Mastaa Chelsea warejea

New Content Item (1)
New Content Item (1)

LONDON, ENGLAND.MASTAA wa Chelsea, Ben Chilwell na Reece James wamerejea rasmi na tayari wameanza mazoezi na wachezaji wenzao wapya waliosajiliwa dirisha dogo la usajili akiwemo Mykhailo Mudryk.

Chilwell alianza mazoezi kwa mara ya kwanza tangu alipopata majeraha mwishoni mwa mwezi wa Oktoba mwaka jana.

Aidha kwa upande wa James yeye ataendelea kukaa nje ya dimba licha ya kuanza mazoezi na wachezaji wenzake, imeelezwa beki huyo atakaa nje kwa muda wa mwezi mmoja zaidi.

Naye Ruben Loftus-Cheek alionekana mazoezini baada ya kupona majeraha yalikuwa yakimsumbua. Hiyo ni taarifa njema kwa Kocha Graham Potter kwa sababu kikosi chake kimesheheni wachezaji wengi majeruhi.

Chelsea imeweka rekodi ya kuwa na wachezaji wengi majeruhi kwenye kikosi katika historia ya klabu hiyo.

Lakini baada ya usajili wa wachezaji dirisha hili dogo, umechangamsha kikosi cha Potter aliyekuwa na presha kutokana na mwenendo mbaya wa timu.

Mudryk alijiunga na Chelsea kwa rekodi ya usajili iliyogharimu kitita cha Pauni 88 milioni akitokea Shakhtar Donetsk, aliungana na wachezaji wenzake kwenye Uwanja  wa Cobham unaotumiwa na The Blues kwaajili ya mazoezi.

Mudryk anaamini atacheza mchezo wa Ligi Kuu England dhidi ya Liverpool utakaochezwa kesho. 

Joao Felix alicheza mechi ya kwanza dhidi ya Fulham wiki iliyopita, lakini atakosa mchezo huo kutokana na adhabu ya kadi anayoitumikia na atakuwa nje ya dimba hadi mwezi ujao.

Potter alipata ushindi mmoja katika mechi 10 alipocheza dhidi ya Crystal Palace wikiendi iliyopita.