaundi, asisti, kupora mipira (steals), kuzuia (blocks),
makosa aliyofanya (turnovers). Kwa kifupi, kadri PER inavyokuwa kubwa ndivyo mchezaji alivyocheza vizuri zaidi kulingana na muda aliokuwepo uwanjani.
Cade Cunningham (Detroit Pistons)
Mteule namba moja wa drafti 2021 anayekua haraka. Detroit ilimaliza kwa ushindi wa 44–38 msimu uliopita na kuepuka mchujo (play-in), hasa kwa sababu ya Cade. Alifikia wastani wa juu wa pointi 26.1 na asisti 9.1, na akawa ndiye staa wa Pistons.
Jaylen Brown (Boston Celtics)
Trae Young wa Atlanta Hawk ana takwimu, lakini Brown ni bora Celtics. Ikumbukwe Brown ni bingwa na pia ameshinda ‘finals MVP’ na ni nguzo muhimu Celtics. Msimu huu amekuwa akiibeba timu wakati Jayson Tatum akiuguza jeraha.
Devin Booker (Phoenix Suns)
Alikuwa karibu kuwa mchezaji bora NBA msimu uliopita. Anatajwa kuwa na moyo wa ushindani na ni mmoja wa wa wachezaji bora katika kuzuia. Lakini, Phoenix bado ina maswali juu yake msimu huu, na Booker bado anasubiri taji lake la kwanza.
Jalen Brunson (New York Knicks)
Kutoka kuchaguliwa raundi ya pili (kwenye drafti 2018), hadi kuwa tegemeo la Knicks kaushangaza ulimwengu wa kikapu. Jalen alimaliza tano bora kwenye MVP 2023/24, lakini sasa kwa kuwa staa wa kikosi anatakiwa kuwa imara zaidi msimu huu na tayari keshaanza kuonyesha vitu vyake uwanjani.
Kevin Durant (Houston Rockets)
Hakuna anayepinga kipaji bora cha mkongwe Durant ambaye tayari keshavuka pointi 30,000, na keshashinda medali nne za dhahabu Olimpiki. Kwa sasa yupo zake Houston akipambana kuirudisha timu fainali baada ya miaka 30. Kuna mambo anafanya uwanjani yanayosaidia kuamua mechi.
Stephen Curry (Golden State Warriors)
Kama ni kwenye soka ingeelezwa kwamba huyu ni mshambuliaji bora zaidi wa muda wote na bado yupo juu. Lakini, timu yake haipo katika ubora uliozoweleka kama zamani. Amefunga pointi zilizotokana na ‘three-pointers’ zenye jumla ya pointi 4,000, lakini analenga kunyakua taji msimu huu.
Karl-Anthony Towns (New York Knicks)
Ushirikiano wake na Brunson uliwapeleka Knicks fainali za Kanda Mashariki msimu uliopita. Kwa sasa anaendelea kupanda katika mlima wa NBA, lakini keshaonyesha msimu huu utakuwa bora kwake.
Tyrese Maxey (Philadelphia 76ers)
Msimu huu anashika nafasi ya tatu kwa pointi (32.1), akiwa anaibeba timu mabegani licha ya Joel Embiid kuwa katika kiwango kibovu.
Donovan Mitchell (Cleveland Cavaliers)
Baada ya kuondoka Utah, Mitchell amekuwa bora zaidi akiwa na wastani wa pointi 30.4.
Anthony Edwards (Minnesota Timberwolves)
Edwards maarufu kama Ant-Man ameichukua timu mikononi mwake. Amewahi kufika fainali za Kanda ya Magharibi mara mbili mfululizo. Anachohitaji kwa sasa ni kupanda hadi fainali kubwa.
Luka Doncic (Los Angeles Lakers)
Akiwa fiti mchezoni hutoa burudani uwanjani akizunguka uwanja mzima kusaka ushindi wa timu. Kwa sasa amepungua uzito na yupo tayari kulipiza kisasi baada ya kuachwa na Dallas msimu huu. Ana wastani wa pointi 43 anapokuwa fiti na hilo linatarajiwa kujitokeza zaidi 2025/26.
Victor Wembanyama (San Antonio Spurs)
Wembanyama yupo katika msimu wake mwingine bora zaidi tangu alipotua Spurs 2023. Mchezaji huyo mrefu zaidi anatajwa kuwa mtulivu kusoma mchezo. Ana wastani wa pointi 50, na Spurs sasa inashinda tu. Msimu huu anaweza kuibuka MVP na Mchezaji Bora wa Ulinzi wa Mwaka.
Shai Gilgeous-Alexander (Oklahoma City Thunder)
Hii ni mashine ya kufunga pointi na MVP wa msimu uliopita. Aliiongoza Thunder kushinda mechi 68 na ubingwa wa NBA msimu uliopita. Amesaini mkataba wa Dola 285 milioni hivi karibuni na kwa sasa timu inategemea zaidi uwepo wake uwanjani.
Giannis Antetokounmpo (Milwaukee Bucks)
Katika ulimwengu mwingine Giannis angekuwa staa namba moja. Lakini, mustakabali wake Milwaukee ni mgumu kwani licha ya kuwa na wastani wa pointi 33.4 na ribaoundi 11.9 pamoja na kufanya maajabu kila siku ya mechi usiku uwanjani, lakini kikosi chao hakipo vizuri sana. Kwa upande wake namba zinambeba kwani kila eneo anapeta msimu huu.
Nikola Jokic (Denver Nuggets)
Usibishe! Jokic ni bora duniani. Ana rekodi ya kwanza ya 30-20-20 katika historia ya NBA yaani pointi 30+, ribaundi 20+ na asisti 20+ katika mchezo mmoja. Huyu ni MVP mara tatu na mchezaji mwenye ufundi wa kipekee. Amefunga pointi 55 katika mitupo 18 kati ya 23 ndani ya dakika 34.